Katika moja kati ya mahubiri yake, Nabii Bushiri ambaye ni mzaliwa wa Malawi anayefanya kazi zake nchini Afrika Kusini, alidai kuwa ameona hali ya umauti ikimnyemelea Lowassa na kuwataka waumini wake kuomba ili awe na maisha marefu.
Akizungumza leo katika ibada kanisani kwake, Gwajima alilaani utabiri wa Nabii Bushiri, akidai kuwa amekodiwa na watu wenye nia mbaya ili atabiri ubaya kuhusu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ili kufanikisha mpango wao wa kufanya tukio baya.
Gwajima alidai kuwa kwa uwezo wa kiroho, amewafahamu watu waliopanga kutekeleza njama dhidi ya Lowassa na viongozi wengine wa Serikali huku wakimtumia nabii huyo kuwaandaa watu kisaikolojia.
“Nataka nimueleze Nabii Bashiri kuwa nafahamu watu waliomkodi kufanya hivyo, na utabiri wake hautawezekana kamwe. Hakuna kiongozi yoyote wa serikali wala wa upinzani atakayekufa kwa utabiri huo. Wote wataishi kwa jila la Yesu,” alisema Gwajima ambaye leo alikuwa akihubiri kwa lugha ya kiingereza na kufasiriwa kwa lugha ya kiswahili.
Hata hivyo, Askofu huyo anayefahamika kwa kauli zake tata alieleza kuwa kwa uwezo wa kiroho amewafahamu watu waliopanga njama hizo na namna walivyoenda Afrika Kusini kukutana na mhubiri huyo kwa lengo la kumkodi atoe utabiri huo.
“Wanaweza kujiuliza nimewafahamu vipi. Roho yangu ilisafiri nao hadi Afrika Kusini, walivyokutana na Nabii Bashiri nilikuwa naye, yote waliyozungumza naye nayafahamu na hata walichompa ninakifahamu,”alisema.
“Ninawafahamu kwa majina na walipo na ninawataka wakome mara moja kuendelea na mpango wao. Wasipositisha mpango wao huo, Jumapili ijayo nitawataja hapa wote kwa majina,” alisikika Gwajima.
Gwajima alidai kuwa hamaanishi kuwa Bushiri sio mtumishi wa Mungu, lakini utabiri wake juu ya viongozi wa Tanzania ni wa kukodiwa.
Nabii Bushiri ambaye amekuwa akizua mijadala na hata kuingia katika mgogoro na baadhi ya nchi za Afrika, pia aliwahi kutabiri kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu Tanzania pamoja na tukio la tetemeko la ardhi nchini.
Tazama video hapa chini
Social Plugin