MADIWANI KAHAMA WATAKA SEKONDARI ILIYOTUMIA MIAKA 11 KUJENGWA IKAMILIKE

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kahama,Abel Shija
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga,wameamuru kukamilishwa mara moja kwa ujenzi uliotumia miaka 11 katika Shule ya Sekondari Kitwana,iliyoko Kata ya Busoka,ili kunusuru wanafunzi
kutembea umbali wa kilometa 15,kufuata masomo.

Maazimio ya Baraza hilo yalifikiwa juzi,baada ya Diwani wa Kata ya Busoka,Julius Malale,kuwasilisha malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Kitwana,wanaohitaji kurejeshewa maeneo yao waliyoyatoa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Kitwana,ambao umeshindikana kukamilika.


Katika malalamiko hayo,Wananchi hao wamedai hawaoni faida ya kuyatoa maeneo hayo na kuhitaji kurejeshewa,kutokana na kutokamilika ujenzi wake kwa miaka 11,huku Shule nyingine zilizoanza ujenzi wake hivi karibuni zikikamilika,ilhali vijana wao wakiendelea kuteseka kutembea umbali zaidi ya kilometa 15 kufuata shule katika kata jirani.


“…kuna shule zilizoanza ujenzi na Kitwana zimekamilika na kuanza kutumika,zingine ujenzi wake umeanza hivi karibuni nazo zinafanya kazi,sasa wana kijiji hao waliotoa maeneo hayo wanadai leo ni miaka 11,imeshindikana kumaliza ujenzi huo wa sekondari,warejeshewe maeneo yao,kwani hayana tija tena kwa elimu,” alisema Malale.


Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kahama mjini,Hamidu Kapama,aliliambia baraza hilo kutokamilika ujenzi kwa sekondari hiyo,ni uzembe uliosababishwa na halmashauri kupitia afisa elimu sekondari kwakuwa serikali imekuwa ikiongea bila utekelezaji suala ambalo linawakatisha tamaa wananchi. 


Akijibu malalamiko hayo Ofisa elimu sekondari,Anastazia Manumbu, aliliambia baraza hilo kuwa bado halmashauri inaendelea na mchakato wa ukamilishaji wa sekondari hiyo kwa kubainisha kwamba kwa kipindi hiki wanaendelea na ujenzi wa vyoo na nyumba ya mwalimu.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kahama,Abel Shija,alihitimisha mjadala na kuungwa mkono na madiwani wote kwa kumtaka Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Kapami,kuhakikisha Sekondari hiyo,inakamilika mapema iwezekanavyo, kwa kutumia mafungu ya dharura iwapo kama haikupangiwa bajeti.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post