KAMPUNI YA BIA TBL YAPUNGUZA WATUMISHI WAKE 100 NDANI YA SAA 24


Kampuni ya Bia ya Tanzania Breweries (TBL), imepunguza watumishi wake takribani 100 ndani ya saa 24.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watumishi wa TBL, watumishi waliopunguzwa ni wale wa kitengo cha masoko.

Mtoa taarifa mmoja kutoka kwenye duru za uongozi wa TBL ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema kuwa uamuzi huo ulitekelezwa Jumatatu ya wiki hii.


Alisema sababu kuu ya kupunguza wafanyakazi hao ni kulinda uchumi wa kampuni baada ya mauzo ya bidhaa kuporomoka kwa kasi katika kipindi cha mwaka jana hadi mwaka huu.

Ofisa masoko mmoja wa kampuni hiyo ambaye hajakumbwa na panga la kupunguzwa kazi, alidokeza kwamba uamuzi huo unatokana na hali ya mauzo na uchumi wa kampuni kutokuwa rafiki.

Aliongeza kuwa uamuzi wa Serikali wa kuzuia biashara ya pombe kali zinazofungashwa kwenye mifuko ya plastiki(viroba) umeathiri kwa kiasi kikubwa soko la bidhaa yao aina ya Konyagi.

“ Wameachishwa kinyama sana, waliitwa siku ya Jumatatu na kuachishwa papo hapo(on spot), wakaambiwa wayaache magari yao na kusaini fomu ya kuondoka, miye kwa bahati nzuri nimepona. Na hili jambo la viroba ndio limepigilia msumali wa mwisho,” alisema ofisa huyo.

Msemaji wa Kampuni ya TBL, Georgia Mutagahwa alipotafutwa kwa ajili ya uthibitisho wa taarifa hiyo, hakupokea simu kila ilipopigiwa.

Chanzo - Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post