Kiongozi wa timu ya mpira wa kikapu ya Weusi Basketball Club ya jijini Dar es Salaam, Mntambo Mngeja (kulia) akipata maelekezo ya juu ya kujiandikisha kutoka kwa mratibu ya michuano ya Sprite Bball Kings, Basilisa Biseko wakati wa zoezi la uandikishaji wa timu mbalimbali kwa ajili ya ushiriki wa michuano hiyo.
Uandikishaji ulifanyika Tegeta Complex jijini Dar es Salaam huku timu zaidi ya 20 zikijitokeza kujiandikisha. Michuano ya Sprite Bball Kings inaendeshwa na kituo cha Televisheni na Radio cha East Africa (EATV/Radio) kwa udhamini wakampuni ya Coca-Cola.
******
Ikiwa ni siku ya kwanza kwa timu mbali mbali za michuano ya kikapu ya Bball Kings, zaidi ya timu 20 zimejitokeza kujiandikisha mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa zoezi la uandikishaji linaloendelea jijini Dar es Salaam.
Michuano ya mchezo wa kikapu ya Bball Kings inayoendeshwa na kituo cha Televisheni na Radio cha East Africa (EATV/Radio) kwa kushirikiana na Kampuni ya Coca-Cola kupitia kinywaji chake cha Sprite siku ya jumamosi imeshuhudia wawakilishi wa timu mbalimbali wakijitokeza na kujaza fomu za ushiriki, huku wawakilishi wa timu hizo wakijigamba kujidhatiti kikamilifu kuchukua ubingwa wa mwaka huu.
Kati ya timu zilizojitokeza ni pamoja na Cavarious, Lycans, Tegeta Camp, Lord Baden, K-Warriors, DMI, St Joseph na MJ Junior.
Nyingine ni Oilers, TMT, Mchenga, Bahari Beach, Street Boys, Street Warriors, Chanika Legends, God With Us, Weusi Basketball Club, Junior Basketball Club na Celestial Basketball Team.
Akizungumza wakati wa uandikishaji wa timu shiriki, Mkuu wa Kitengo cha Mauzo na Masoko wa wa EATV, Roy Mbowe alisema mwitikio wa timu mbalimbali umejaa hamasa kubwa na wa kuridhisha, huku kila timu iliyojitokeza ikiwa na wachezaji wasiozidi 10.
“Mashindano hayo yanahusu vijana wenye umri wa kuanzia miaka 16 na watapaswa kuunda timu ya wachezaji 10 ambao watachuana na timu nyingine zitakazokuwa zimejiandikisha, huku tukitoa fursa katika wachezaji hao 10, timu inaweza kuwa na wachezaji wasiozidi watatu kutoka katika timu kubwa za Ligi Darasa la Kwanza za za kikapu za hapa nchini,’’alisema Mbowe.
Michuano ya Sprite Bball Kings itaendeshwa kwa njia ya mtoano katika hatua ya kwanza ili kupata timu 16 zitakazoingia hatua ya pili na kutaja zawadi kwa timu itakayotwaa ubingwa itakuwa ni Sh.milioni 10 wakati mshindi wa pili atapata Sh.milioni tatu huku pia kukiwa na zawadi ya Sh milioni mbili kwa mchezaji bora (MVP).
Mashindano hayo yatakayoshirikisha wachezaji kutoka mikoa yote nchini, yanatarajiwa kuanza mwezi huu na kumalizika Julai mwanzoni.
Social Plugin