Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE JOHN HECHE AZIDIWA AKIMBIZWA HOSPITALI

Mbunge  wa Tarime Vijijini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche ameshindwa kuendelea kuhudhuria vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini hapa, kutokana na matatizo ya kiafya na kulazimika kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.

Heche alipata tatizo la afya na kufikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma jana alfajiri. Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Caroline Damian alikiri kuwa Heche, alipokewa hospitalini hapo alfajiri ya jana na kuhudumiwa kwa muda kabla hajasafirishwa kupelekwa mahali ambako hakuwa tayari kupataja.

“Hatujampa rufaa ila matibabu yake yanaratibiwa na Kliniki ya Bunge, hivyo tulimpokea na kumhudumia kwa muda kabla taratibu za kumsafirisha hazijakamilika, tulipoambiwa ndege ya kumsafirisha ipo tayari, aliondolewa kwetu na kusafirishwa kwa ajili ya matibabu,”alieleza daktari huyo.

Awali, mbunge huyo alipata tatizo la afya na kulazimika kuwa chini ya uangalizi wa kitabibu. Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, alikaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni akijibu maswali ya wananchi walihoji hali ya mbunge huyo, ambaye ilikuwa ikielezwa kuwa hospitalini.

Kabla ya muda huo kuwadia, ilielezwa kuwa Heche alipata maumivu ya tumbo kabla hajapelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili ambako alifanyiwa upasuaji. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema Taifa, Tumaini Makene jana  alithibitisha taarifa ya kuugua ghafla kwa Heche na kuletwa jijini Dar es Salaam katika hospitali hiyo.

“Ni kweli Heche aliugua ghafla akiwa Bungeni huko Dodoma, alisafirishwa kwa ndege jana asubuhi saa moja na kuletwa Muhimbili ambako anaendelea na matibabu,” alisema Makene.

Ofisa Habari wa Muhimbili, Neema Mwangomo alithibitisha kupokelewa Heche jana saa nne asubuhi na kwamba anaendelea na vipimo kubaini nini tatizo lake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com