Baadhi ya wasanii wa kundi la Mama Ongea na Mwanao, waliokuwa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 za mgombea mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mama Samia Suluhu, wamekanusha madai ya kutolipwa wala kukidai chama hicho madeni yoyote wakati na baada ya kampeni hizo kumalizika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam leo, Makamu Mwenyekiti wa muda wa kundi hilo, Yobnesh Yusuph maarufu Batuli, alisema madai hayo si kweli kwani wasanii wote walilipwa na mikataba wanayo.
“Nikiwa kama Makamu Mwenyekiti wa ‘group’ hili la Mama Ongea na Mwanao kwa muda, ni kweli kuna uvumi ulienea katika mitandao kwamba wasanii tulioshiriki kampeni na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu hatujalipwa, si kweli nakanusha taarifa hizo kuwa si za kweli.
“Ingawa kwenye msafara wa mamba kenge hawakosekani, wapo wanaoshawishiwa kulichafua kundi letu, kumchafua Makamu wa Rais na kuichafua CCM, mimi nakataa, wasanii wote tulilipwa na mikataba ipo.
"Haiwezekani wewe staa mkubwa unakaa mbele ya vyombo vya habari unaongea uongo kwamba wasanii hatujalipwa wakati wewe ndiyo ulikuwa unawalipa hicho kitu hakiwezekani,” alisema Batuli aliyekuwa ameongozana na baadhi ya wasanii wa kundi hilo.
Hivi karibuni msanii nyota wa filamu na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu ambaye alitoka CCM na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema wasanii hao wanadai malipo yao ambapo hakutaja kiasi wanachodai na kwamba wamekuwa wakizungushwa pindi wanapoulizia madeni hayo.
Social Plugin