Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

POLISI WATUHUMIWA KUUA MWANAFUNZI WA CHUO CHA UVUVI BAGAMOYO

Askari  wa Jeshi la Polisi, Kituo cha Kigamboni wanadaiwa kumuua kwa kumpiga risasi tumboni, mwanafunzi wa Chuo cha Uvuvi Mbegani, Bagamoyo Boniventure Kimali (25), wakimtuhumu kuwa ni jambazi.


Tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa 3:30 usiku wa kuamkia juzi huko Kigamboni Vijibweni, nyumbani kwa kaka wa marehemu aitwaye, Naftan Barampami ambaye alikuwa akiishi naye.

Akisimulia jinsi ilivyokuwa, Barampami alisema usiku huo wakiwa bado wapo nje ya nyumba yao huku kila mmoja akiendelea na shughuli zake ndogo ndogo na wengine wakiwa wamejipumzisha, ghafla walishangaa kusikia milio ya risasi zilizopigwa mfululizo.

“Tulishtuka, milio hiyo ilitokea upande wa uwanjani ambapo ni jirani na nyumbani kwetu, tuliogopa kila mtu ilibidi atafute namna ya kujiokoa, tulikimbia, mimi nilikimbilia ndani, Boni alikimbia kuelekea nyuma ya nyumba yetu,” alisema.

Alisema akiwa ndani ya nyumba yake alisikia mtu akilia huku akiwasihi watu waliokuwa wamemzingira wasimuue.

“Ikabidi nisogee jirani zaidi na dirisha, nikakaa kwa utulivu na kuangalia nje kupitia dirishani kilichokuwa kikiendelea, ghafla nilimsikia Boni akilia kwa uchungu huku akiugulia maumivu, kumbe walikuwa tayari wamempiga risasi,” alisema.

Alisema askari wote walikuwa wamevaa kiraia, marehemu alikuwa akiendelea kuwasihi wasimuue huku akiwasihi wamuwahishe hospitalini kwani alikuwa akisikia maumivu makali.

“Aliwaomba wampekele hospitali na watujulishe ndugu zake lakini hawakumsikiliza, punde alifika mwenzao ambaye alishtuka na kuwaeleza wenzake wamefanya kosa kwani waliyempiga risasi si jambazi ambaye walikuwa wanamtafuta,” alisema.

Alisema japo alitamani kutoka nje ili akamsaidie ndugu yake lakini alihofia maisha yake kwani mmoja wa askari hao alionya asitokee mtu yeyote katika eneo hilo.

“Niliogopa mno, ikabidi nibaki pale pale dirishani nikifuatilia, nilihofu iwapo nisingetii amri hiyo na kutoka nje na mimi wangenipiga risasi,” alisema.

Barampami  alisema akiwa dirishani hapo, alimshuhudia yule askari aliyefika katika eneo hilo akichukua simu yake na kuwasiliana na wenzake ambao aliwataka wawahishe gari haraka katika eneo hilo.

“Lilipofika, walimchukua marehemu wakampakiza ndani ya gari hilo na kuondoka naye, wakati huo alikuwa bado anaugulia maumivu,” alisema.

Alisema baada ya muda kupita eneo hilo lilikuwa shwari akatoka nje na baadhi ya ndugu zake na kwenda kituo kidogo cha Polisi Vijibweni.

“Pale tuliuliza kama walikuwa wamemfikisha hapo, askari tuliyemkuta alituambia walielekea Kituo Kikuu cha Polisi Kigamboni, tukaenda huko,” alisema.

Alisema walipofika walipokewa na baadhi ya askari waliowakuta ambao waliwaeleza ndugu yao alikuwa amepelekwa Hospitali ya Vijibweni kwa matibabu.

“Tukaenda hadi huko lakini daktari mmoja alituambia hawakumpokea na kumuhudumia kwani hawakuwa na maelezo yaliyojitosheleza, tukarudi Kigamboni lakini awamu hii hatukupewa ushirikiano kama awali, tulipewa amri tusisogee katika eneo hilo,” alisema.

