Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATOA TAMKO WAANDISHI WA HABARI KUSHAMBULIWA VURUGU ZA MKUTANO WA CUF

Serikali imepokea kwa masikitiko taarifa za kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya waandishi wa habari katika mvutano uliotokea juzi jijini Dar es Salaam kati ya wafuasi wa pande mbili zinazokinzana za Chama cha Wananchi (CUF). Tumechukua muda kidogo kulifuatilia suala hili na kubaini licha ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti polisi, wapo waandishi ambao vifaa vyao vya kazi pia vililengwa katika shambulizi hilo.



Tunachukua fursa hii kulaani kitendo cha kuumizwa wanahabari tena waliokuwa wamealikwa kuhudhuria mkutano huo. Ifahamike kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii.


Kifungu cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwepo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa. Misingi ya uhuru huu wa kitaaluma pia imesisitizwa katika Ibara za 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu imeuridhia.


Tunawatakia nafuu ya haraka wanahabari waliojeruhiwa na wenzao wengine waliopatwa na jakamoyo katika tukio hilo. Kwa kuwa suala hili tayari limeripotiwa polisi, tunawaomba wadau wote wa habari na wanasiasa kwa sasa kutulia na kuviachia vyombo husika vilifanyie kazi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.


Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com