KAMATI ya Ulinzi na Usalama wilayani Kahama mkoani Shinyanga imeziruhusu halmashauri za Msalala na Ushetu kuanza kuteketeza wanyama wakali aina ya fisi, wanaotishia usalama wa wananchi.
Taarifa hiyo ilitolewa kwa vyombo vya habari hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, Simon Berege wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Alisema hayo baada ya kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, kilicholenga kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo.
Berege alisema kwa sasa halmashauri hizo mbili, Msalala na Ushetu, zinaendesha kazi ya kuwasaka fisi hao wanaotishia maisha ya wananchi na kuwaua kwa kutumia bunduki ili kunusuru maisha ya wananchi hao.
“Hawa fisi wakiingia vijijini wanatishia maisha ya wananchi hasa wanawake na watoto, lakini fisi hawa wanawaogopa wanaume hivyo kwa ruhusa ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, tumeanzisha oparesheni maalumu ya kuwatokomeza fisi kwa kuwaua kwa kutumia bunduki na sumu,” alisema Berege.
Alisema siku hiyo wakati akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake, fisi mmoja tayari alikuwa ameuawa na maofisa wa idara ya wanyamapori katika Kata ya Chela, baada ya kutaka kutafuna watoto. Aliswema fisi waliouawa hadi sasa ni 14. Akifafanua juu ya idadi ya fisi waliouawa ili kunusuru wananchi kuliwa na fisi hao, mkurugenzi huyo alisema katika Kijiji cha Kakola waliuawa fisi saba, Kata ya Ngaya fisi sita na Kata ya Chela aliuawa fisi mmoja.
IMEANDIKWA NA RAYMOND MIHAYO,- HABARILEO KAHAMA