Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AZUNGUMZIA VITENDO VYA KUULIWA,KUPOTEA NA KUTEKWA KWA WATU TANZANIA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuendelea kuiamini Serikali yao na kuvipa muda vyombo vya dola kuendelea kufanya uchunguzi dhidi ya matukio mbalimbali ya kihalifu yaliyotokea nchini ili kubaini chanzo cha matatizo na wahusika.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea na utamaduni wa kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa pindi vinapotokea vitendo vya kihalifu au viashiria vyake katika maeneo mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 20, 2017) Bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe aliyetaka kupata kauli ya Serikali juu ya hofu iliyotawala nchini kuhusu vitendo vya watu kuuliwa, kupotea na kutekwa.

Waziri mkuu amesema “tukitoa taarifa mapema tunaweza kuharibu upelelezi, tuviachie vyombo vetu vya dola viendelee kufuatilia kuona nani anayesababisha vitendo hivyo na dosari iko wapi na nini chanzo chake alisisitiza,”.

Kadhalika Waziri Mkuu amewasii Watanzania kuendeleza utamaduni mzuri wa watu kuheshimiana, kufuata kanuni na kuviachia vyombo vya dola kutekeleza majukumu yake.

 “Moja ya majukumu ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa amani kwa kuwa na ulinzi wa uhakika kwao wenyewe na mali zao wakati wote,”.

Hata hivyo, Mheshimiwa Mbowe aliishauri Serikali kushirikiana na vyombo vya kiuchunguzi vya kimataifa kuchunguza tukio la kupotea kwa msaidizi wake Ben Saanane lililotokea miezi sita iliyopita, ambapo Waziri Mkuu amesema kuwa Taifa lina mahusiano mazuri na mataifa mbalimbali na inashirikiana nayo katika mambo mbalimbali likiwemo suala ya ulinzi ambapo si rahisi kuainisha namna wanavyoshirikiana.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa vyombo vyetu vina weledi,vifaa na uwezo wa kutosha kufanya uchunguzi juu mambo yanayotokea nchini hivyo amesisitiza wananchi kuendelea kuiamini kwani matukio haya ya kihalifu likiwemo la mtu kutoweka au kufariki na haina kikomo cha uchunguzi, mara zote uchunguzi unategemeana na aina ya tukio lenyewe au mazingira lilipo tokea

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inafanya mapitio kwa vyama vyote vya Ushirika nchini kufuatia baadhi ya vyama hivyo kuwa na mwenendo mbaya hali inayochangia upotevu wa fedha nyingi na kukatisha tamaa wakulima.

Amesema hivi karibuni katika kikao cha wadau wa zao la korosho kilichofanyika wilayani Bagamoyo Bodi ya Korosho ilidaiwa kuhusika na ubadhilifu wa sh. bilioni 30 ambapo Serikali iliunda timu maalumu ya uchunguzi na kubaini upotevu wa sh. bilioni sita na siyo sh. bilioni 30.

Hata hivyo amesema kwamba hasara hiyo ya sh. bilioni sita haikusababishwa na bodi bali vyama vikuu na vya ushirikika vilivyopo kwenye ngazi ya Kata na wilaya, ambavyo vyote vilifanyiwa uchuguzi na hatua zimeanza kuchukuliwa.

Amesema matatizo hayo yako katika vyama vyote vya ushirika hususan vya mazao ya Tumbaku, Kahawa,Pamba, Chai na mazao mengine makuu, ambapo Serikali imeanza kupitia taarifa za ukaguzi kwa kina ili iweze kufanya ukaguzi na sasa wanaendelea na uchunguzi wa chama kikuu cha tumbaku.

Waziri Mkuu amesema wakimaliza kufanya uchunguzi katika chama kikuu cha tumbaku watachunguza vyama vingine vya pamba, kahawa na chai lengo likiwa ni kuwalinda wakulima na kuhakikisha wanapata tija. “Naomba kusisitiza hatua zinaendelea kuchukuliwa na tutaendelea kuimarlisha na ushirika,”.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mheshimiwa Mama Salma Kikwete aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusu ubadhirifu wa sh. bilioni 30 uliofanywa na Bodi ya Korosho nchini.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P 980, DODOMA
ALHAMISI, APRILI 20, 2017.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com