Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ORODHA YA VYUO VIKUU 10 VIKONGWE ZAIDI DUNIANI

Taasisi mbalimbali za Elimu zimekuwa zikishindana kujenga misingi imara ya elimu bora kwa lengo la kujihakikisha ubora zaidi kwa taasisi husika jambo linaloongeza ushindani hasa kwenye elimu za juu ambapo Vyuo Vikuu vimekuwa vikijengwa na vile vya awali vikiboreshwa zaidi.

Nimekusogezea orodha ya Vyuo Vikuu vikongwe zaidi duniani ambavyo vinaendelea kutoa huduma zake hadi sasa.

10. Chuo Kikuu cha Siena, Italia – 1240

Ni miongoni mwa Vyuo Vikuu vya kale zaidi katika historia ya Vyuo Vikuu duniani kikiwa Chuo Kikuu cha kwanza kuhudumia jamii nchini Italia ambapo kilianzishwa mwaka 1240 kikijulikana kwa jina lake la asili la Studium Senese. Chuo hiki sasa ni maarufu kwa kuwa na School of Law na School of Medicine na kikiendelea kudahili wanafunzi.


9. Chuo Kikuu cha Naples, Frederico II, Italia – 1224

Chuo Kikuu hiki kikongwe kilianzishwa na Kiongozi wa Kirumi Frederick II ili kuleta ushindani na Chuo Kikuu cha Bologna ambapo aliwalazimisha watu waliokuwa chini yake kutojiunga na Chuo Kikuu kingine zaidi ya hiki. Tangu hapo kimekuwa kikidahili wanafunzi hadi wakati huu huku kikitajwa kuwa moja ya Vyuo Vikuu mashuhuri zaidi kwenye masuala ya Utafiti nchini Italia.


8. Chuo Kikuu cha Padua, Italia – 1222

Kinatajwa kuwa moja ya Vyuo Vikuu vinavyovutia sana ambapo kilianzishwa mwaka 1222 na zaidi ya wanafunzi 1,000 wengi wao wakihamia kutoka Chuo Kikuu cha Bologna. Kilijulikana kama Chuo Kikuu kinachoendeshwa na wanafunzi ambapo wanafunzi wake ndiyo waliwachagua Maprofesa na kuwapangia mishahara.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliopitia kwenye Chuo Kikuu hiki ni pamoja na Galileo. Sasa kinatajwa kuwa moja ya Vyuo Vikuu bora Duniani.


7. Chuo Kikuu cha Cambridge, England – 1209

Kinatajwa kuwa moja ya Vyuo Vikuu vikongwe zaidi na vyenye hadhi kubwa. Kilianzishwa na kundi la wanachuoni ambao walikimbilia Cambridge, England wakitokea Chuo Kikuu cha Oxford baada ya kuwa na migongano na watu wa Oxford. Kinasifika kwa kutoa elimu bora na kitaaluma hakijawahi kutoka nje ya top 5 ya Vyuo Vikuu bora duniani.


6. Chuo Kikuu cha Paris, Ufaransa – 1160

Chuo hiki ndiyo sababu kubwa ya kuutambua mji wa Paris kama mji mkuu wa Ufaransa. Karne ya 13 kilinufaika na upendeleo uliotolewa kwa wanafunzi na wahadhiri wake uliotolewa na watawala wa Ufaransa na kuwa huru kinachojitegemea. Miongoni mwa masomo ya mwanzo yaliyofundishwa ni Theologia yakifuatiwa na Sanaa, Masuala ya Dawa na masomo ya sheria ya dini (Ukatoliki).

Chuo Kikuu cha Paris kinatajwa kuwa kituo cha Utamaduni na Sayansi barani Ulaya.


5. Chuo Kikuu cha Salamanca, Uhispania – 1134

Chuo Kikuu cha Salamanca kilianzishwa mjini Salamanca, Uhispania mwaka 1094 na kilipewa hadhi mwaka 1164 na Mfalme Alfonso IX ambapo moja ya vitu vinavyofurahisha ni eneo kinapopatikana ambalo linatajwa kuwa Urithi wa Dunia chini ya UNESCO.

Kinasifika kutokana na uwepo wa Idara ya Humanitia hasa katika masomo ya lugha.


4. Chuo Kikuu cha Oxford, England – 1096

Katika list hii kinakamata nafasi ya nne kikianzishwa mwaka 1096 katika mji wa Oxfordshire, England. Karne ya 13 masomo ya theologia yalikuwa kitovu kikubwa wakati masomo ya Sayansi yakianza kufundishwa mwishoni mwa karne ya 17.

Shrika la Uchapishaji la chuo hiki ‘Oxford University Press’ lilianzishwa chuoni hapo mwaka 1478 na miongoni mwa wanachuoni mahiri waliozalishwa na Oxford ni pamoja na Mwanafizikia Robert Boyle, mtaalamu wa masuala ya Nyota Edmond Halley, na waandishi mashuhuri kama Lewis Carroll na C.S. Lewis, Mawaziri Wakuu 26 wa Uingereza na washindi 27 wa Tuzo ya Amani ya Noble.


3. Chuo Kikuu cha Bologna, Italia – 1088

Kipo katika mji wa Bologna, Italia kikiwa moja ya Vyuo Vikuu vya mwanzo kabisa ambavyo vimedumu hadi sasa. Katika karne za 12 na 13 chuo hiki kilidahili wanafunzi kutoka kila kona ya Ulaya ambapo masomo ya sheria ya nchi na dini yakifundishwa kwa wingi. Karne ya 13 palianzishwa Kitivo cha Medicine na wanawake walianza kupata udahili karne za 17 na 18.

Kwa sasa Chuo Kikuu cha Bologna kinadahili zaidi ya wanafunzi 85,000 katika shule zake 11.


2. Chuo Kikuu cha Al-Azhar, Misri – 970

Chuo Kikuu cha Kiislam kilichoanzishwa mwaka 970 ambapo masomo mengi yanayofundishwa katika Chuo hiko yanatokana na Qur an hasa Sheria ya Kiislam ambapo pia vitivo vya Medicine na Engineering yakianzishwa miaka ya hivi karibuni, 1961.


1. Chuo Kikuu cha Al-Quaraouiyine, Morocco – 859

Kinapatikana katika mji wa Fes, Morocco kikijulikana pia kama Al Quaraouiyine ambapo kwa mujibu wa UNESCO na Guinness World Records ndiyo Chuo Kikuu kikongwe zaidi duniani ambacho kinaendelea kutoa huduma kama kawaida.

Kilianzishwa mwaka 859 na Fatima al-Fihri, binti msomi wa mfanyabiashara tajiri wa Kiislamu ambapo sasa kinatajwa kuongoza miongoni mwa Vyuo Vikuu katika Ulimwengu wa Kiislam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com