MWENENDO wa sakata la kusafirisha mchanga wa madini nje ya nchi, umeonyesha kila dalili kwamba huenda suala hilo sasa likachukua muda mrefu zaidi.
Tangu kamati ya wataalamu wa sayansi iliyoundwa kuchunguza kiwango cha madini katika mchanga uliohifadhiwa katika makontena 277 yaliyoko bandarini Dar es Salaam, iwasilishe ripoti yake, kumekuwapo na sintofahamu ya kujua nani mkweli katika sakata hili kwa maana ya Serikali ya Tanzania kwa upande mmoja na wawekezaji Kampuni ya Acacia kwa upande mwingine.
Wakati ripoti iliyowasilishwa kwa Rais Dk. John Magufuli ikionyesha kuwa kiwango cha madini kinachosafirishwa nje ya nchi ni mara kumi zaidi, ikilinganishwa na kile ambacho kimekuwa kikielezwa, Acacia katika matamko yao mawili waliyoyatoa wiki hii imepinga ripoti hiyo.
Acacia inadai kuwa kama kiwango hicho kinachosemwa katika ripoti ya kamati hiyo ni kweli, basi Tanzania ni nchi inayoongoza duniani kwa kuwa na kiwango kikubwa cha madini ya dhahabu.
Katika tamko lake la mwanzo, Acacia ambayo inachimba madini katika migodi mikubwa ya Bulyanhulu na Buzwagi, ilieleza kuwa katika kila kontena la mchanga kuna madini ya shaba kilogramu 3,000, dhahabu kilo 3, na madini ya fedha kilo 3 na hivyo kufanya thamani ya kontena moja kuwa ni Sh milioni 300.
Katika ripoti ya Kamati ya Rais Magufuli, inaeleza kuwa katika makontena yote 277 yaliyochunguzwa dhahabu ilikuwa na uzito wa kati ya tani 7.8 na 13.16 zenye thamani kati ya Sh bilioni 676 na trilioni 1.147.
Kiwango hicho ni tofauti na makadirio ya wazalishaji na Wakala wa Serikali wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) ambao walionyesha kuwa katika makontena hayo, dhahabu ilikuwa ni tani 1.2 yenye thamani ya Sh bilioni 97.5 tu.
Kwa upande wa madini mengine kama fedha, katika ripoti aliyokabidhiwa Rais Magufuli ilikuwa ni kati ya tani 1.7 na 1.9 yenye thamani kati ya Sh bilioni 2.1 na bilioni 2.4 wakati TMAA ikidai ni kg 831 zenye thamani ya Sh bilioni moja.
Kuhusu madini ya shaba, kamati hiyo ilibaini kulikuwa na tani 1,440.4 na 1,871.4 zenye thamani ya Sh bilioni 17.9 na bilioni 23.3.
Kiwango hicho ni tofauti na nyaraka zilizopatikana bandarini ambazo zilionyesha kulikuwa na tani 1,108 zenye thamani ya Sh bilioni 13.6.
Kinachozua maswali na pengine baadhi sasa kuanza kuona kwamba hatima ya sakata hilo ni mapema mno kujua mwisho wake, ni kitendo cha wadau mbalimbali nao kuhoji uthabiti wa ripoti iliyowasilishwa kwa Rais Magufuli.
Jana gazeti la MTANZANIA Jumamosi lilimkariri aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 1993 – 2005, Andrew Chenge akihoji viwango vya fedha vilivyokadiriwa na kamati iliyokabidhi ripoti yake kwa Rais Magufuli.
“Lakini, ukikaa kimya italeta maneno, maana madini hayo ni mali ya Watanzania kwani wengine wanaamini tunaibiwa na wengine hawaamini. Wakizipiga zile hesabu na mimi ukaniambia ni trilioni, nakataa kwa sababu ‘I know it (najua)’, nadhani kuna mahesabu wameyakosea,” alikaririwa Chenge.
Chenge ambaye ni miongoni mwa watu wanaonyooshewa vidole na baadhi ya wanasheria ambao wanaamini sheria na mikataba mibovu aliyoshiriki kuiandaa wakati akiwa Mwanasheria Mkuu ndiyo kiini cha Serikali kupoteza fedha kama ilivyoanishwa na Kamati ya Rais Magufuli, pamoja na kuhoji huko viwango, alisisitiza kuwa suala la madini lina mambo mengi na hata kushangaa ni kwa nini amekuwa akinyooshewa kidole.
Hoja inayofanana na hiyo ya Chenge kuhusu viwango, inaungwa mkono na mmoja wa maofisa wa ngazi za juu ambaye alipata kufanya kazi katika Wizara ya Nishati na Madini.
Ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa hoja ya kwamba kazi yake itaharibika, aliliambia gazeti hili kuwa kamati hiyo haikueleza ukweli juu ya usafirishwaji wa madini hayo na muda uliotumika kuanza kusafirisha mchanga huo kwenda nje ya nchi kwa uchenjuaji.
“Kama utakumbuka mwaka 2007, Tume ya Jaji Bomani iliundwa kuchunguza mikataba ya madini na sera ya sekta hiyo. Katika kufanya, kazi tume hiyo iliangalia sera na sheria na mwisho ikawasilisha mapendekezo yake serikalini kwa utekelezaji.
“Mwaka 2008, mchakato ukaanza wa kubadili sera na mwaka 2009 sera hiyo ikapatikana na mwaka 2010, tukapata sheria mpya.
