Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM YAWATAKA VIONGOZI WENYE DHAMANA WAJITAFAKARI MAUAJI YA KIBITI

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimelaani vikali mauaji ya baadhi ya viongozi, raia na askari polisi, waliouawa kwa kupigwa risasi katika wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga mkoa wa Pwani, na kutoa pole kwa familia zilizoguswa na mauaji hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari  jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey  Polepole alisema chama hicho kwa niaba ya wananchi kinawataka viongozi wenye dhamana na usalama wa wananchi kujitafakari, huku akisisitiza kuwa ikiwa mauaji hayo yataendelea, chama hicho kitaielekeza serikali kuwachukulia hatua.

“Sasa imetosha, yeyote mwenye dhamana ajitafakari.Hatupendi kusema hali hii ikiendelea watu wawajibike, ingawa kuwajibika kwa sababu ya watu kupoteza maisha ni ustaarabu wa kiungozi. Viongozi wote na wenye dhamana mchukue hatua, sitaki tufike pahala niseme, CCM tutaielekeza serikali kuchukua hatua kwa walio na dhamana kwa kutowajibika katika majukumu yao,” alisema na kuongeza Polepole.

“Tunaamini demokrasia ya vyama vingi ni mshikamano tunahisi kama tumeachwa wenyewe, tumevunjika moyo sana , sielewi mshikamano wa kuweka Tanzania moja, unakuja wakati wa uchaguzi au kugawana ruzuku? tumesikitishwa, nimeona wenzangu wametingwa na kufanya siasa za madaraka kuliko siasa za maendeleo zinazohusu shida za watu wetu.”

Aidha, Polepole alisema anasikitishwa na ukimya wa vyama vya upinzani kuhusu mauaji hayo, ambapo ameeleza kipindi hiki vyama vyote pasina kujali itikadi za kisiasa vingeungana kutetea uhai wa wananchi wa maeneo hayo ambao ndiyo wapiga kura wao.  

Alisema CCM wangependa kuona vyama vyote kwa sasa vinaungana hasa katika kipindi hiki ambacho wananchi wana hofu na maisha yao kutokana na mauaji hayo lakini jambo hilo limekuwa tofauti kwa wapinzani wao kuwa kimya na kutoonyesha kuumizwa na mauaji hayo.

“Hakuna namna bora ya kuwahudumia wananchi kama kuwa na mshikamano, wale wananchi wakienda kwenye kura wanachagua vyama vyote, wale wenzetu wamekuwa kimya, wametusikitisha, na hata wale walioongea wamecheza maneno, tusicheze maneno wakati uhai wa wenzetu upo hatarini,

“Sisi kama Chama cha Mapinduzi tukikaa kimya tutakuwa hatuwatendei haki watanzania ambao wakati kama huu wanapitia wakati mgumu, ninawaomba viongozi wote wenye dhamana wachukue hatua,” alisema Polepole.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com