Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbinga, Leonard Kambo ambaye alidaiwa kuuawa na watu watano wa kanisa hilo amekutwa akitoa ubatizo katika usharika wa KKKT Kitandilo, Makambako, Mkoani Njombe.
Wakati Mchungaji huyo aliyedaiwa kuuawa mwaka 2011 akionekana akitoa ubatizo kanisani, watu waliodaiwa kumuua mchungaji huyo wamo mahabusu tangu mwaka huo 2011.
Ndugu wa watuhumiwa wa mauaji hayo ndio waliohaha kusaka picha ya mchungaji huyo baada ya kupata taarifa kwamba alihamishiwa eneo la Makambako baada ya kutokea tuhuma kwamba ameuawa.
Kwa mujibu wa habari hizo, baada ya ndugu kupata taarifa kwamba mchungaji huyo yupo hai, walitumia kila njia kupata picha yake ili itumike kama ushahidi kwamba yupo hai na tuhuma dhidi ya wauaji si za kweli.
Muumini mmoja wa kanisa hilo alieleza kuwa ndugu wa watuhumiwa hao walihakikisha wanamnasa mchungaji huyo kwa kamera popote alipo ili wasitishe kifungo cha ndugu zao na uongo dhidi yao.
Mmoja wa watuhumiwa wa kesi hiyo ambaye alikamatwa kisha kuachiliwa huru, Leonard Myale alisema kuwa baada ya kumuona na kupata picha ya mchungaji huyo akiwa hai, watathibitisha Polisi ili akamatwe na watuhumiwa wengine waachiwe huru.
“Tumeteswa sana, tumedhalilishwa, tumepuuzwa na kusemwa vibaya na Wakristo wenzetu, ndugu zetu na hata jamii haikutuamini juu ya tuhuma hizi za uongo ambazo hata Polisi walitubambikiza kesi bila kufanya utafiti wa kina. Tulikanusha kuhusika na mauaji hayo lakini Polisi hawakutuamini. Sasa tunaamini tuko huru, wenye mamlaka watachukua hatua za kutusaidia” alisema Elenia Mhoka mtuhumiwa mwingine wa mauaji hayo.
Aidha aliyewahi kuwa Mchungaji wa KKKT Kitandililo, Geofrey Mtweve, alitafutwa ili kueleza kuhusiana na suala hilo, lakini hakutaka kuzungumza chochote na kusema kuwa yeye siyo msemaji wa kanisa hilo.
“Mimi si msemaji wa kanisa ila ni kweli nilikuwa Kitandililo, uongozi umenihamisha kuja Ilembula, nimebadilishana na Mchungaji Leonard Kambo, ambaye ndiye nimemkabidhi usharika, mengine sifahamu lolote. Wasiliana na uongozi wa Jimbo,” alisema Mtweve.
Aidha mchungaji Kambo alipotafutwa na kuulizwa kuhusiana na yeye kutuhumiwa kifo na kama ni kweli aeleze kuwa alifufuka lini, lakini mawasiliano yakawa mabovu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, baada ya kuelezwa tukio hilo aliomba kupatiwa picha na namba ya RB na kuahidi kuwa atalifanyia kazi suala hilo.
Credit: TanzaniaDaima
Social Plugin