MOTO WATEKETEZA MABANDA 13 YA WAFANYABIASHARA WA MBAO SOKO LA KAMBARAGE SHINYANGA


Moja ya banda la kuuzia mbao katika eneo la Soko la Kambarage manispaa ya Shinyanga likiwa lote limeteketea kwa moto -Picha  kwa hisani ya Mtetezi wa Haki Blog
Askari wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani Shinyanga wakifanya juhudi za kuzima moto katika mabanda ya kuuzia mbao.
Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kikiendelea na kazi.

Moto ambao haikufahamika mara moja chanzo chake umeteketeza mabanda 13 ya wafanyabiashara wa mbao eneo la Soko la kata ya Kambarage manispaa ya Shinyanga na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.

Moto huo umetokea usiku wa kuamkia Jumamosi, Aprili 29, mwaka huu baada ya kulipuka katika moja mabanda yaliyopo katika eneo hilo na kusambaa kwenye mabanda jirani ambapo umeteketeza tani kadhaa za mbao za wafanyabiashara hao.

Hata hivyo juhudi zilizofanywa na askari wa kikosi cha Zimamoto na uokozi mjini Shinyanga ziliwezesha moto huo kutoleta madhara zaidi kutokana na eneo hilo kuwa na mabanda mengi ya wafanyabiashara wa mbao na mashine za kuchana na kuranda mbao.

Mmoja wa mashuhuda wa moto huo ambaye ni mlinzi katika moja ya mabanda yaliyopo katika eneo hilo, Faustine Mapuli alisema aligundua kuwepo kwa moto kwenye moja ya mabanda wakati alipokuwa akikagua lindo lake ambapo alipiga kelele na kuwaita wenzake walioanza kufanya juhudi za kuuzima kwa kumwagia michanga.

Hata hivyo alisema walipoona moto bado unazidi kuendelea kuwaka waliamua kutumia pia maji jambo ambalo lilisababisha moto ulipuke kwa kasi zaidi na ikawabidi kuwapigia simu waajiri wao ambao ndiyo wamiliki wa mabanda na wao walipiga simu ofisi ya Zimamoto kuomba msaada wa gari la kuzimia moto.

Aliendelea kueleza kuwa pamoja na kufika kwa gari la zimamoto tayari moto ulikuwa umeishasambaa eneo la vibanda vingi na kuteketeza kabisa mbao nyingi, mashine za kupasua na kurandia zilizokuwemo katika vibanda hivyo.

Mmoja wa wamiliki wa mabanda hayo, Moses Mizungu alisema baada ya kupata taarifa za kutokea kwa kwa moto katika eneo hilo mnamo saa sita usiku.

alisema baada ya kupokea taarifa hizo mara moja alipiga simu katika ofisi za Zimamoto lakini hata hivyo alipofika eneo la tukio alikuta tayari moto umeteketeza eneo la vibanda vingi ikiwemo mali zake zote zilizokuwa ndani ya kibanda chake.

Kwa upande wake kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokozi mkoani Shinyanga Ndeto Malisimba, ametoa lawama zake kwa walinzi wanaolinda mabanda hayo ambao walichelewa kutoa taarifa za kuwepo kwa moto hali iliyochangia moto uteketekeza eneo kubwa.

Malisima alisema iwapo taarifa zingetolewa mapema huenda hasara iliyosababishwa na moto huo isingekuwa kubwa kiasi kinachokisiwa hivi sasa kupatikana.

Chanzo cha moto huo bado kinachunguzwa.

-Picha na habari kwa hisani ya Mtetezi wa Haki Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post