Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini wametakiwa kuzingatia mipaka ya madaraka yao na kuhakikisha hatua wanazochukua katika utendaji wao zinafuata Sheria ,Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana Mei 9, 2017 wakati akifungua mafunzo kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma.
Majaliwa alisema kuwa viongozi hao wanatakiwa kusimamia kikamilifu nidhamu katika Utumishi wa Umma kwa sababu wenyewe ni kioo katika kuishi kwa kuzingatia miiko ya Utumishi wa Umma.
Aidha, viongozi hao wametakiwa kutoa kipaumbelea katika kufuatilia na kusimamia kwa makini sekta za afya, kilimo, elimu na maji kwa kuwa ndizo zinazogusa zaidi maisha ya wananchi.
Pia, Majaliwa aliwaelekeza wasimamie na kuziba mianya yote ya upotevu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya na kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji pamoja na kusimamia usafi na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao.
Naye Naibu Waziri Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI, Suleiman Jafo alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha viongozi hao wanapata mafanikio makubwa katika utendaji wao wa kazi ili Serikali iweze kupata tija.
Social Plugin