WATU sita wamekufa na mmoja kujeruhiwa katika matukio mawili tofauti yaliyotokea mkoani Rukwa likiwemo la mkazi wa Kijiji cha Ilonga, Kata ya Mambwe Nkoswe wilayani Kalambo, David Sakanyanya (26) aliyemuua bibi yake, Sikilieli Nampunje (55) kwa kumpiga risasi wakigombea mashamba ya urithi kwa zaidi ya miaka mitatu.
Aidha, wavuvi watano wamekufa maji na mmoja kujeruhiwa baada ya mtumbwi kupinduka wakati wakivua samaki katika Ziwa Rukwa lililoko katika Wilaya ya Sumbawanga. Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Polycarp Urio alithibitisha kutokea kwa matukio hayo mawili, akieleza kuwa mtumbwi uliokuwa ukitumiwa na wavuvi hao sita ulipinduka baada ya kukumbwa na dhoruba na kusababisha mtumbwi huo kuzama.
Urio aliwataja marehemu hao kuwa ni Paschal Kizepa (30), mkazi wa kijiji cha Santauki, Peter William (45) wa kijiji cha Mtowisa, Edward Emily (40) wa kijiji cha Kalakala, Frank Kadima (36) wa Uzia na Saliboko Damas (28) mkazi wa kijiji cha Lwanji, vyote viko katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga.
Mvuvi aliyejeruhiwa ametambuliwa kuwa ni Florence Mpomwa (27), mkazi wa kijiji cha Kipa na miili ya marehemu imekabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya maziko. Kuhusu mkasa wa mjukuu kumuua bibi yake kwa kumpiga risasi, alisema mauaji hayo yalifanyika juzi wakati Nampunje alipokwenda kumshtaki mjukuu wake, David Sakanyanya (26) kwa uongozi wa kata akidai kuwa ameporwa mashamba yake na mjukuu wake huyo.
Mume wa marehemu, Abbas Kapunda alisema mkewe aliuawa kwa kupigwa risasi na mjukuu huyo akiwa njiani kwenda nyumbani akitokea shambani. “Ghafla tulisikia mlio kwa bunduki ulioambatana na mayowe ya kuomba msaada ndipo tulikimbia hadi kwenye eneo la tukio … nilishuhudia mke wangu Sikilieli akiwa anagaagaa chini huku akivuja damu kwa wingi.
Mashuhuda walitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji ulioutaarifu uongozi wa kata nao ukaitaarifu polisi, askari polisi walifika eneo hilo la tukio muda mfupi tu …. mke wangu alikimbizwa katika Zahanati ya Kalembe, lakini alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu,” alidai Kapunda.
Naye Moses Alfred ambaye ni mmoja wa ndugu wa marehemu, alidai chanzo cha kifo cha ndugu yao (Sikilieli) kuwa na mgogoro wa mashamba kati yao. Alisisitiza kuwa, wakati wa uhai wake Sikilieli alikuwa akifuatilia haki yake ya mashamba aliyoachiwa na baba yake mzazi ambaye kabla ya kufariki dunia (baba huyo), aligawa mashamba kwa watoto wake, lakini wengine hawakuridhika ambapo walimnyang’anya kwa madai kuwa hana uwezo wa kumiliki mashamba hayo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilonga, Peter Munga alisema familia hiyo imekuwa na mgogoro huo kwa takribani miaka mitatu; huku Kaimu Kamanda Urio akieleza kuwa mtuhumiwa ameshakamatwa na anaendelea kuhojiwa.
IMEANDIKWA NA PETY SIYAME- habarileo SUMBAWANGA
Social Plugin