MASHUHUDA waliofika kwanza kwenye eneo la tukio la ajali mbaya iliyotokea jana asubuhi walikuta wanafunzi 37 na walimu waliokufa kwenye ajali hiyo wakiwa wamelundikana sehemu ya mbele ya basi hilo lililokuwa limeharibika vibaya.
Kukiwa hakuna muathirika hata mmoja katika viti, wengi wanaamini kuwa watoto waliokuwa wameingiwa hofu walitoka kwenye viti vyao na kukimbilia kwa walimu wao baada ya gari kuanza kuyumba.
Mkazi wa Rhotia, Nancy Baha alisema aliona basi hilo la shule likiwa katika mwendo kasi lakini katika mtindo wa kuyumbayumba, ikiwa ni asubuhi yenye ukungu kabla yeye na mashuhuda wengine waliokuwa dukani kushuhudia kwa macho yao basi hilo lenye rangi ya njano likirushwa juu na kudumbukia korongoni, likitanguliza sehemu ya mbele.
Watu wengine walioshuhudia ajali hiyo wanakumbuka watoto wakipiga kelele, ni dhahiri watoto hawa kabla ya kupatwa mauti walishuhudia jambo la kutisha maishani mwao. Inadaiwa kuwa lori lililokuwa likija mbele ndio lilisababisha dereva wa basi kutoka nje ya barabara kwa lengo la kukwepa kugongana uso kwa uso na ndipo basi lilitumbukia kwenye korongo la Mto Marera.
Mistari mitatu ya viti vya nyuma vya basi hilo aina ya ‘Mitsubishi Rosa,’ lenye namba za usajili T-871 BYS, vilikutwa kama vilivyo, hivyo waliofika mapema eneo la tukio kwa ajili ya kuokoa majeruhi wanaamini wanafunzi kwa woga walitoka kwenye siti zao na huenda walikuwa wanakimbilia kwa walimu wao waliokuwa wamekaa mbele kwa ajili ya msaada au huenda walikuwa wanajaribu kukimbilia mlango.
Wakati taifa likiwa katika msiba huu mzito, kutokana na vifo vya wanafunzi wa darasa la saba zaidi ya 35 na walimu wao watatu, watu waliofika wa kwanza eneo la ajali walisema miili yote ilikutwa eneo la mbele la basi hilo.
Wanafunzi hao na walimu wao waliondoka Arusha saa 2.00 asubuhi, pengine dereva alikuwa katika haraka kufika wanakokwenda kuwahi muda wa mtihani katika shule ya Tumaini English Medium iliyopo wilayani Karatu.
Ajali imetokea karibu saa 4:00 asubuhi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alithibitisha idadi ya watu waliokufa kuwa ni wasichana 16, wavulana 17 na watu wazima wanne akiwemo dereva, hata hivyo mtoto wa 38 inadaiwa amekufa baadaye katika Hospitali ya Mount Meru. Watoto wanne na mtu mzima mmoja wamenusurika kifo lakini wamejeruhiwa.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Esther Mahawe alitembelea majeruhi katika Hospitali ya Wilaya ya Karatu kuwajulia hali. Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo, alisema wanafunzi wa shule ya Lucky Vincent walikuwa njiani kwenda mji wa Karatu kushiriki mtihani wa moko wa kirafiki na wenzao wa Shule ya Msingi ya Tumaini Junior, Karatu. Basi hilo ni mali ya shule ya Lucky Vincent likiwa na Bima ya Zanzibar.
Mmiliki wa shule Innocent Mushi hakupatikana kwa sababu siku nzima simu yake ilikuwa imezimwa. Mushi ni mfanyabiashara anayemiliki shule ya Lucky Vincent na biashara ya usafirishaji mkoani humo.
Jambo la ajabu, wiki iliyopita, moja ya gari la Mushi aina ya Scania liligonga mwanafunzi wa shule nyingine katika eneo la Sakina. Katika eneo la shule Kwa-Mrombo, wazazi, ndugu na marafiki waliokuwa wamejaa huzuni kubwa walikuwa wamekusanyika na hali hiyo ilikuwepo pia katika kambi ya polisi Arusha kwani baadhi ya watoto waliokufa ni wa maofisa wa polisi.
Majina ya marehemu
Majina ya marehemu yaliyotajwa hadi sasa kutokana na ajali hiyo ni Mteage Amos, Justine Alex, Irene Kishari, Praise Ronald, Shadrack Biketh, Junior Mwashuya, Aisha Saidi, Heri Rashid, Gema Gerald, Rebecca Daudi, Hagai Lucas, Sada Ally, Lucy Ndemna, Mussa Kasim na Neema Martin. Wengine ni Witness Mosses, Rukia Khalfani, Naomi Hosea, Hevenight Hosea, Eliapenda Eliudi, Arnold Alex, Marion Mrema, Rehema Msuya, Sabrina Said, Prisca Charles, Grayson Robson Massawe, Lara Tarimo na Neema Eliwahi.
Wote walikuwa wanafunzi wa darasa la saba ambao walikuwa wafanye Mtihani wa Taifa wa Shule Msingi 2017 . Shule hiyo pia iliongoza mitihani ya taifa mwaka jana. Shule ya Awali na Msingi ya Lucky Vincent ambayo wanafunzi wake wameteketea katika ajali hiyo jana asubuhi waliongoza mwaka jana katika Mtihani wa Taifa Kimkoa.
Shule hiyo iliyopo eneo la Field Force, Kwa-Mrombo katika kata ya Olasiti, mjini Arusha ilikuwa shule ya 20 bora kati ya shule 8,109 nchini na katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka jana ilikuwa na wahitimu 101 na wanafunzi wote waliofanya mtihani walipata Daraja A katika somo la Kiingereza.
