Serikali imeahidi kuendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wazalendo katika utekelezaji wa miradi mikubwa lakini imewaonya wale ambao wamekuwa wakitekeleza miradi chini ya viwango vilivyowekwa kwenye mikataba.
Hayo yalisemwa jana mjini Dodoma na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa makandarasi ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB).
Samia aliagiza kuwa miradi yote ya thamani isiyozidi Sh bilioni 10 wapewe wakandarasi wa ndani hasa kwa miradi inayotekelezwa kwa fedha za ndani kwani wakandarasi hao watasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania na kuongeza uwekezaji ndani ya nchi.
Alisema kuwapa miradi mikubwa wakandarasi wazalendo kuna faida kubwa kwani kutasaidia kuwajengea uwezo hivyo kuweza kushindana na wakandarasi wa nje hivyo fedha nyingi za serikali kubaki ndani.
“Tanzania bora na yenye viwanda itatokana na wakandarasi bora na wenye uzalendo, hatuwezi kufikia huko tunakotaka kwenda wakati miradi mikubwa ya ujenzi inafanywa na wakandarasi wanje…. miradi ni yetu na fedha ni zetu hivyo lazima tuwape nyinyi,” alisema.
Aidha, aliwataka wakandarasi wazalendo wakamilishe kazi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa pale wanapopewa miradi ili wajenge uaminifu kwa serikali kuendelea kuwaamini na kuwapa miradi mikubwa.
Makamu wa Rais aliwaonya baadhi ya wakandarasi wanaoshirikiana na maofisa wa serikali kuongeza gharama kubwa za ujenzi wa miradi kwa misingi ya rushwa hali ambayo imekuwa ikifuja fedha za serikali.
“Jamani kwenye mkutano huu tujitathimini na tuanze upya maana kuna wenzetu ambao hawana maadili na wanaendekeza rushwa, serikali ikitumia taasisi zake inatekeleza miradi mikubwa kwa gharama ndogo lakini nyinyi wengine mnaweka gharama kubwa ambazo si halisi,”alisisitiza.
Aliipongeza CRB kwa namna inavyoendelea kuratibu kazi za wakandarasi wazawa huku akiitaka kuendelea kuwajengea uwezo ili watekeleze miradi mikubwa kama kampuni ya nje.
“CRB mmefanyakazi kubwa sana kuandaa mkutano huu na kwa kuwa mmekutana hapa naomba mjadiliane kwa uwazi na muelezane ukweli kuhusu changamoto mlizonazo na namna mtakavyozitatua na sisi serikali mkituletea maazimio yetu sisi tunaahidi kuyafanyia kazi,”alisema.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Makame Mbarawa, yeye alisema asilimia 75 ya madeni ya wakandarasi yameshalipwa na yaliyobaki yatalipwa wakati ukifika na aliwaomba wawe wavumilivu wakati huu.
“Msidhani serikali imewasahau, tunafanya kazi kwa bidii kuhakikisha wote mnalipwa kwa sababu sisi tunaamini na tunafahamu kwamba ili makampuni yenu yaendelee lazima mlipwe hela zenu hivyo endeleeni kuchapa kazi hela zilizobaki zinakuja,” aliahidi Profesa Mbarawa.
Mwenyekiti wa CRB, Consolata Ngimbwa, aliomba serikali iharakishe malipo ya wakandarasi kwani wengi wao wako kwenye hali mbaya kifedha. Alisema baadhi ya wakandarasi walifariki dunia kutokana kabla hatajalipwa malimbikizo ya madeni wanayoidai serikali baada ya kukamilisha miradi mbalimbali ya ujenzi.
Alisema wakandarasi wengi wazalendo wana uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi hivyo aliiomba serikali iweke kipaumbele kwa kuwapa miradi hiyo.
Vile vile, aliwageukia wakandarasi ambao wamekuwa na kawaida ya kutekeleza miradi chini ya kiwango na wengine kutokomea mara baada ya kulipwa fedha za awali za ujenzi.
Msajili wa CRB, Rhoben Nkori aliwataka wakandarasi kutekeleza miradi wanayopewa na kuahidi kuwa bodi yake itaendelea kuhakikisha mkandarasi asiye na viwango anafutiwa usajili.