Mitandao ya mawasiliano ya kijamii kama vile Twitter, Facebook inasababisha watu wengi zaidi kuhisi wenye upweke , kulingana na wanasaikolojia wa Marekani.
Ripoti ya uchunguzi wao inasema kuwa masaa zaidi ya mawili ya matumizi ya mitandao ya kijamii kwa siku huongeza uwezekano mara dufu wa mtu kujihisi ametengwa na jamii.
Ripoti hiyo ya wanasaikolojia inadai uwezo wa kupata mawazo ya maisha ya watu wengine unaweza kusababisha hisia za wivu.
Utafiti huo pia uliangazia watu wanaotumia mitandao ya Instagram, Snapchat na Tumblr.
Ni muhimu kukumbuka kuwa yale unayoyashuhudia katika mitandao ya kijamii si sababu muhimu ya kukufanya ujihisi vibaya -lakini inaweza kuwa sababu.
Kwa maneno rahisi, yale unayoyashuhudia kwenye mitandao ya kijamii yanawezakuchochea hisia ambazo tayari unazo.
" Hatujatambua nini kinachokuja kwanza - matumizi ya mitandao ya kijamii ama dhana ya kuhisi umetengwa na jamii ," amesema Elizabeth Miller, profesa wa tiba ya watoto katika chuo kikuu cha Pittsburgh, ambaye ni mmoja waandishi wa utafiti.
" Inawezekana kwamba vijana ambao awali walihisi wametengwa na jamii walianza kutumia mitandao ya mawasiliano ya kijamii.
Ama inawezekana kwamba kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii kulisababisha kwa kiasi fulani kujihisi wametengwa na dunia halisi."
Nadharia za ripoti hiyo zinaelezea kwamba kwa jinsi unavyotumia muda mwingi kwenye mtandao wa kijamii, ndivyo unavyotumia muda mdogo kufikiria mawasiliani halisi ya dunia.
Matumizi ya mitandao ya mawasiliano ya kijamii pia yanaweza kusababisha hisia za kutengwa, kama vile kuona picha za marafiki zako wakifurahia tukio fulani ambalo wewe hukualikwa.
Wataalam hao wa Saikolojia waliwahoji watu wazima takriban 2,000 walio na umri wa miaka kati ya 19 - 32 kuhusu matumizi yao ya mitandao ya mawasiliano ya kijamii.
Profesa Brian Primack, kutoka Chuo Kikuu cha tiba cha Pittsburgh, alisema: " Hili ni suala muhimu kulichunguza kwasababu matatizo ya afya ya akili na kutengwa na jamii yamefikia katika viwango vya mlipuko miongoni mwa vijana.
" Sisi ni viumbe tulioumbwa kuishi kijamii, lakini maisha ya kisasa yanatufanya tutengane baada ya kutuleta pamoja.
"huku ikionekana kuwa mitandao ya kijamii inatoa fursa ya watu kuishi kama jamii, nadhani uchunguzi huu unaonyesha kuwa huwenda isiwe suluhu ambalo watu walilitegemea."
Wanasaikolojia wanasema matatizo ya afya ya akili na kutengwa na jamii yamefikia katika viwango vya mlipuko miongoni mwa vijana.
Chanzo-BBC