“Sera hiyo ilisema tuongeze thamani ya madini kwa kujenga smelting area (eneo la kuchenjua) kwa ajili ya kuchenjua mchanga hapa nchini na wakati huo huo wawekezaji waelimishwe ili wajue namna ya kuomba leseni za uwekezaji huo na namna zitakavyotolewa.
“Kuhusu hoja ya ile kamati kwamba tumekuwa tukiibiwa madini yetu kwa miaka mingi, kamati hiyo haikuwa sahihi kwa sababu migodi inayotoa huo mchanga ni Buzwagi na Bulyanhulu.
“Mgodi wa Buzwagi walianza kusafirisha mchanga nje ya nchi mwaka 2008 na Bulyanhulu wao walianza mapema mwaka 2002 kama sikosei. Kwa hiyo wanaposema tumeibiwa kwa miaka 19, sikubaliani nao,” alisema ofisa huyo.
Mrithi wa Chenge, ambaye naye alizungumza juzi na gazeti dada la MTANZANIA Jumamosi, Frederick Werema, kauli yake kwamba haoni kama kuna tatizo katika suala la kisheria katika mikataba ya madini, nayo imeacha sintofahamu wakati ambapo haijulikani kamati ya wanasheria nayo itakuja na majibu ya namna gani.
Wakati hatima ya suala hilo ikiwa bado haijulikani, hofu imetanda ya Acacia kuifikisha Tanzania katika mahakama za kimataifa.
Hofu hiyo inakolezwa na tamko lao la mwisho walilolitoa juzi, ambalo pamoja na mambo mengine, Acacia walisema kuwa wamejipanga kutumia njia zozote kukabiliana na jambo hilo.
Zipo hisia kwamba uamuzi wa Acacia kuitaka Serikali ya Rais Magufuli iunde tume huru ili kuchunguza upya suala hilo, ni hatua ambayo inaonekana kama mtego kwa Serikali ya Tanzania.
Wapo wanaoamini kuwa Acacia imefanya hivyo kwa malengo mawili, kwamba uamuzi wowote wa Serikali kukataa ama kukubali kutekeleza jambo hilo itakuwa ni mwanya kwao kuishtaki katika mahakama za kimataifa.
Kwamba Serikali ikikataa kuunda tume huru kitakuwa kisingizio namba moja cha utetezi wa kuhalalisha mashtaka yao katika mahakama za kimataifa kwa hoja kwamba tuliomba tume huru wakakataa.
Si hilo tu, inaelezwa kuwa endapo Serikali itakubali ni wazi majibu ya tume huru yanaweza kuwa tofauti na uchunguzi wa Kamati ya Rais Magufuli na hivyo kuipa Acacia hoja za kuipeleka mahakamani.
Kutokana na mwenendo huo na hatua ya Acacia kuomba kuundwa kwa tume huru, Mwanasheria Victoria Mandari alisema inapotokea upande fulani unaomba iundwe tume huru, unapaswa kueleza kwanza kama Kamati ya Rais Magufuli haikuwa huru.
Katika muktadha huo, alisema hawezi kukanusha au kusema chochote kwa sababu hajafanya utafiti wa kubaini kama kamati hiyo haikuwa huru au la kwa kuwa anajua utaratibu wa kamati hufanya kazi kwa maelekezo iliyopewa.
“Kuna suala la usiri pamoja na kufuata hadidu za rejea walizopewa, sasa kama walizingatia hayo na wewe huamini, basi tuambie wazi kwamba kamati haikuwa huru na kama ni hivyo inabidi utueleze haikuwa huru kwa kiwango gani na ili iwe huru ilitakiwa kuwaje. Je iliingiliwa? Je, kuna mkono wa mtu?
“Kwa sababu ili uweze kuhitaji tume huru, unatakiwa uwe umefanya utafiti na umepata majibu ya uhakika ambayo yanapinga ripoti ya uchunguzi wa kamati,” alisema.
Naye Jaji mstaafu, Amir Manento, alisema hawezi kuzungumzia masuala ya madini kwa sababu hana utaalamu wowote kuhusu madini.
Alisema anaamini kuwa kinachosikika kwa sasa nje ya ripoti iliyokabidhiwa kwa Rais Magufuli ni mambo ya kubuni tu.
“Nami nimekuwa ni msikilizaji wa haya yanayozungumzwa kwa sasa baada ya ripoti kukabidhiwa kwa Rais. Najua yanayoongelewa ni masuala ya kubuni tu, kwa sababu neno labda limetawala, hata nyinyi watu wa magazeti mnaandika labda akina fulani matumbo joto na kadhalika.
“Yamekuwa ni mawazo ya watu binafsi ndiyo yametawala, kwa hiyo hata mimi sitaki kutoa mawazo yangu kwa kitu ambacho siwezi kuthibitisha. Kwa ujumla haya tunayoyasikia kwa sasa hayapo kwenye msingi wa sheria ila ni akili ya kawaida,” alisema Jaji Manento.
Katika hatua nyingine, Jaji Manento alihoji maana ya tume huru huku akimtaka mwandishi awaulize Acacia watoe tafsiri halisi.
“Nasikia tume huru, hivi ni nini? Binafsi sijawahi kujihusisha na tume yoyote ile ambayo inasemwa ni huru au si huru. Sasa hao wanaosema wanataka tume huru waulizeni kwamba wanamaanisha nini,” alisema Jaji Manento.
Social Plugin