Shule ya Msingi Lucky Vincent ilikuwa shule namba moja mkoani Arusha na kuzishinda shule nyingine za msingi 331 katika wilaya saba za mkoa huo. Wakati wanafunzi wote wa Lucky Vincent walipata ‘A’ kiingereza, wanafunzi 92 walipata ‘A’ kwenye somo la sayansi , 81 walipata ‘A’ ya hesabu na 63 walipata ‘A’ Kiswahili (63), ikionesha walikuwa wazuri katika masomo ambayo wengine wanayaona magumu sana.
Katika hatua nyingine, Mwalimu Mkuu Msaidizi, Longino Vincent alisema amehuzunika sababu jana asubuhi yeye ndiye aliyepanga orodha ya wanafunzi hao na kwa sababu walipanda magari matatu kila gari walipanda wanafunzi 32 na walimu wao na kulielezea tukio limemfanya apate mshituko mkubwa baada ya kusikia ajali hiyo.
Kwa mujibu wa Vincent, chanzo cha ajali hiyo ni kuwa gari lilikosa breki ndipo dereva alipohangaika nayo na kutumbukia kwenye korongo hilo lililosababisha wanafunzi na walimu wao kupoteza maisha.
Alisema watoto hao waliondoka saa 12:30 asubuhi na safari yao ilikuwa ya saa mbili tu kutoka Arusha hadi Karatu jumla ya watoto hao walikuwa 96 na walimu wao. “Gari lilikosa breki dereva wetu Denis alikuwa akihangaika kujaribu kuokoa maisha ya watoto wetu lakini haikuwezekana ndipo likatumbukia kwenye korongo,… hili gari limepata hitilafu na kwa sababu dereva alikuwa katikati ndipo aliamua aingie hapo kwenye korongo akidhani ni dogo kumbe ni korongo kubwa na walimu wawili waliokufa ni Innocent Papian ambaye ni Mwalimu wa kingereza na Julius Mollel Mwalimu wa sayansi,” alisema.
Mkuu wa wilaya ya Arusha, Gabriel Fabian Daqqaro alisema ibada ya kuwaombea watoto waliokufa katika ajali itafanyika kesho saa tatu asubuhi katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid na taratibu za mazishi kufanywa.
Rais John Magufuli atuma rambirambi
Katika hatua nyingine, Rais John Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya wanafunzi wa darasa la saba, walimu na dereva wa gari la shule ya msingi iitwayo Lucky Vincent ya Arusha vilivyotokea jana saa tatu asubuhi baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika eneo Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilisema kwa masikitiko Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na kueleza kuwa ajali hiyo imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia Taifa na imesababisha uchungu, huzuni na simanzi kubwa kwa familia za marehemu na Taifa kwa ujumla.
“Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo naomba unifikishie pole nyingi kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote wa wanafunzi, walimu na dereva waliopoteza maisha, hiki ni kipindi kigumu kwetu sote, na uwaambie naungana nao katika majonzi na maombi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Rais aliongeza kusema kuwa, “muhimu kwa sasa tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema, majeruhi wapone haraka na wote walioguswa na msiba huu wawe na moyo wa subira, ustahimilivu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.”
Spika wa Bunge atuma salamu za pole
Wakati huo huo, Spika wa Bunge Job Ndugai amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kutokana na vifo vya wanafunzi, walimu na dereva wa Shule ya Msingi Lucky Vicent ya mkoani Arusha, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali jana asubuhi katika eneo la Rhotia Marera, wilayani Karatu, mkoani Arusha.
“ Mkuu wa Mkoa nakupa pole sana, nimepokea kwa mshtuko taarifa hii ya ajali iliyogharimu maisha ya watoto wetu, hakika hili ni pigo kwa taifa zima, namuomba Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi,” alisema Ndugai.
Aliongeza kuwa, “natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao, Mwenyezi Mungu awape nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu, vilevile nawaombea majeruhi wote wa ajali hiyo wapate uponyaji wa haraka.”
Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema chama chake kimepokea kwa majonzi na simanzi kubwa taarifa ya vifo vya wanafunzi pamoja na waalimu wao.
Taarifa kwa vyombo vya habari ilisema Zitto alisema taifa limepoteza nguvu kazi ambayo si rahisi pengo lake kuzibwa na kuwapa pole waalimu wa shule ya awali na Msingi ya Lucky Vicent, wazazi wa watoto, ndugu, jamaa na marafiki ambao wamepoteza vipenzi vyao.
Kiongozi huyo wa ACT aliomba kwa Mwenyezi Mungu majeruhi wapone haraka na waweze kuendelea na masomo yao mpaka wafikie malengo waliyotarajiwa. “ACT- Wazalendo tumesikitishwa na vifo hivi vya watoto wetu pamoja na walimu wao, tunawapa pole ndugu jamaa na marafiki Mwenyezi Mungu awape nguvu ya kuhimili kipindi hiki kigumu kwao… Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, Amini,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Wakati huo huo, wakati tunakwenda mtamboni wazazi walikuwa wakitambua miili katika hospitali ya Mount Meru. Tukio hili la wanafunzi wa Lucy Vincent, linakumbusha tukio lingine baya ambalo taifa lilipata mshtuko na majonzi baa da ya wanafunzi zaidi ya 40 wa Shule ya Sekondari ya Shauritanga waliokufa kwa ajali ya moto bwenini Juni 18, mwaka 1994.
Habari hii imeandikwa na Marc Nkwame na Veronica Mheta, Arusha.
Social Plugin