WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harisson Mwakyembe amesema asilimia 90 ya watangazaji wa redio na televisheni nchini hawana sifa za kitaaluma katika tasnia ya habari.
Waziri Mwakyembe alitoa taarifa hiyo juzi bungeni alipokuwa anawasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 ya Sh bilioni 28.2. Kwa mujibu wa Waziri, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilifanya ukaguzi wa kina katika huduma za utangazaji kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 ikihusisha ukaguzi wa vifaa vya utangazaji, vyumba vya habari, maktaba, mikataba ya ajira pamoja na sifa za watangazaji katika vyombo vya habari.
‘’Vituo vyote vimeonesha kuwa na ubora wa huduma inayotolewa, hata hivyo asilimia 90 ya wafanyakazi wamebainika kutokuwa na sifa za kitaaluma za uandishi wa habari na utangazaji na kwamba hiyo ndiyo changamoto kubwa inayoikabili tasnia ya habari,’’ alisema Dk Mwakyembe.
Ukiacha changamoto hiyo, Waziri alisema taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake zimefanya vizuri katika majukumu yake kwa mwaka wa fedha uliopita, miongoni mwake ni pamoja na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) wazalishaji wa magazeti ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo na Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC).
Taasisi nyingine ni TCRA, Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo na Baraza la Michezo la Taifa (BMT). Dk Mwakyembe alitoa pongezi kwa TSN kwa kuboresha majukumu yake ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha na kuongeza kwamba kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 magazeti hayo ya serikali yamevutia wasomaji wengi na pia kuongeza idadi ya watangazaji katika magazeti hayo kiasi cha kuongoza katika matangazo kwenye vyombo vya habari.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Juma Nkamia aliipongeza serikali kwa kutenga Sh bilioni 2.4 kwa ajili ya kununua mtambo mpya wa kisasa wa uchapishaji magazeti kwa ajili ya TSN.
“Kamati inapendekeza mtambo wa sasa wa kuchapisha magazeti wa Dar es Salaam uhamishiwe makao makuu ya serikali Dodoma ili kurahisisha usambazaji wa magazeti katika mikoa jirani ya Tabora, Mwanza, Iringa na mikoa mingine.
Chanzo-Habarileo
Social Plugin