Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

EWURA : GESI IMESAIDIA SEKTA YA UMEME KUIMARIKA TANZANIA


Baadhi ya mitambo ya kuchakata gesi katika kituo cha Madimba mkoani Mtwara
*****
USAMBAZAJI wa umeme nchini kwa sasa unadhibitiwa na Shirika la Umeme (Tanesco) ambalo mmiliki wake ni Serikali.

Tanesco ndiyo wanaozalisha umeme, kuusafirisha na kuusambaza kwa wateja nchini. Huko Zanzibar pia, ni Tanesco ndio inayowapatia umeme. Wanaliuzia Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ambalo lenyewe linausambaza katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

Ripoti ya Ewura ya ukaguzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ya mwaka 2015/16 inaonesha katika uzalishaji, Tanesco inasaidiwa na wawekezaji binafsi waliogawanyika katika makundi matatu.

Wazalishaji hao ni kampuni binafsi kubwa zinazofua umeme yaani Independent Power Producer (IPPs), wazalishaji wadogo wa umeme (SPPs) na wazalishaji wa umeme wa dharura (EPPs).

Katika kundi hilo la wazalishaji, zipo kampuni 11 ambazo ni Tanesco, Songas, IPTL, Kampuni ya Mwenga, Kampuni ya kufua umeme ya Tanzania Wattle (TANWAT), Kampuni ya Tanganyika Planting (TPC), Ngombeni Power Ltd, Kampuni ya Kufua umeme wa maji ya Andoya, Kampuni ya Kufua umeme wa maji ya Tulila, Kampuni ya Kufua umeme ya Yovi na kampuni ya kufua umeme ya Darakuta.

Kadhalika, zipo kampuni zilizokuwa zinazalisha umeme ambazo kwa sasa mkataba wake na Tanesco umemalizika. Kampuni hizo ni Aggreko ambayo iliyokuwa inazalisha umeme wa dharura na mkataba wake umemalizika Machi 2016, pamoja na Symbion iliyokuwa inazalisha megawati 112 mkataba wake umemalizika Mei 24, 2016.

Kati ya kampuni hizo, kampuni mbili pekee ndizo zinazozalisha umeme na kusambaza ambazo ni Tanesco na Mwenga. Hata hivyo, usafirishaji wa umeme bado uko chini ya Tanesco. Kwa upande wa wazalishaji wadogo waliosajiliwa na Ewura ni kampuni ya kusambaza umeme vijijini ya Jumeme.

Kampuni hiyo kwa sasa inazalisha umeme na kuusambaza katika visiwa vilivyoko katika Ziwa Victoria vya Bwisya na Ukara katika Wilaya ya Ukerewe. Ewura pia imesajili wakandarasi mbalimbali wapatao 227. Katika mchanganuo huo katika mwaka unaoishia Juni 2016, Ewura ilipokea maombi 262 ya kampuni za wakandarasi wa umeme.

Kiwango hicho ni ongezeko la asilimia 25 ukilinganisha na maombi 209 yaliyopokewa mwaka ulioishia Juni 2015. Kati ya maombi hayo 269, waombaji 227 tu ndio waliokuwa na sifa zinazostahili na hivyo, kusajiliwa na Ewura. Waombaji 35 hawakupita kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo maombi yao kutokuwa na nyaraka muhimu pamoja na kuambatanisha vyeti vya kughushi.

“Ewura kwa kushirikiana na Tanesco tunasisitiza kuwa wakandarasi wa umeme wanaofanya shughuli zao nchini, wahakikishe kuwa wamepewa usajili, kinyume cha hivyo ni uvunjaji wa sheria,” inasema Ripoti hiyo ya Ukaguzi ya Mwaka ya Ewura.

Katika ukaguzi na ufuatiliaji wa usambazaji wa umeme, Ewura ilifanya ukaguzi katika mikoa 11 ambayo ni Singida, Mtwara, Shinyanga, Kilimanjaro, Geita, Tanga, Mbeya, Katavi, Rukwa, Kagera na Iringa.

Miongoni mwa kasoro walizobaini ni kuwepo maeneo ambako jenereta zinavuja oili na baadhi ya maeneo yana umeme wenye nguvu kidogo hali inayosababishwa na wateja kuwa wengi na transfoma kulemewa na mzigo. Ewura pia ilifanya ukaguzi wa awali kwa kampuni zilizotuma maombi ya kutaka kuzalisha umeme ambazo ni kampuni ya sukari ya Kilombero, kampuni ya kufua umeme ya Yovi na kampuni ya Darakuta.

