WATU wanaokunywa pombe kupita kiasi wapo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya Kifua Kikuu (TB) kuliko wale wanaokunywa kwa kiasi, imebainishwa.
Kundi jingine lililopo katika hatari ya kupata ugonjwa huo ni lile la wavuta sigara na wanaojidunga na kuvuta dawa za kulevya.
Mratibu wa Kifua Kikuu (TB) na Ukoma, Mkoa wa Ki-TB Ilala II na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Mary Kajiru, alisema hayo jana alipozungumza na MTANZANIA Jumapili katika mahojiano maalumu.
“Mara nyingi utakuta wanakunywa pombe kupindukia, wanaojidunga dawa za kulevya na waovuta sigara hupendelea kukaa au kuishi ‘geto’, wengi huwa na lishe duni, huwa wanakosa hamu ya kula kutokana na ule ulevi, hivyo miili yao huwa dhaifu, hukosa virutubisho vinavyohitajika.
“Kwa kuwa miili yao huwa dhaifu, hali hiyo huchochea uwezekano wa kushambuliwa na magonjwa mbalimbali ikiwamo TB,” alisema.
Alisema wale wanaovuta sigara moshi unaoingia ndani ya miili yao huenda moja kwa moja kwenye mapafu na kufanya uharibifu.
“Kuna TB za aina mbili, ya mapafu na ile iliyo nje ya mapafu, TB ya mapafu ni hatari zaidi, kwani vimelea hutoka nje pindi mtu mwenye maambukizi anapokohoa na kusambaa kwa wingi hewani, huwa ni zaidi ya mamilioni ya bakteria,” alisema.
Alisema kundi jingine ni lile la watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU), wanaoishi kwenye msongamano kama vile sokoni, kwenye daladala, wazee wenye miaka zaidi ya 65, watoto chini ya miaka mitano, nao wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya TB,” alisema.
Aliongeza: “Kundi lingine ni watu wenye magonjwa ya muda mrefu kama vile kisukari, saratani na mengineyo, lakini hawa ni kwa kiwango kidogo.”
Alifafanua kwamba, TB ni ugonjwa ambao husababishwa na vimelea aina ya bakteria aitwaye mycobacterium tuberculosis.
“Mara nyingi huwa si rahisi kumuona bakteria huyo kwa macho hadi tutumie hadubini,” alisema.
Alitaja dalili za mtu mwenye maambukizi ya TB kuwa ni kukohoa, homa za mara kwa mara, kutokwa jasho jingi kuliko kawaida hasa usiku, kupungua uzito na kutoa makohozi yaliyochanganyika na damu.
“Watu wanapoona dalili hizi wawahi hospitalini, matibabu ni bure, wasikimbilie tu kununua dawa, wengi hufika hospitalini wakiwa wamechelewa,” alisema.
Na VERONICA ROMWALD – MTANZANIA DAR ES SALAAM
Social Plugin