Alisema waliwasiliana na ndugu zao kuwaeleza hali waliyoikuta akiwamo ndugu yao Daudi Gwelenza ambaye anafanya kazi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

“Tuliwataka wajaribu kupita katika hospitali mbalimbali kumtafuta hasa Muhimbili, ndipo Gwelenza akaenda pale chumba cha kuhifadhia maiti,” alisema.

Gwelenza alisema alipofika hapo alielezwa kuna mwili ambao umefikishwa na askari wa Kigamboni, aliruhusiwa kuuona ndipo akakuta ni ndugu yake huyo.

“Nilimuangalia sura nikakuta ni yeye, nikamwangalia tumboni kweli alikuwa amepigwa risasi eneo la kushoto tumboni, alikuwa na mchanga mwingi wa bahari inaonesha huenda aliburuzwa, nilisikitika mno sikuweza tena kuendelea kuangalia tena,” alisema.

Aliongeza “Lakini nishangaa kwanini katika maelezo yaliyoandikwa juu ya taarifa ya marehemu hawakuandika kwamba amepigwa risasi, waliandika tu amepigwa na waliandika hajulikani jina lake, yaani kama vile walimuokota mahali akiwa ameuwawa.

Katika eneo hilo kulipatikana maganda mawili ya risasi yenye namba 311 (10) na 10 (77).

Msemaji wa familia, Goodluck Kimali ambaye ni kaka wa marehemu, alisema kitendo kilichofanywa na askari hao hakivumiliki.

“Kwa mujibu wa majirani na mashuhuda wa tukio hili, wanasema angewahishwa hospitalini asingepoteza maisha, kwanini hawakumuwahisha huko, kwanini walimpiga risasi tumboni na si mguuni ili asiwakimbie, kwa sababu hakuwa na silaha yoyote, kwanini walimuua,” alihoji.

Alisema tangu kutokea kwa tukio hilo hakuna askari yeyote aliyefika nyumbani hapo kukagua, kujiridhisha juu ya kile walichokuwa wakimtuhumu marehemu.

“Hatujamuona askari hata mmoja kukagua, kwanini hawajafika kufanya ukaguzi, hii inamaanisha wanajua walichokifanya, kitendo hiki hakivumiliki, Tanzania ni nchi ya amani, askari anapaswa kulinda raia na mali zake, lakini imekuwa kinyume chake,” alisema.

Alisema ingawa wanafuatilia kwa ukaribu suala hilo hata hivyo hawaoni kama kweli watasaidiwa kupata haki ya ndugu yao.

“Kuna urasimu mwingi nauona, tunaomba watupe mwili wa ndugu yetu tukampumzishe, maana hata tukisusa na kuwaachia hawawezi kurejesha uhai wake, lakini vitendo hivi vikomeshwe, sisi tunavumilia lakini ipo siku raia watachoka,” alisisitiza.

Alisema watakapokabidhiwa mwili huo, wanatarajia kuusafirisha wakati wowote hadi kijijini kwao Mwayeye, Wilaya ya Buligwe mkoani Kigoma kwa ajili ya maziko.

Mkurugenzi wa Mafunzo na Utafiti wa Chuo cha Mbegani, Ambaksye Simtoe alisema tukio hilo limewashtua kwani marehemu alikuwa kijana mtulivu, msikivu na mpole.

“Alikuwa anasoma kozi ya Uchakataji Samaki, Ubora na Masoko, ngazi ya Diploma, mwaka wa tatu, Juni, mwaka huu angehitimu masomo yake.

“Alikuwa yupo field (mafunzo kwa vitendo) katika Soko la Kimataifa la Samaki Feri, tumesikitika mno, kifo chake kimekuwa cha ghafla hatukutarajia kama ipo siku haya yatatokea,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com