WAKATI Mkurugenzi wa Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Lucky Vincent ya jijini Arusha, Innocent Mushi na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Longino Nkana wakipandishwa kizimbani kutokana na vifo vya watu 35 wakiwemo wanafunzi 32 wa shule hiyo, ndege maalumu inatarajiwa kutua nchini leo kuwabeba majeruhi watatu wakatibiwe Marekani.
Mwinjilisti maarufu duniani kutoka Shirika la Samaritan Purse, Bill Graham wa Marekani na ndiye aliyebeba gharama za kukodisha ndege maalumu aina ya DC 8 kupeleka wanafunzi waliojeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani Karatu, Arusha.
Watoto hao wameumia shingo, miguu na sehemu mbalimbali za miili yao. Kwa mujibu wa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyarandu aliyezungumza jana na waandishi wa habari mjini Arusha, gharama za kukodisha ndege kwenda Marekani si chini ya dola za Kimarekani 350,000 (Sh milioni 700). Gharama hizo ni nje ya matibabu, chakula na malazi kwa wakati wote ambao wagonjwa hao na wasindikizaji watakuwa nchini humo.
“Tumefanikiwa kupata ndege aina ya DC 8 kutoka Shirika la Samaritan Purse linaloongozwa na mtoto wa Billy Graham aitwaye Franklin kwa ajili ya kuwasafirisha watoto Doreen Mshana, Sadia Awadh na Wilson Tarimo na wazazi wao watatu, yaani mama zao,” alisema Nyalandu akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Alisema pia watoto hao wataambatana na daktari wa hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Elias Mashalla na muuguzi Simphorosa Silalye. Kwa mujibu wa Nyalandu, ndege hiyo inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro KIA) leo jioni ikitokea Charlotte ,Jimbo la North Carolina, Marekani.
“Endapo taratibu za safari ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa visa utafanikiwa, basi ndege inaondoka na wagfonjwa na wasindikizaji Jumapili (kesho) na baada ya kufika mjini Charlotte, North Carolina watasafiri kwa ndege nyingine maalumu ya kubeba wagonjwa hadi mji wa Sioux City, Iowa ambako watapokelewa na uongozi wa Hospitali ya Mercu na Shirika la STEMM,” alisema Nyalandu.
Alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kupongeza juhudi za Rais, Dk John Magufuli, Makamu wake, Samia Suluhu Hassan na uongozi wa Mkoa wa Arusha chini ya Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo kwa kuguswa na kushiriki katika kila hatua kuanzia baada ya ajali, mazishi hadi ufuatiliaji wa afya za majeruhi.
‘’Hili jambo ni letu sote hapa, hatuhitaji sifa bali tunachopaswa Watanzania wote kushirikiana kwa pamoja na kuweka mbele ubinadamu na kujitoa kwa hali na mali kuwasaidia hawa watoto ili waweze kupata nafuu na kurudi shuleni,” alisema Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gambo alisema kuwa katika michango yote iliyochangwa kwa ajili ya rambirambi kwa msiba huo mpaka jana zilipatikana fedha kiasi cha Sh milioni 215.
Gambo alisema katika fedha hizo, kila familia ilikabidhiwa zaidi ya Sh milioni 3.8 na pia Serikali ilibeba gharama za usafiri, majeneza, mafuta ya magari na malipo ya madereva. Alisema Sh milioni 190 zilitumika katika matumizi mbalimbali ya msiba huo na kuwataka walioahidi kuchangia kutimiza ahadi zao.
Kizimbani Wakati majeruhi ambao ni wanafunzi wa shule hiyo wakitarajiwa kupelekwa Marekani, mmiliki wa shule hiyo na mwalimu mkuu msaidizi walipandishwa kizimbani kwa makosa kadhaa ya usalama barabarani, ikiwa ni pamoja na kusafirisha watoto bila ya kuwa na vibali.
Wakisomewa mashitaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Hakimu Mkazi Arusha, Desdery Kamugisha, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Rose Sule alidai watuhumiwa hao wawili wamefunguliwa kesi Namba 78/2017 huku Mkurugenzi wa shule hiyo akishitakiwa kwa makosa manne na Mwalimu Nkana akishitakiwa kwa kosa moja.
Akimsomea Mkurugenzi wa Lucky Vincent makosa yake, wakili huyo alidai kosa la kwanza ni la kuendesha gari la abiria bila ya kuwa na leseni ya usafirishaji ambapo Mei 6 mwaka huu katika eneo la Kwamrombo, Arusha Mjini akiwa mmiliki wa gari namba T 871 BYS aina ya Toyota Rosa, alifanya shughuli ya usafirishaji bila ya kuwa na leseni ya abiria.
Kosa la pili ni kuruhusu kuendesha gari bila ya kuwa na bima (Road Licence), Mei 6 mwaka huu akiwa mmiliki wa gari hilo aliruhusu gari hilo kuendeshwa bila ya kuwa na bima. Kosa la tatu ni kushindwa kuingia mkataba na mwajiriwa wake, Dismas Gasper ambapo Mei 6, 2017 akiwa mmiliki wa gari alishindwa kuingia mkataba na dereva huyo aliyeendesha gari lililopata ajali ambaye naye alifariki dunia katika tukio hilo.
Kosa la nne ni kubeba abiria zaidi ya 13 ambapo Mei 6 mwaka huu, mkurugenzi huyo ambaye ni Ofisa Msafirishaji na mmiliki wa shule ya Lucky Vincent alibeba na kusafirisha abiria zaidi ya 13 katika gari hilo kitendo ambacho ni kinyume na sheria.
Kosa la tano ni la Mwalimu Mkuu Msaidizi ambapo anashitakiwa kwa kuandaa safari iliyozidi abiria 13 ambapo ni kinyume cha sheria inadaiwa kuwa Mei 6 mwaka huu, Nkana akiwa Mwalimu Mkuu Msaidizi na mwandaaji wa safari alipakia abiria zaidi ya 13 kwenye gari lililosababisha vifo vya wanafunzi hao.
Baada ya washitakiwa hao kusomewa mashitaka yao yanayowakabili wakili anayewatetea washitakiwa hao, Method Komomogolo aliomba dhamana kwa washitakiwa hao huku Wakili wa Serikali Sule akisema hana pingamizi na dhamana yao.
Hakimu Kamugisha alitoa masharti ya dhamana kwa washitakiwa hao ambayo ni kila mshitakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni 15 na kwamba hawatakiwi kuondoka nchini au ndani ya mkoa bila ruhusa ya mahakama pamoja na kuwasilisha hati zao za kusafiria.
Watuhumiwa hao walitimiza masharti ya dhamana yao na kesi yao kuahirishwa hadi Juni 8, mwaka huu.
Chanzo-Habarileo
Social Plugin