Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, wanahusika na sakata la mchanga wa madini (makinikia) unaosafirishwa nje ya nchi.
Pia amesema Mkapa na Kikwete hawawezi kukwepa lawama juu ya mchanga huo kwa kuwa mikataba kati ya Serikali na wawekezaji wa migodi inayotajwa, ilisainiwa kwa nyakati tofauti wakati wao wakiwa madarakani.
Kauli hiyo aliitoa mjini Dodoma jana alipozungumza katika mkutano wa Baraza Kuu la Chadema uliokutanisha wajumbe 332, kati ya 370 waliotakiwa kuhudhuria.
“Kama kuna kitu kinaangamiza nchi, ni pale unapomwambia mfalme umevaa suti wakati unaona yuko uchi. Katika sakata hili la mchanga, sisi kama chama cha siasa, tumekaa na wataalamu wetu na kukusanya taarifa kwa sababu wengi wanalizungumzia kwa kauli tofauti,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Kwanza kabisa inabidi tuelewe kwamba mchanga wa madini umekuwa ukisafirishwa kwenda nje ya nchi kutoka kwenye migodi yetu miwili ya Bulyanhulu kuanzia mwaka 2001 na Buzwagi kuanzia mwaka 2008.
“Eleweni kwamba leseni za kusafirisha mchanga kwenda nje zilitolewa na Serikali hii hii ya CCM na katika mikataba hiyo, kunatambulika kuna madini mengine mbali na dhahabu katika migodi hiyo.
“Pia makontena ya madini yanapokuwa bandarini kabla ya kusafirishwa, watu wa TRA, TMAA, lazima wahakiki makontena yenye mchango huo ili kujiridhisha na kilichomo.
“Wakati mikataba hii inasainiwa, Rais Dk. John Magufuli alikuwa kwenye Baraza la Mawaziri na pia Mkapa na Kikwete, wanayajua haya kwa sababu mikataba ilisainiwa wakati wao wakiwa madarakani kwa nyakati tofauti.
“Nasema hivyo kwa sababu enzi za Mkapa, mikataba mingi ya madini ilisainiwa na hata Kikwete alipokuwa Waziri wa Nishati, kuna mkataba aliusaini.
“Kibaya zaidi, CCM wamekuwa wakitumia wingi wao vibaya bungeni kupitisha sheria mbovu kwa sababu hata mwaka 1997, Bunge lilipitisha kwa siku moja sheria mbili za madini chini ya hati ya dharura na mwaka 1998, Bunge lilipitisha sheria nyingine ya madini inaweka utaratibu wa uchimbaji wa madini na kuruhusu wawekezaji kutoa mrabaha wa asilimia tatu ingawa baadaye mrabaha huo ulibadilishwa na kuwa asilimia nne, huku sheria hiyo ikiruhusu mchanga usafirishwe kwenda nje ya nchi.
“Yaani, hata mikataba yetu inaruhusu wawekezaji kupewa misamaha ya madini wakati sheria haisemi hivyo. Kwa hiyo, kinachotokea sasa ni matokeo ya CCM kutufikisha tulipofika.”
Kutokana na hali hiyo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema kuna uwezekano mkubwa Kampuni ya Acacia inayomiliki migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu ambako mchanga huo ulipatikana, ikafungua mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro.
“Jana nilikuwa nasoma Gazeti la Telegraph la Uingereza ambapo wanasema tatizo sio wawekezaji bali ni Waafrika wanaoingia mikataba ya uwekezaji na wanasema kwa mujibu wa mkataba wetu, mchanga sio mali ya Tanzania bali ni mali ya wawekezaji.
“Kwa hiyo, kinachoonekana sasa ni kwamba nchi inaingia katika mgogoro wa kidiplomasia na wawekezaji na kama wakiamua kwenda mahakamani, hatutashinda kesi kwa sababu mikataba tuliisaini vibaya.
“Kibaya zaidi, ni kwamba kesi haitakuwa Kisutu, Kinondoni, Mwanza au Kigoma, bali itafanyika huko huko kwao,” alisema.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema kwa kuwa uwezo wa Tanzania ni mdogo katika uwekezaji wa miradi mikubwa, Serikali inatakiwa kuwa makini kwa sababu si kweli kwamba wawekezaji wote ni wezi na pia si kweli kwamba wote ni waaminifu.
Akizungumzia hali ya kisiasa, Mbowe alisema katika uzoefu wao kisiasa, Serikali ya awamu ya tano ndiyo ngumu katika harakati zao kwa sababu Rais Magufuli anakandamiza demokrasia.
Kwa mujibu wa Mbowe, alisema serikalini kuna baadhi ya viongozi wanaamini njia pekee ya kuwaweka madarakani ni kuvunja sheria na kuminya demokrasia, jambo ambalo wamelivumilia kwa muda mrefu na kuwafanya viongozi hao waamini Chadema ni waoga.
Alitoa mfano wa matukio aliyosema ni uminywaji wa demokrasia nchini ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa, kukamatwa kwa wanasiasa wa upinzani na kufikishwa mahakamani bila sababu na kupotea kwa kada wa Chadema, Ben Saanane.
“Awamu hii ya tano ni ngumu sana kisiasa, lakini pia inatoa fursa kwetu kwa sababu wananchi wana maisha magumu kweli kweli kuliko Serikali yoyote katika nchi yetu.
“Rais lazima ajue kwamba matendo yake yanaathiri Watanzania milioni 50 na ajue sisi tunahitaji pia aliyeko madarakani alete amani kwa sababu nchi ni yetu sote.
“Kwa kifupi, nchi yetu kwa sasa haiko salama, kisiasa, kiuchumi na wala kijamii, kwa sababu kila mmoja anashuhudia jinsi watu wanavyouawa Rufiji na Mkuranga.
“Pamoja na hayo, eleweni kwamba haki haipatikani kwa kuombwa bali kwa mapambano. Kwa hiyo, lazima katika kikao chetu hiki tutoke na uamuzi mgumu ili watawala wa nchi hii waelewe salama ya nchi ni kusimamia haki kwa watu wote na sio kwa wana CCM peke yao, kama mbwai na iwe mbwai,” alisema Mbowe.