Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MITANDAO YA KIJAMII INAVYOWEZA KUNUFAISHA BIASHARA YAKO


Na Jumia Travel Tanzania 

Mitandao ya kijamii si tu inatumika kwa kuwaunganisha watu au kupata taarifa mbalimbali bali hata kibiashara pia. Yapo makampuni, mashirika na watu binafsi wanaitumia vema kibiashara na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa tu. Sasa na wewe unashindwa nini kufanya hivyo ikiwa unawashuhudia wengine wakinufaika na biashara zao?


Lakini kabla ya kuamua kutumia mitandao ipi ya kijamii kwa ajili ya biashara yako, Jumia Travel ingependa kukushauri kwanza kuzingatia masuala matatu yafuatayo: 

Chagua mitandao wa kijamii itakayofaa. Sio mitandao yote inaweza kukusaidia kibiashara kama unavyoona wengine wanavyoitumia. Kwa mfano, mtandao wa facebook unafaa zaidi kwa kuwashirikisha wateja wako taarifa, picha na video kuhusu bidhaa zako, instagram nayo ni picha kwa kiasi kikubwa ingawa wametambulisha na huduma ya video pia, huku Twitter yenyewe kitaalamu inafaa zaidi kama uko na mtu ambaye atakuwa makini katika kujibu masuala mbalimbali yatokanayo na taarifa unazowashirikisha wateja wako paop kwa papo. 

Jiwekee malengo unayotaka kuyafanikisha. Kufungua kurasa za mitandao ya kijamii pekee bila ya kuwa na malengo maalum haitokusaidia kibiashara. Hakikisha unakuwa na malengo uliyojiwekea na mikakati ya kuyafanikisha kupitia njia za mitandao ya kijamii uliyoichagua. Je ni kutangaza bidhaa au huduma mpya? Au kuweka hamasa juu ya kampeni fulani?


Pangilia maudhui utakayokuwa unayaweka mtandaoni. Haimaanisha kuwa na kurasa za mitandao ya kijamii basi ndio uwe unaweka taarifa bila mpangilio. Pangilia muda wa kuweka taarifa mbalimbali kwenye mitandao hiyo ili kuwapa fursa wateja wako kuelewa na hatimaye kuchukua hatua. Ukiwa unaweka taarifa mbalimbali bila ya mpangilio utakuwa unawachosha na kuwakera wateja kwani watashindwa kuzisoma na kuzielewa zote. Ipo mifumo mbalimbali inayoweza kukusaidia kufanya hivyo kama vile Hootsuite.
Mitandao ya kijamii inazo faida kadhaa kwenye biashara ambazo mtu hawezi kuzigundua moja kwa moja. Ila kwa namna moja ama nyingine ukiitumia kikamilifu zifuatazo ni faida ambazo unaweza kuziona kwenye biashara yako:

Kuifanya biashara yako kujulikana. Kwa dunia tunayoishi sasa hivi mtu akitaka kufahamu kuhusu biashara yako, kitu cha kwanza atakachokifanya ni kuitafuta kwenye mitandao ya kijamii. Kwa sababu ana uhakika huko atapata taarifa zote anazozihitaji. Hivyo basi hakikisha unapofungua akaunti basi inakuwa imejitosheleza, kwa mfano kama ni hoteli, hakikisha umeweka jina sahihi, inatoa huduma gani, mahali ilipo, mawasiliano, picha na video pia vitasaidia kumuongoza mteja.

Kuwavutia wateja wapya. Mteja wako wa siku zote anaweza asijisumbue kuingia mitandaoni kutafuta taarifa za biashara yako, ila asiyekufahamu atafanya hivyo. Kwa hiyo kupitia mitandao hii unaweza kujikuta wateja wapya wanaongezeka kila kukicha na usijue wametokea wapi.

Kuongeza umaarufu wa biashara yako. Ukiwa unajishughulisha sana kwenye mitandao ya kijamii inakuwa ni rahisi hata watu wanapolitafuta jina la biashara yako kuonekana kwa urahisi. Umaarufu wa jina fulani hauji tu kwa kufungua kurasa za mitandao ya kijamii na kukaa kimya. Hakikisha unakuwa unaweka taarifa mbalimbali ili watu wanapotafuta kitu fulani jina la biashara yako liwe kipaumbele kuonekana au kutokea.

Kuipa biashara yako mamlaka katika soko. Mtu anaweza kujiuliza mamlaka inakuja vipi kwenye upande wa biashara. Hali hii hutokea pale unapokuwa umejitosheleza kwenye masuala mbalimbali hususani katika sekta husika. Kwa mfano, nchini Tanzania unapotafuta habari mbalimbali mtandaoni jina la blogu ya Michuzi hutokea kwa haraka zaidi. Ndivyo hivyo itakavyokuwa biashara yako ikiwa inajishughulisha mara kwa mara kuwapatia wateja taarifa mbalimbali kwenye sekta uliyopo. 

Huchochea mauzo kwa kiasi kikubwa. Kupitia ukaribu unaouweka na wateja wako mtandaoni ni rahisi kwao kutumia bidhaa au huduma zako. Mitandao ya kijamii hujenga hali ya uaminifu kwani unapoweka taarifa mtandaoni na mteja akaulizia taarifa zaidi na wewe ukamjibu unakuwa umetengeneza ukaribu baina yenu. 

Hupunguza gharama za matangazo na masoko. Ukilinganisha na njia nyingine za matangazo kama vile luninga, redio, mabango na magazeti; mitandao ya kijamii ni rahisi zaidi. Wamiliki wa mitandao kama vile Facebook, Twitter, Instagram na Youtube huwachaji watumiaje wake kiasi kidogo sana cha fedha kutangaza biashara zao ambazo kila mtu anaweza kuzimudu. Pia ni rahisi kufuatilia mwenendo wa matangazo unayoyalipia yamewafikia watu wangapi.

Kuwa karibu na wateja wako. Vifaa kama vile kompyuta, tabiti na simu za mkononi vimerahisisha watu kuwasiliana na kupata taarifa kwa haraka zaidi. Hivyo unapokuwa kwenye mitandao ya kijamii unakuwa na fursa ya kuwafikia wateja wote hao walioko kwenye mifumo hiyo. Kwa kiasi kikubwa ukaribu unakuja pale unapokuwa unawashirikisha wateja wako taarifa mbalimbali na kujibu maswali yao mara kwa mara. 

Kuwapatia taarifa zaidi wateja wako. Kwa sasa hivi kupiga simu ya huduma kwa wateja au kutembelea tovuti kwa ajili ya taarifa ya kampuni fulani imekuwa nadra sana. Hayo yote yanakuja mwishoni baada ya mteja kutopata chochote mtandaoni kitu ambacho pia kitapunguza uaminifu wa wateja kwa biashara yako. Taarifa zilizopo kwenye mitandao yako ya kijamii zinatosha kabisa kumfanya mteja kuchukua maamuzi ya kutumia bidhaa au huduma zako.

Sio lazima utumiapo mitandao ya kijamii uzione faida zote hizo zilizoorodheshwa hapo juu. Lakini kwa mujibu wa tafiti mbalimbali ukiyazingatia matumizi sahihi na kwa umakini hutoona haja ya njia nyinginezo. Jumia Travel inaamini kwamba haujachelewa kuitangaza biashara yako mtandaoni na kama ulishafanya hivyo basi pitia upya na uone kama unayazingatia yaliyoandikwa kwenye makala haya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com