Ikiwa ni siku ya tatu ya Bunge la Bajeti, jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, limeanza kusikika ndani ya mhimili huo wa dola baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kuhoji ukimya wa Serikali juu ya tuhuma za vyeti feki, kumiliki mali nyingi zisizoendana na kipato chake yakiwamo magari ya kifahari ya aliowatuhumu kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya na matumizi mabaya ya madaraka.
Akizungumzia suala la vyeti, alisema Serikali inaendesha uhakiki wa watumishi wa umma ikiwamo vyeti vya taaluma jambo ambalo ni jema, lakini ni muhimu kazi hiyo ikafanywa kwa weledi bila kuathiri masharti ya Ibara ya 13 (1) ya Katiba ya nchi inayoonya ubaguzi wa aina yoyote kwa mtu yeyote bila kujali cheo chake, kabila lake, dini yake, elimu yake na hata jinsia yake.
“Wapo Watanzania wengi waliochukuliwa hatua baada ya kukutwa na vyeti feki, lakini cha ajabu Rais ameendelea kumkingia kifua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye anashutumiwa kutumia cheti ambacho si chake na kushindwa hata kuamuru uchunguzi wa jambo hilo ufanyike, ni kitendo cha kufedhehesha sana kwani kinawagawa Watanzania.
“Ubaguzi wa namna hiyo unalifanya kundi fulani kujisikia wanyonge na hawana haki na kundi jingine kujisikia wao wana haki zaidi ya wengine. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutenda haki katika zoezi hili la uhakiki kwani limeshaanza kuonyesha dalili za ubaguzi na upendeleo na linaweza kusababisha matabaka ya watu katika taifa,”alisema Mbowe.
Kiongozi huyo alisema kambi yake inaunga mkono vita ya dawa za kulevya, lakini hivi karibuni vita hivyo vilichukua sura mpya baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwataja hadharani watuhumiwa wa dawa za kulevya.
“Kitendo cha kuwataja watu hadharani bila ushahidi wowote, kilifanywa kibabe kwa kuwakejeli, kuwadhihaki na kwa uonevu mkubwa kwakuwa hakukuwa na ushahidi wowote na pia mahakama haikuhusishwa katika hatua za awali. Hii ina maana kwamba mkuu huyo wa mkoa aliamua kuwa hakimu kwa kutumia cheo chake kuchafua majina ya watu na haiba waliyoitengeneza kwa muda mrefu na kwa gharama kubwa.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshangazwa sana na kitendo cha Rais kuendelea kumkingia kifua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam katika matukio tofauti tofauti, huku ushahidi wa wazi ukionyesha matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa haki za binadamu, umiliki wa mali ulio wa shaka, ikiwamo magari ya anasa ya wafanyabiashara aliowatuhumu kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, vitisho kwa vyombo vya habari, kuingilia uhuru wa habari nchini, matumizi mabaya ya rasilimali za nchi ikiwa ni pamoja na kufanya tafrija ya kutimiza mwaka mmoja kazini kwa kivuli cha kampeni ya kutokomeza dawa za kulevya.
“Ni jambo la kusikitisha sana kuona Rais akimtoa kafara waziri wake kwa gharama ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Tunajiuliza kuna jambo gani lililojificha baina ya Rais na Mkuu huyu wa Mkoa? Tatizo la madawa ya kulevya si tatizo la mtu mmoja na wala halihitaji kufanywa kama vita ya mtu binafsi.
“Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua Rais ana mamlaka ya kuteua na kutengua uteuzi, lakini hana mamlaka ya kumkingia kifua mtu yeyote pale anapovunja sheria za nchi, hata kama Rais ndie aliyempa dhamana. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inawataka viongozi wote waliopewa dhamana kuheshimu utu na haki za kila raia.
“Ugomvi binafsi, kutofautiana kiitikadi, kiimani na hata kimtazamo kusimfanye yeyote mwenye dhamana kutumia mamlaka yake katika kumwonea mtu yeyote. Kama taifa tuna jukumu la kusimamia misingi ya utu na kuheshimiana.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mheshimiwa Rais kumchukulia hatua za kinidhamu Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam. Aidha, Rais aache ubaguzi katika uamuzi wa kinidhamu kwa baadhi ya viongozi wa umma, kwani hii ni kuwa na ‘double standard’ katika utekelezaji wa majukumu yake,” alisema mbowe.
Social Plugin