Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BARAZA LA MITIHANI -NECTA KUHAKIKI VYETI FEKI KWA KASI YA AJABU


BARAZA la Mitihani (Necta) limesema idadi ya watu waliokwenda kuhakiki imekuwa ikipungua siku hadi siku na kusisitiza kuwa uhakiki wa rufaa hizo utafanyika kwa haraka na kwa haki na uadilifu katika kushughuliki malalamiko yaliyowasilishwa kwao.

Akizungumza jana, Ofisa Habari wa baraza hilo, John Nchimbi alisema: “Siku za mwanzo tulikuwa tunapokea watu wengi wanaokuja kuhakiki vyeti vyao, idadi imekuwa ikipungua, hata leo (jana) ambayo ni siku ya mwisho idadi ni ndogo sana.” Nchimbi ambaye alisema bado mapema kwa ofisi yake kutaja idadi kamili ya waliojitokeza kuhakiki vyeti hivyo, alisema baada ya uhakiki majibu ya uhakiki yatapelekwa Wizara ya Utumishi.

“Tukishamaliza kuhakiki majibu ya uhakiki yanapelekwa utumishi kama ilivyokuwa awali, na wao ndio watasema kile kilichobainika,” alisema. Tangu kutolewa kwa fursa ya kukata rufaa na kuhakiki vyeti vyao, kulikuwepo na umati wa watumishi wa umma waliojitokeza kukata rufaa na kuhakiki vyeti vyao.

 Orodha ya watumishi iliyotolewa na serikali ilikuwa na makundi matatu ya watumishi watumishi walioghushi vyeti, waliowasilisha vyeti visivyokamilika na wale wenye vyeti vyenye utata ambavyo cheti kimoja kinatumiwa na zaidi ya mtumishi mmoja.

Hata hivyo, makundi yote matatu yamejitokeza na kuwasilisha rufaa na malalamiko yao Necta. Akizungumzia sakata hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema jana bado kazi ya kushughulikia rufaa za waliokata kuhusishwa na vyeti feki inaendelea na ikikamilika, umma utapewa mrejesho.

 Jana ilikuwa mwisho kwa watumishi waliotajwa kwenye orodha ya watu walioghushi vyeti feki kukata rufaa na kuhakiki vyeti vyao Utumishi na Baraza la Mitihani Tanzania.

Kairuki aliliambia gazeti hili mjini Dodoma kuwa, umma utapewa mrejesho wa malalamiko yaliyopokelewa pindi kazi hiyo itakapokamilika na kwamba hata uhakiki uliofanywa na Necta bado haujawasilishwa kwao na mpaka jana walalamikaji walikuwa wakiendelea kupeleka rufaa zao jana hivyo ni mapema kusema chochote.

 Taarifa kutoka wizarani mjini Dodoma jana zilieleza pia kuwa, taarifa rasmi ya kazi hiyo itatolewa baada ya Necta kukamilisha uhakiki na kuwasilisha taarifa zake wizarani humo. 

Hadi jana mchana kwenye ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma zilizopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kazi hiyo ilitarajiwa kukamilika saa 9.30 alasiri.

Mwandishi wa habari hizi alifika wizarani hapo kwa ili kuonana na Katibu Mkuu Utumishi kwa ajili ya kufahamu zaidi uendeshaji wasuala hilo hilo ulivyokuwa mpaka linapohitimishwa na alielezwa kuwa Katibu Mkuu yuko Dar es Salaam kikazi. 

Hata hivyo, Ofisa Habari wa Wizara hiyo, James Mwanamyoto alisema kuwa msemaji wa taarifa hizo ni Katibu Mkuu au Waziri husika na kuwataka waandishi kusubiri kwani taarifa ikiwa tayari itatolewa kwa umma.

 Kwa upande wa watumishi wenye vyeti vya kughushi wanapaswa kuwasilisha rufaa zao kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala wa Bora ambaye ndiye atakayewasilisha rufaa hizo kwa baraza hilo la mitihani.

Serikali kupitia Wizara ya Utumishi ilitoa orodha ya watumishi 9,932 wanaodaiwa kughushi vyeti na kupewa siku 14, kujiondoa kazini na wale wataokaidi watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kifungo cha miaka saba jela.

 Wiki moja baadaye, Wizara pia ilitoa orodha nyingine ya watumishi 2,016 wanaodaiwa kuwasilisha vyeti visivyokamilika ambao wengi walitokea kwenye taasisi na mashirika ya serikali na kutakiwa kusilisha vyeti vyote hadi mwishoni mwa mwezi huu.

 Hivi karibuni Rais John Magufuli alikabidhiwa taarifa ya uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma ambapo watumishi zaidi ya 9,932 walibainika kuwa na vyeti vya kughushi na alitangaza kuwafuta kazi na aliwapa siku 15 wawe wameondoka kazini bila kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com