Wanawake wawili wilayani Igunga mkoani Tabora wameuawa kikatili kwa kukatwa na mapanga na watu wasiojulikana huku mmoja akikatwa kiganja cha mkono wa kulia.
Mtendaji wa Kata ya Tambalale, Salumu Kitindi alimtaja aliyeuawa kuwa ni Elizabeth Charles (45), mkulima wa kijiji cha Tambalale, kata hiyo ya Tambalale, Tarafa ya Nsimbo.
Kitindi alisema watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwa mama huyo ambaye kwa sasa ni marehemu usiku kisha kuingia ndani na kumshambulia kwa mapanga hadi kupoteza uhai wake ambapo baada ya kufanya mauaji hayo walikata kiganja cha mkono wa kulia kisha kuondoka nacho kusikojulikana.
Naye Mtendaji wa Kata ya Mwisi, Issa Omary alisema katika kata yake, mwanamke Suzana Alex (24) mkulima mkazi wa Kijiji cha Busomeke, Tarafa ya Simbo ameuawa kwa mapanga kwa kukatwa sehemu mbalimbali za mwili wake huku mumewe, John Matheo (27) akijeruhiwa vibaya ambapo amelazwa Hospitali Misheni ya Ndala iliyoko Nzega.
Aidha, Omary alibainisha kuwa watu hao walifika katika mji huo saa saba usiku ambako walivunja mlango na kuingia ndani kisha kuanza kuwakata kwa mapanga wanandoa hao na kusababisha Suzana kuuawa papohapo kisha kuondoka bila ya kubeba kitu chochote.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo, John Mwaipopo alithibitisha kuuawa kwa akinamama hao na kueleza kuwa Jeshi la Polisi Igunga linaendelea na msako wa kuwabaini waliohusika na mauaji hayo huku akitoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na mauaji kuacha mara moja.
Social Plugin