Nyingine ni kampuni ya sukari ya Kagera, kampuni ya sukari ya Mtibwa, Kampuni ya Saruji ya Tanga, Kampuni ya Chokaa ya Maweni, Kampuni ya dhahabu ya Geita, Kampuni ya Nishati ya Ludewa, kampuni ya Fondazione ACRA-CCS na kampuni ya mafuta ya East Coast.

Ukaguzi huo ulihusisha nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa na waombaji hao wanaokusudia kuzalisha umeme wa megawati 1 kwa ajili ya matumizi yao wenyewe. Mamlaka hiyo ya udhibiti pia ilifanya ukaguzi wa ubora na viwango vya mitambo ya kufua, kusafirisha na kusambaza umeme.

Katika eneo hilo Ewura ilibaini kuwa kuwapo kwa umeme mdogo na kuwapo matukio ya kuzimika mara kwa mara kwa umeme kunatokana na miundombinu ya kusafirisha umeme kuchakaa na kutofanyiwa matengenezokwa muda mrefu. Kwa mujibu wa Ewura kiasi cha megawati 84 kinachozalishwa nchini kiko nje ya mfumo wa gridi ya taifa, wakati megawati 1,358 zinazozalishwa umeme wake unaingizwa katika gridi ya taifa.

Mahitaji ya umeme yaliyopo hadi Machi 15, 2016 yalikuwa ni megawati 1,026. Hadi Juni 2016 kiasi cha umeme kilichokuwa kimezalishwa ni GWh 6,449. Kiwango hicho ni ongezeko la asilimia 2.9 la kiasi cha umeme kilichozalishwa mwaka 2015 ambacho ni GWh 6,262.

Uniti hizo za umeme zilipokelewa na Tanesco kutoka kwa wazalishaji wakubwa (IPPs), Wazalishaji wadogo (SPPs) na umeme mwingine ulinunuliwa kutoka nchi jirani. Umeme unaotumika nchini kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Ewura unatokana na maji yanayochangia asilimia 31 ya uzalishaji, gesi asilia inayochangia asilimia 56 na mafuta yanayochagia asilimia 13.

Ongezeko hilo linatokana na kukamilika kwa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam linaloingiza gesi yake katika mitambo ya Kinyerezi I na katika mitambo ya gesi ya Tanesco iliyoko Ubungo.

Uzalishaji wa umeme wa maji unazidi kushuka, Ewura inaeleza kuwa hiyo inatokana na uhaba wa maji katika mito na mabwawa ambako kuna mitambo ya kufua umeme wa maji hasa kwa miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba 2015. Katika mwaka 2015/16 mitambo inayotumia mafuta ikiwemo ile ya dharura iliondolewa kutokana na ongezeko la umeme unaozalishwa na gesi.

Mitambo ya dharura ya Aggreko iliyokuwa inazalisha megawati 70 Ubungo na Tegeta imefikia kikomo. Umeme unaozalishwa kutokana na gesi asilia umeongezeka kutoka asilimia 41 hadi kufikia asilimia 56. Baada ya kusitishwa kwa mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura, mitambo iliyobaki ilitosheleza kuzalisha umeme kulingana na mahitaji ya sasa.

Hadi Juni 2016, wateja waliokuwa wameunganishwa umeme na Tanesco walikuwa ni 1,743,820 wakati mwaka 2015 wateja waliokuwa wameunganishwa walikuwa 1,502,474.

Kuongezeka kwa wateja waliounganishiwa umeme kumetokana na kuwapo kwa watu wanaounganishwa umeme kutokana na fedha za Mfuko wa Umeme Vijijini.

Kampuni ya kufua umeme wa maji ya Mwenga iliyoko wilayani Mfundi yenyewe imeunganisha wateja wapatao 1,826 ukilinganisha na wateja 1,312 wa mwaka 2015. Maoni ya Ewura ni kwamba kuna kuboreka kwa sekta ya umeme nchini na kwamba wawekezaji kwa sasa wameangalia zaidi katika utumiaji wa umeme utokanao na mionzi ya jua na ule unatokana na nishati jadidifu.

IMEANDIKWA NA SHADRACK SAGATI - HABARILEO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com