KUTANA NA MMEA WENYE HARUFU INAYOMFANYA MTU KUKUMBUKA MAMBO


Watafiti nchini Uingereza wamesema huenda harufu ya mmea wa rosemary ikawa na uwezo wa kusaidia mtu kukumbuka mambo.

Mmea huyo, ambao huwa na maua ya rangi ya nyeupe, waridi, zambarau au samawati, sana hutumiwa kama kiungo kwenye chakula, vinywaji au mchuzi.

Utafiti ulibaini kwamba wanafunzi waliokuwa kwenye chumba kilichopulizwa harufu ya rosemary, iliyokuwa kwenye mafuta, walikuwa na uwezo wa kukumbuka mambo kwa asilimia 5 hadi 7 zaidi kuliko wanafunzi ambao hawanusi harufu hiyo.

Mark Moss kutoka Chuo Kikuu cha Northumbria anasema matokeo ya kutumia mmea huo yalikuwa sawa pia kwa watu wazima.

Dkt Moss alisema utafiti huo unaonekana kutilia mkazo itikadi kuhusu uwezo wa mmea huo.

Amesema kwa miaka mingi, mmea huyo umehusishwa na uwezo wa kukumbuka mambo.

Enzi za kale, wanafunzi Wagiriki walikuwa wakijifunga shada la maua shingoni walipokuwa wanafanya mitihani.

Na Ophelia, katika mchezo wa kuigiza wa Hamlet wake William Shakespeare, kuna wakati husema: "Kuna rosemary, hiyo ni ya ukumbusho."

Nguvu za tiba

Utafiti huo, ambao matokeo yake yatawasilishwa wiki hii katika mkutano mkuu wa Chama cha Wanasaikolojia cha Uingereza, utakuwa unatilia mkazo "busara ya miaka mingi" kwamba rosemary husaidia kumbukumbu.

Katika utafiti huo uliofanywa na Dkt Moss na Victoria Earle, wanafunzi 40 wa miaka 10 na 11 walifanya mitihani kadhaa ya kupima uwezo wao wa kukumbuka mambo wakiwa kwenye vyumba vyenye harufu ya rosemary na wakiwa vyumba ambavyo havina harufu ya mmea huo.

Wanafunzi walioshirikishwa hawakuwa wanafahamu kwamba walikuwa wanachunguzwa kuhusu uwezo wa harufu hiyo.

Lakini Dkt Moss anasema wale waliokuwa vyumba vyenye harufu ya rosemary waliimarika kwenye matokeo yao kwa 5% hadi 7%.

Wanafunzi waliolalamika kwamba walibaguliwa na walimu wao walikuwa na uwezekano mara 1.7 zaidi wa kujihisi kwamba wametengwa.
Utafiti huo kuhusu uwezo wa rosemary ulifanywa baada ya utafiti mwingine mdogo kudokeza kwamba huenda kuna uhusiano kati ya rosemary na uwezo wa kukumbuka mambo.

Dkt Moss alisema utafiti wake na Earle ulithibitisha kwamba mmea huo una faida kwa watoto na watu wazima.

Lakini alisema kuna tofauti katika kiwango cha manufaa kwa watu mbalimbali. Kuna baadhi ambao hawakufaidi kwa vyovyote vile katika uwezo wao wa kukumbuka mambo.
'Ujumbe kwa ubongo

Alisema uwezo wa binadamu kunusa huwa wa juu na hutuma ujumbe kwenye ubongo, ambao huanzisha shughuli nyingine mwilini.

Huwa kuna chembe za kusafirisha ujumbe wa neva katika ubongo ambazo huhusika katika kumbukumbu, na Dkt Moss anasema huenda chembe hizi ndizo huathiriwa na harufu ya rosemary.

Alisema ni kama dawa, ambapo ubongo huathiriwa na kitu ambacho mtu anapumua.
Via>>BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post