Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli, amefanya uzinduzi wa mabweni mapya ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, UDSM.
Rais Magufuli amesema kukamilika kwa mabweni hayo ya kisasa ndani ya kipindi chini ya miezi minane ni ishara kuwa Tanzania inaweza. “Tukiamua tunaweza tukafanya watu wakaona miujiza,” amesema.
Ameongeza kuwa wapo watu walibeza kuwa shilingi bilioni 10 zisingeweza kukamilisha ujenzi huo na kwamba hawakumiani kuwa yasingeweza kujengwa na Watanzania. Ameshauri kuwa mafanikio hayo yawe vifundisho kwa viongozi wa serikali kutotoa tenda kwa wakandarasi wa nje zenye gharama kubwa na kuwaacha wale wa ndani.
Kwa upande mwingine Rais amesema mabweni hayo yatalipiwa kwa shilingi 500 pekee, tofauti na 800 kwa mabweni mengine. Mabweni hayo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840.
Awali akizungumza kwenye uzinduzi huo, makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alissema mabweni hayo yana vitanda 1,920 vya double decker, makabati 1,920, shelves za vitabu 1,920, meza, 1,920, viti 3,840 magodoro 3,840.
“Tutahakikisha kuwa huduma zote muhimu kama vile cafeteria ya chakula, maduka kwaajili ya mahitaji mbalimbali, zahanati, salon, kituo cha polisi na nyinginezo vinapatikana hapa hapa,” alisema Profesa Mukandala.
Aliongeza kuwa ujenzi wa cafeteria umeshaanza na ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 500 kwa wakati mmoja. Amehakikisha kuwa chuo kimejipanga kuhakikisha kuwa mabweni yanatunzwa na tayari wameshampata msimamizi mkuu aliyepewa mafunzo maalum ya muda mfupi.
Prof Mukandala alimshukuru Rais Magufuli kwa namna alivyojitolea kuhakikisha mabweni hayo yanakamilika kwa kufuatilia kwa ukaribu kila hatua za ujenzi wake.
“Hili ni jambo kubwa sana na historia itaandikwa kwa herufi za dhahabu,” alisema.
Aliongeza kuwa wizara tatu zimehusika kwenye ujenzi wa mabweni hayo ambazo ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga taifa, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mawaziri wote wa wizara hizo Dr. Hussen Mwinyi, Profesa Makame Mbarawa na Profesa Joyce Ndalichako walikuwepo.