IKIWA ni siku chache baada ya mkazi wa Mtaa wa Kanyerere jijini Mwanza, Maximilian Ndegere (40) Mwanza kumuua mkewe Teddy Patrick (38) kwa risasi na kisha yeye kujiua, matukio ya wanandoa kuuana kutokana na migogoro ya kifamilia na wivu wa kimapenzi yameendelea kutokea jijini Mwanza.
Kutokana na mauaji hayo, Jeshi la Polisi jijini Mwanza linamsaka kwa udi na uvumba mwanamume ambaye amemuua mkewe kwa kile kinachoonekana kuwa ni wivu wa mapenzi na kisha kutokomea kusikojulikana.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ahmed Msangi alisema polisi wanamtafuta Charles John (35) ambaye ni mkazi wa Pasiansi Mashariki katika Kata ya Pasiansi, Manispaa ya Ilemela.
Kamanda Msangi alisema John alishiriki katika tukio la kumpiga mkewe Ester Charles (30), Mei 30 mwaka huu saa 9.09 alfajiri na kumwacha akiwa amekufa chumbani kwake huku mwili ukiwa na majeraha.
Alisema katika kipindi chote cha mahusiano yao, wawili hao walikuwa kwenye migogoro ya mara kwa mara ya kifamilia, ambayo mwanamke huyo alikuwa akimtuhumu mumewe kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine.
Alisema siku hiyo ya ugomvi, majirani walisikia ugomvi ukiendelea kati ya wanandoa hao, na walikwenda kuwasuluhisha na kuwasaidia kwa vile walizoea kuwasikia wakipigana mara kwa mara na kisha kuelewana na kuendelea na maisha yao kama kawaida.
“Baada ya muda kupita majirani hawakusikia ugomvi tena, na kudhani kuwa wameelewana, lakini baadaye alisikika mtoto mdogo akilia kwa muda mrefu ndipo majirani walikwenda dirishani kuangalia na kumuona mama yake akiwa amelala kimya kitandani bila ya kumsaidia mtoto, huku baba yake akiwa hayupo, walipata shaka na kutoa taarifa polisi,” alifafanua Kamanda Msangi.
Alisema baada ya polisi kupata taarifa walikwenda kwenye eneo la tukio na kumkuta Ester akiwa tayari amekufa huku mwili wake ukiwa na majeraha ya kupigwa na kitu kizito. Aidha shingo yake ilikuwa imekabwa na kitambaa kigumu.
“Baada ya mume, kuona mke wake amekufa, huyu aliamua kukimbia kusikojulikana na sisi tumeanzisha msako mkali wa kumtafuta na tutahakikisha tunamkamata,” alieleza.
Alisema polisi inaendelea na uchunguzi wa mauaji hayo ya kinyama na kuongeza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi na uchunguzi utakapokamilika utakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya maziko.
Katika tukio jingine, Kamanda Msangi alisema Melikiad Misana (50) ambaye ni mkazi wa Miriti wilayani Ukerewe amekufa wakati akiwa njiani kukimbizwa hospitalini baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali mgongoni kwake upande wa kushoto na mkewe Bukherehere William (25) ambaye naye alijeruhiwa na mumewe kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kwenye mikono yake, tumboni na kusababisha utumbo kutoka nje baada ya kuzuka kwa ugomvi baina yao.
Kamanda Msangi alisema uhalifu huo ulifanyika Mei 29, mwaka huu saa 4.15 asubuhi katika Kitongoji cha Kamengo Kijiji cha Muriti Tarafa ya Ilangara wilayani Ukerewe, ambako inadaiwa siku ya tukio, Bukherehere hakulala nyumbani kwake, lakini baadaye alirudi nyumbani akiwa amelewa chakari kitendo ambacho hakikumfurahisha mkewe.
“Kutokana na hali hiyo, wanandoa hao walijikuta wakiingia kwenye ugomvi na kisha kuanza kupigana kwa kutumia vitu vyenye ncha kali, huku kila mmoja akimchoma mwenzake hali iliyosababisha wote kupoteza fahamu kutokana na majeraha waliyopata,” alifafanua Kamanda Msangi.
Alisema baada ya majirani kupata taarifa, walitoa taarifa polisi na polisi walipofika kwenye eneo la tukio waliwachukua majeruhi na kuwakimbiza hospitalini, lakini wakiwa njiani mwanamume alifariki dunia huku mkewe akiwa hajitambui.
Alisema majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe akiendelea kupatiwa matibabu akiwa chini ya ulinzi wa polisi huku polisi wakiendelea na upelelezi kuhusu mauaji hayo. Alisema hali yake sio nzuri na mwili wa mumewe umehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi
.
IMEANDIKWA NA NASHON KENNEDY,-HABARILEO MWANZA