Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHEIN: MIMI NI RAIS...UCHAGUZI MWINGINE 2020


RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amefuta ndoto za Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ambaye amekuwa akitamba kwamba karibuni ataunda serikali, akisisitiza Uchaguzi Mkuu mwingine utafanyika mwaka 2020.

Dk Shein amesema kuwa yeye ndio Rais wa Zanzibar na kueleza kuwa hakuna Baraza la Wawakilishi linalovunjwa ndani ya mwaka mmoja na kiutaratibu baraza hilo huvunjwa baada ya miaka mitano kwa sheria, taratibu na kanuni zake.

Hivyo, Dk Shein aliwataka wananchi na wanaCCM kuepuka kauli za upotoshwaji zinazosambazwa mitandaoni.

Aliyasema hayo juzi kwenye Ukumbi wa CCM, Mkoa wa Mjini iliyopo Amani baada ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa vijana kwa ajili ya maandalizi ya Ligi ya Mpira wa Miguu kwa timu 18 za Unguja.

Dk Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar anayoiongoza yeye itaendelea kuwa madarakani na kueleza kuwa mazungumzo aliyoyafanya juzi kati yake na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni mazungumzo ya kawaida baada ya kumwita kwa lengo la kubadilishana mawazo na kueleza changamoto zilizopo katika majimbo yao.

Alisema akiwa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi pia, ni sehemu ya baraza hilo na kwenda kuzungumza na wajumbe wa baraza hilo sio jambo jipya kwani ameshawahi kufanya hivyo kutokana na taratibu na kanuni zilizopo.

Pamoja na hayo, aliwasisitiza wanaCCM na wananchi kuwa hakuna baraza linalovunjwa asubuhi hivyo kauli hizo zinazozungumzwa na zinazosambaa ni za upotoshaji na zisizo na ukweli.

Aidha, aliwaeleza wanaCCM wakiwemo vijana waliohudhuria katika hafla hiyo kuwa mihimili mitatu iliyopo ikiwemo Mahakama, Serikali na Baraza la Wawakilishi hakuna mhimili hata mmoja unaomshurutisha mwenziwe bali hufanya kazi kwa mashirikiano ya pamoja ili kufikia malengo yaliokusudiwa katika nchi.

Naye Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd alieleza kuwa uzushi unaosambazwa katika mitandao hauna maana na kueleza kuwa amepokea simu nyingi kutoka kwa wananchi kutokana na kauli hizo za mitandaoni ambazo si za msingi kuwa Dk Shein juzi alikabidhi nchi kwani maneno hayo hayakuanzajuzi, bali ni kawaida kwa wapinzani.

Hivyo aliwataka wanaCCM na wananchi kupuuza kauli hizo.

Maalim Seif aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kabla ya CUF kususia Uchaguzi Mkuu wa marudio wa Machi 20, mwaka jana, amekuwa akipita visiwani na kudai kuwa karibuni mambo yatakuwa mazuri na juzi katika mitandao ya kijamii, ikihusisha Dk Shein na mabadiliko makubwa katika uongozi wa Zanzibar.
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com