BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limeendelea kupokea umati wa watumishi wa umma waliojitokeza kukata rufaa na kuhakiki vyeti vyao ambao majina yao yalibainishwa kwenye orodha iliyotolewa na serikali ya watumishi walioghushi vyeti.
Gazeti la Habarileo lilishuhudia umati huo wa watumishi ukiwa umekusanyika katika ofisi hizo za Necta zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam huku baadhi yao waliowahi wakipewa namba na kuingia ndani kuwasilisha vyeti na wengine wakisubiri nje kupangiwa utaratibu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari wa baraza hilo, John Nchimbi alikiri baraza hilo kupokea umati mkubwa wa watumishi hao wanaokata rufaa ambao wanaongezeka kila siku.
Nchimbi alisema kwa sasa kuna makundi matatu ya watumishi hao yakiwemo kundi la watumishi walioghushi vyeti, watumishi waliowasilisha vyeti visivyokamilika na watumishi wenye vyeti vyenye utata ambavyo cheti kimoja kinatumiwa na zaidi ya mtumishi mmoja.
“Kiutaratibu sisi Necta tunatakiwa kuwashughulikia watumishi waliopo kwenye orodha ya vyeti vyenye utata, tunamtaka mtumishi aliyekata rufaa awasilishe vyeti vyake halali kwetu tunampa namba na anaondoka zake,” alisema Nchimbi.
Hata hivyo, alifafanua kuwa pamoja na ukweli huo, makundi yote matatu yamejitokeza na kuwasilisha rufaa na malalamiko yao Necta jambo ambalo baraza hilo inabidi liwahudumie.
Alisema kiutaratibu watumishi ambao vyeti vyao havijakamilika, wanatakiwa kuwasilisha rufaa zao kwa waajiri wao na vielelezo baada ya hapo waajiri hao watawasilisha mbele ya baraza hilo rufaa hiyo iliyoambatana na vielelezo.
Kwa upande wa watumishi wenye vyeti vya kughushi wanapaswa kuwasilisha rufaa zao kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala wa Bora ambaye ndiye atakayewasilisha rufaa hizo kwa baraza hilo la mitihani.
“Bahati mbaya kwa sasa wote wanakuja kwetu lakini tunawahudumia, tunajitahidi kuhakikisha kila mtu anapata haki yake, utaratibu mzijma ukikamilika kwa tarehe iliyotangazwa na Rais John Magufuli, tutapeleka idadi ya waliokata rufaa na matokeo kunakohusika,” alifafanua.
Baadhi ya watumishi waliojitokeza katika eneo hilo la Necta, walioomba kutotaja majina yao kwa usalama wao kikazi, walibainisha kuwa wameamua kukata rufaa kwa kuwa wana uhakika hawajaghushi vyeti vyao.
“Mimi nimeshangaa kuliona jina langu kwenye orodha ya walioghushi kwanza nimeshtuka sana, nimeambiwa vyeti vyangu vinatumiwa na watu wengine ambao hata siwajui, nimekuja hapa kuthibitisha kuwa mimi ndio mmiliki halali wa vyeti vyangu,” alisema mmoja wa watumishi hao aliyetambulisha kuwa anafanya kazi kwenye halmashauri.
Kwa upande wake, mtumishi mwingine aliyedai kuwa ni mwalimu, alipongeza utaratibu uliowekwa na Necta wa kusikiliza malalamiko ya watumishi na kubainisha kuwa tangu afike hapo baada ya kupewa namba amefanikiwa kuwasilisha vyeti vyake na sasa anasubiri matokeo.
Hata hivyo, mtumishi huyo alionyesha wasiwasi juu ya ajira yake na kubainisha kuwa kuwa kwa kuwa jina lake limeshaondolewa kwenye mfumo wa malipo wa mwajiri wake, huenda ikachukua muda mrefu kurejeshwa tena hivyo hali yake kimaisha kuzidi kuwa ngumu.
