Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HOFU YA VYETI FEKI : MATANGAZO YA KUPOTELEWA VYETI KWENYE MAGAZETI YAFURIKA

MATANGAZO ya upotevu wa vyeti yameongezeka katika magazeti mbalimbali na kwa siku ya jana pekee yalikuwapo 90.


Kitendo cha matangazo hayo kuongezeka kimeibuka ikiwa imebaki siku moja kwa baadhi ya watumishi wa Serikali wanaodaiwa kuwa na vyeti feki kutakiwa kukamilisha mchakato wa kukata rufaa.


Taarifa ya watumishi hao, ambao ni miongoni mwa 9,932 kutakiwa kukata rufaa ilitangazwa wiki iliyopita na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro, kutokana na kuamini pengine wameonewa kutajwa katika orodha ya vyeti feki.


Baada ya Dk. Ndumbaro kutoa taarifa hiyo, matangazo hayo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku na yamekuwa yakihusisha zaidi upotevu wa vyeti vya kidato cha nne vinavyodaiwa kuwa na utata kwa baadhi ya watumishi.


Miongoni mwa waliotangaza matangazo hayo wamo wahadhiri wa vyuo vikuu na haijajulikana kama nao wanahusika moja kwa moja katika uhakiki huo.


Pia huenda matangazo hayo yakaongezeka zaidi baada ya kuwapo kwa taarifa ya kutangazwa kwa orodha mpya ya watumishi wanaodaiwa kuwa na vyeti feki waliopo katika taasisi na wizara zilizobaki, pindi mpango mwingine wa uhakiki wa vyeti utakapokamilika.


Wakati matangazo hayo yakiendelea kuongezeka kwa kasi magazetini, orodha ya rufaa hizo inatarajiwa kutolewa kesho na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA).


Juzi Dk. Ndumbaro alilithibitishia MTANZANIA Jumapili kuwa, awamu nyingine ya mpango huo ipo katika hatua za mwisho na muda wote kuanzia sasa majina hayo yatatangazwa.


Dk. Ndumbaro alisema orodha hiyo mpya iliyopaswa kutangazwa Jumatano wiki hii itatoka siku yoyote kuanzia kesho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com