MFANYABIASHARA WA KUKU ADAI ALISINGIZWA KESI YA MAUAJI KISA ANA VVU ASIWAAMBUKIZE


MFANYABIASHARA wa kuku, Michael Gadi (52) amedai kuwa baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ngulu Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro walimsingizia kesi ya mauaji baada ya kushindwa kumfukuza kwa kuhofia atawaambukiza Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Gadi alieleza hayo juzi mbele ya Jaji Patricia Fikirini wakati akijitetea dhidi ya mashitaka ya mauaji ya bila kukusudia yanayomkabili katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi. 

Akitoa ushahidi wake huku akiongozwa na Wakili Elikunda Kipoko, Gadi alidai kwa muda mrefu wanakijiji walikuwa wanafanya njama za kumuondoa, kwa sababu asiwaambukize VVU.

Wakili Kipoko: Mshitakiwa, kesi inayokukabili inasema ulimuua Michael Masanga kwa kumchoma kisu, ni kweli? Gadi: Siyo kweli

 Wakili Kipoko: Unaieleza nini mahakama kuhusu tuhuma hizo? Gadi: Sijafanya hilo kosa, unajua kijijini tunaishi kwa wivu na kwa muda mrefu, walikuwa wanafanya njama za kuniondoa kwa sababu ya maradhi yangu (VVU) wanaona nitawachafulia kijiji.

Katika utetezi wake, Gadi alidai kuwa Mei 18, 2014, alitoka Same na kurudi nyumbani saa 10 jioni, akapumzika ilipofika usiku alisikia kelele, akafungua dirisha na kuona watu wengi pamoja na askari wa mgambo wakimtaka afungue mlango lakini alikataa kufanya hivyo hadi balozi atakapofika. 

Aliendelea kudai baada ya balozi kufika alifungua mlango na askari walimkamata na kukagua ndani kwake, wakachukua kisu na kumpeleka katika kituo kidogo cha polisi cha Ngulu na baadaye alihamishiwa kituo cha Mwanga.

Gadi alidai baada ya siku tatu walimtoa kituoni na kumueleza wanakwenda nyumbani kwake kukagua tena, walipofika akawaambia hawezi kufungua mlango kwa sababu askari anayeitwa Samweli alichukua ufunguo wa nyumbani kwake.

 Alidai walimtafuta askari Samweli akawafungulia mlango “wakati wakiendelea kukagua nilisikia wakisema kisu hiki hapa kwenye godoro, wakaniuliza hiki kisu cha nani? nikawaambia siyo changu wamuulize aliyekuwa na ufunguo wa chumba changu”.

Katika ushahidi wake Gadi alikana maelezo aliyoyatoa kituo cha polisi pia alidai hajawahi kuzungumza na Masanga (marehemu) zaidi ya kujua jina lake.

 Baada ya kusikiliza ushahidi huo, Jaji Fikirini aliahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya pande zote mbili kuwasilisha majumuisho ya hoja, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi saba na mshitakiwa alijitetea mwenyewe.
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post