ALIYEKUWA Muu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecki Sadiki (pichani), amesema ameamua kuondoka serikalini baada ya utumishi wa muda mrefu na anakwenda kupumzika mkoani Mwanza huku akiwa mfugaji wa samaki.
Aidha Sadiki alisema pia kulingana na afya yake, anahitaji kupisha vijana wadogo wamsaidie Rais Dk John Pombe Magufuli kulingana na kasi yake kwani yeye ameepuka kumkwaza rais wakati wa utekelezaji wa majukumu yake kama mkuu wa mkoa. “Uamuzi huu wa kupumzika nilimuomba rais kwa muda mrefu sana, na nikirudi kijijini nitaendelea na ufugaji Samaki maana nilishaandaa bwawa la kufugia, nitaendelea nalo huku nikiwaza jambo lingine la kufanya,” alisema.
Sadiki alisema hayo jana wakati wa mahojiano maalum na Habarileo kuhusu sababu zilizochangia kumuomba Rais Magufuli kuacha kazi yake ya ukuu wa mkoa wa Kilimanjaro. “Namshukuru rais kuridhia ombi langu, nimetumikia serikali tangu mwaka 1999 nikiwa mkuu wa wilaya na baadaye mkuu wa mkoa kuanzia mwaka 2005 hadi sasa ninapoondoka mwenyewe... nimeona ni wakati muafaka kumweleza aliyeniteua kuwa nahitaji kupumzika nikiwa na akili timu na afya njema,” alisema.
Alisema Sababu nyingine kubwa ni kuhofia afya yake kutomudu kasi ya rais Magufuli, kwani alifanywa upasuaji mwaka 2012 na 2014 nchini India ingawa hakutaka kuweka wazi maradhi yaliyokuwa yakimkabili. “Kama kiongozi muungwana lazma ifike mahali ukiri kwamba wapo vijana wenye uwezo mzuri na kasi ambayo inaendana na serikali ya awamu ya tano... mimi nilishatekeleza wajibu wangu na mchango kwa serikali yangu, sasa inatosha, tupate mawazo na michango ya wengine,” alisema.
Sadiki ambaye amekuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro tangu Machi 13,2016 alipoteuliwa na Rais Magufuli, alisema siyo vibaya kwa kiongozi kujitathmini na kuwaachia wengine kama atabaini kasi yake ya utendaji kazi imeanza kupungua. Kwa upande wake Afisa Habari wa mkoa huo, Shabani Pazi alisema mkoa umeshtushwa na uamuzi wa mkuu wa mkoa kwani hawakuwa wameuratajia kwani tangu amefika mkoani humo watumishi walioko chini yake walianza kumuelewa na kwenda na kasi yake.
“Ni jambo la mshtuko maana sisi kama watumishi wa ngazi za chini, kiongozi anapoteuliwa mnajifunza yale mema anayotenda na kujaribu kufauata kasi yake… sasa tumeanza kumuelewa nini vipaumbele vyake, anahitaji nini, tunashangaa yaliyotokea,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, mkuu wa mkoa Sadiki pamoja na aliyekuwa jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebeisha Sheria Tanzania, Aloysius Mujulizi na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Upendo Msuya waliomba kuacha kazi na rais akaridhia
IMEANDIKWA NA NAKAJUMO JAMES,habarileo MOSHI