POLISI : TUMIENI SIMU ZENU ZA MKONONI KUREKODI MAKONDAKTA WAKOROFI



JESHI la Polisi mkoani Arusha limewahimiza abiria mkoani humo kutumia simu zao za mikononi kurekodi matendo na lugha chafu kutoka kwa makondakta na madereva wa daladala ambao ni kero katika safari.

Aidha, jeshi hilo limewaagiza makondakta na madereva wa daladala zinazofanya safari kati ya jiji hilo na viunga vyake, kuanza kutoa tiketi kwa abiria wao kuanzia leo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo ameyasema hayo wakati akihutubia katika maadhimisho ya Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra-CCC) yaliyofanyika Stendi ya Kilombero jijini hapa.

Alisema baadhi ya wamiliki wa daladala wamekuwa na tabia ya kutowapa madereva tiketi ili kuonesha namba ya gari na njia inayopita hali inayosababisha usumbufu kwa abiria wanapodai haki zao hususan daladala hizo zinapokatisha safari.

Kamanda Mkumbo alisema abiria wakitumia simu zao kurekodi mienendo michafu ya wahudumu wa gari hizo itakuwa rahisi kwa Jeshi hilo kufuatilia na kuchukua hatua stahiki kwa kuwa kuna ushahidi.

“Kuanzia kesho (leo) daladala zote zitoe tiketi kwa abiria ili linapotokea tatizo, iwe rahisi kuwachukulia hatua. Mmiliki asipotoa tiketi kwa ajili ya abiria, basi husika litachukuliwa hatua,” alisema.

Awali, Katibu wa Sumatra- CCC, Daniel Luka Daniel alisema Baraza hilo linatoa elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondari na msingi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani ili kutoa elimu kwa wanafunzi kujua haki zao sanjari na kutoa taarifa wanapoona wameonewa.

IMEANDIKWA NA VERONICA MHETA-HABARILEO ARUSHA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post