Kwa upande wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi Mtendaji, Profesa Lawrence Museru pamoja na Ofisa Habari wa hospitali hiyo, Aminiel Eligaesh kwa ajili ya kupata ufafanuzi juu ya athari zilizopatikana baada ya watumishi wa hospitali hiyo 134, kusimamishwa kazi kwa kughushi vyeti, bila mafanikio jana kwa kuwa viongozi hao walikuwa kwenye kikao kutwa nzima.
Juzi hospitali hiyo ilitoa orodha na vitengo vya watumishi wake 134 waliobainika kughushi vyeti vya sekondari na kutangaza wazi kuwa wamekosa sifa ya kuwa watumishi wa umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki hivi karibuni alitoa orodha ya watumishi 9,932 wanaodaiwa kughushi vyeti ambao kwa mujibu wa Dk Magufuli aliwapa muda wa siku 14, kujiondoa kazini na wale wataokaidi watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kifungo cha miaka saba jela.
Hata hivyo, ikiwa imepita wiki moja tangu kutolewakwa orodha hiyo, juzi Katibu Mkuu wa Utumishi, Dk Lauren Ndumbaro alitoa tena orodha ya watumishi 2,016 wanaodaiwa kuwasilisha vyeti visivyokamilika.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, watumishi hao ambao wengi wao wanatokea kwenye taasisi na mashirika ya serikali, wametakiwa kuhakikisha hadi mwishoni mwa mwezi huu, wawe wamewasilisha vyeti vyote vilivyokamilika ndipo watakapothibitishwa utumishi wao.
Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu Lucy Ngowi anaripoti kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, imeondokewa na watumishi 383 ambao wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi pamoja na vile vyenye utata baada ya kufanyika kwa uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma.
Watumishi walioondoka wametokea idara za elimu, uhasibu, biashara, uvuvi, afya, sheria, maendeleo ya jamii na utawala. Kuondoka kwa watumishi hao kumeilazimu manispaa hiyo kubadili utaratibu wake kwa kuwarudisha kazini wote waliokuwa likizo pamoja na kuondoa shifti tatu na kubakiza shifti mbili inayowalazimu wafanyakazi kufanya kazi kwa saa 12.
Kwenye elimu manispaa hiyo imehamisha walimu kujaza nafasi katika shule zilizokuwa na uhitaji zaidi, na kwenye malindo wameongeza nguvu kwa kutafuta vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Msongela Palala alisema jana alipozungumza na gazeti hili kuhusu wafanyakazi hao waliogundulika katika manispaa yake. Alikiri kuwa kuondokewa kwa watumishi hao kumeiathiri manispaa hiyo kwa kuwa walimu wa msingi pekee waliokumbwa na sakata hilo idadi yao ni 165, madaktari watatu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana na mmoja katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
Vilevile madaktari wasaidizi sita, matabibu, maofisa uuguzi hivyo kufikisha sekta hiyo ya afya kufikia 98. Alisema watumishi kutoka utawala, maendeleo ya jamii, sheria, ujenzi, mipango miji na ugavi wamefikia 38.
Mkurugenzi huyo alisema watumishi waliogundulika vyeti vya kugushi katika awamu ya kwanza walikuwa 330, awamu ya pili wale wenye vyetu vyenye utata ni 53. Alisema miongoni mwa watumishi hao waliokumbwa na sakata hilo wengi wao hawana vyeti vya kidato cha nne kwa kuwa ajira zao hazikuwataka wapeleke vyeti hivyo kwa mfano walimu wa UPE pamoja na wauguzi wa afya ambao hawakuwa ni lazima wawe na cheti hicho cha kidato cha nne.
Alisema kutokana hali hiyo manispaa hiyo imejipanga kuboresha kwenye maeneo yaliyoathirika kama elimu pamoja na afya. “Kwenye elimu tumejipanga vizuri katika maeneo yaliyoathirika zaidi kwa kuwahamisha walimu kutoka sehemu ambazo hazina uhitaji na kuwapeleka kwenye mahitaji zaidi,” alisema na kuongeza shule ya sekondari ya Pugu wamepeleka ofisa ugavi kwenda kusaidia baada ya aliyekuwepo naye kukumbwa katika sakata hilo.
IMEANDIKWA NA HALIMA MLACHA- HABARILEO
Social Plugin