“ASILIMIA 10 ya fedha za huduma ya kwanza kwa shule haitoshi kuhudumia wanafunzi wote kwani shule zetu zina wanafunzi wengi, lakini tunaendelea kuangalia namna ya kuwasaidia watoto hawa ili waweze kuhudhuria masomo yao,”anasema Kahundi.
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga, Mohamed Kahundi anasema na kusisitiza kuwa, bado kuna changamoto nyingi dhidi ya mtoto wa kike hususan suala la upatikanaji wa taulo za kujisitiri wanafunzi wa kike. Anasema, bajeti inayotolewa na Serikali badio haijitoshelezi.
“Kuweka chumba maalumu shuleni ni sera mpya tuliyoianzisha kupitia mradi wa “School Wash” unaotekelezwa katika kila halmashauri japo kuwa siyo katika shule zote kwa sasa, pale tunapohitajika kujenga vyoo vipya tumeamua kutenga vyumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri kupunguza utoro,” anasema Kahundi.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba anashauri vifaa hivyo kwa ajili ya watoto wa kike visamehewe kodi vinapoingizwa nchini kwa sababu vina gharama kubwa ukilinganisha kuwa watoto hao ni tegemezi bado.
“Ukisema shule zitumie pesa za vifaa zinunue taulo, haziwezi, kila mtu aangalie kuwa ni jukumu lake kuwahudumia watoto wa kike, jamii ituone sisi wanawake kuwa tuna mahitaji mengine yanayohitaji yaonwe ziada,” anasema Talaba.
Ofisa Elimu Msingi wilayani Kishapu, Richard Mutatina amekiri kuwepo na changamoto hiyo anaposema, halmashauri yake imeanza kuchukua hatua za kujenga vyumba maalumu shuleni kwa kushirikisha nguvu za wananchi ili kuweza kuwasaidia watoto wa kike.
“Ni kweli watoto wengi wa kike hushindwa kuhudhuria masomo wanapoingia katika ‘siku zao’, hali hii inachangiwa na kukosa eneo maalumu la wao kujihifadhi wanapokuwa shuleni, na mara nyingi huona aibu, takwimu zinaonesha kwa mwaka hupoteza siku 40 za masomo kutokana na kuwa katika siku zao,” anaeleza “Hata hivyo, tayari halmashauri yetu imeanza kulifanyia kazi tatizo hili na kuangaliwa uwezekano wa kujenga chumba kimoja katika kila shule kwa ajili ya kuwasaidia watoto hawa, tunatarajia kushirikisha pia nguvu za wananchi ili kufanikisha ujenzi huu,” anaeleza.
Mutatina anabainisha kuwa tayari shilingi milioni 279.5 zimetengwa katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba maalumu 33. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyenze iliyopo katika Kata ya Mwadui Lohumbo, Yohana Saraton anasema changamoto waliyo nayo sasa ni upatikanaji wa taulo watakazozitumia wakati wa hedhi.
“Sisi tuna chumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri, lakini pedi hazipo, tunaomba mashirika na wadau mbalimbali wajitokeze kufadhili ugawaji wa taulo hizi katika shule hiyo,” alisema Saraton.
Mwalimu mlezi wa wanafunzi wa kike katika shule hiyo, Leanita Kalinjuna, alisema ukosefu wa taulo hizo kwa ajili ya watoto wa kike, unawafanya baadhi ya wanafunzi wa kike kutohudhuria masomo wanapokuwa katika siku zao.
“Kutokana na kukosekana kwa vitambaa hivyo wanafunzi huwa wanatoa taarifa kama wapo, kwenye hali hiyo na huwa tunawapa ruhusa, ila tunaomba kupatiwa vifaa hivyo,” anasema Mwalimu Kalinjuna.
Aidha, Mwenyekiti wa Kituo cha taarifa na maarifa Kata ya Songwa, Rachel Madundo anasema kuwa wanafunzi wa kike katika shule za msingi na sekondari wilayani Kishapu hupoteza siku 40 za masomo kwa kila mwaka kutokana na shule nyingi wilayani humo kutokuwa na vyumba maalumu vya kujihifadhi pale wanapokuwa katika siku zao.
Pia anasema watoto wa kike hushindwa kuhudhuria masomo wanapokuwa kwenye siku zao kwa hofu ya kuaibika kutokana na ukosefu wa chumba kitakachowawezesha kujirekebisha na kujiweka katika hali ya usafi.
“Huu ni wakati sasa serikali na wadau wengine pamoja na halmashauri kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wanafunzi wa kike mashuleni ili waweze kusoma vizuri bila kukosa vipindi, pia kuangalia miundombinu ya vyoo ambayo itaweza kuwasaidia wanafunzi hasa wakike kwa kuwa wao wanamahitaji maalumu,” anasema Madundo.
Paul Peter kutoka kituo cha taarifa na maarifa, Kata ya Mondo wanaojihusisha na kupinga ukatili wa kijinsia, anasema wakati umefika Serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wanafunzi wa kike shuleni ili waweze kumudu masomo yao vizuri tofauti na hali ilivyo sasa kuna changamoto kubwa.
Diwani wa Kata ya Mwaweja wilayani humo Makanasa Kishiwa, alisema inatia huruma kwani watoto hao ni wao hivyo, Serikali haina budi kuwasaidia na kuongeza kuwa wataendelea kuishawishi Serikali kupitia vikao vyao vya Baraza kuona umuhimu wa kutenga fedha zitakazotumika kununua taulo za kujihifadhi watoto wa kike.
Ni kutokana na hali hiyo, Mkurungenzi wa Shirika la (Agape) Aids Control Programme mkoani Shinyanga John Myola, anato mwito kwa wakazi wa Mkoa wa Shinyanga kujitolea kwa hali na mali kusaidia ujenzi wa vyumba maalumu katika shule za msingi na sekondari vitakavyotumiwa na watoto wa watoto wa kike kujihifadhi wanapokuwa katika “vipindi vyao maalumu”.
Myola anatoa mwito huo katika uzinduzi wa mradi wa utoaji elimu ya afya ya uzazi na haki ya mtoto utakaotekelezwa katika Kata ya Usanda wilayani Shinyanga, chini ya ufadhili wa Shirika la Save the Children.
Anasema, ukosefu wa vyumba hivyo umetajwa kuwa moja ya changamoto inayowakabili watoto wengi wa kike katika shule za msingi na sekondari hali inayochangia wapoteze vipindi vingi vya masomo kila mwaka kutokana na kushindwa kuhudhuria masomo.
Anasema, umefika wakati jamii yenyewe ikabiliane na changamoto ya ukosefu wa vyumba hivyo na ijitolee kuvijenga kwa ushirikiano na Serikali ili kuwanusuru watoto wa kike badala ya kusubiri misaada ya wafadhili au serikali kuu.
“Ukosefu wa vyumba hivi unawaathiri watoto wetu sisi wenyewe, hivyo tusibweteke kusubiri wengine kutuondolea tatizo hili, lazima tuamue, wenyewe tuanze sasa, kata ya Usanda ioneshe mfano kwamba jamii ikiamua inaweza, vyumba hivi havihitaji gharama kubwa, mbali ya watoto kujihifadhi pia vitatumika kutolea huduma ya kwanza kwa watakaopatwa tatizo lolote.”
IMEANDIKWA NA KARENY MASASY - habarileo
Social Plugin