Rais Atengue Kauli Yake Kuhusu Watoto wa Kike Wanaopata Mimba Mashuleni Maana ni Kinyume na Katiba, Sheria, Busara na hata Ilani ya Chama Chake.
Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo imeshtushwa na kusikitishwa sana na tamko la kupiga marufuku wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa shuleni kupata fursa ya kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua lililotolewa na Rais Magufuli Juni 22, 2017 katika hotuba yake kwa wananchi wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Ngome ya Wanawake ya ACT Wazalendo inaiona marufuku hiyo kama hatua kali inayomkandamiza na kumbagua mtoto wa kike kwa kumnyima haki yake ya msingi ya kupata elimu, na kwahivyo inapinga amri hiyo ya marufuku. Marufuku hii ni kinyume cha matakwa ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 11(2) inayosema:
"Kila mtu anayo haki ya kujielimisha, na kila raia atakuwa huru kutafuta elimu katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wake".
ACT Wazalendo inaamini kuwa licha ya kuzuia haki ya kikatiba ya kujielimisha kwa mtoto wa kike lakini pia Rais ametumia mamlaka yake kumbagua mtoto wa kike katika haki zake za msingi kinyume na Ibara ya 13(4) ya katiba inayosema kuwa "Ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa kazi au shughuli yoyote ya Mamlaka ya Nchi".
Marufuku hii ni ubaguzi wa wa wazi dhidi ya watoto, na ni kinyume na Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 (The Law of Child ACT, 2009) ibara 5 (1) inayosisitiza kuwa "Mtoto ana haki ya kuishi huru bila kubaguliwa".
ACT Wazalendo inamtaka Rais atambue kuwa Tanzania imeridhia na kusaini maazimio mbalimbali ya kimataifa kuhusu haki za mtoto wa kike kama vile Azimio la Dunia la Haki za Binadamu la mwaka 1948 (Universal Declaration on Human Rights (1948) ibara ya 26(1), Tamko la Kimataifa la kupinga aina zote za ukandamizaji dhidi ya Wanawake (Convention of the Elimination of all forms of Discrimination Against Women - CEDAW) la mwaka 1979 ambayo yote yameweka msisitizo wa kulinda haki za mtoto wa kike.
Rais alifanya kampeni mwaka 2015 Kwa kutumia ilani ya uchaguzi ya chama chake cha CCM. Ilani hiyo iliahidi kuwa CCM ikifanikiwa kuunda Serikali itaruhusu mtoto wa kike anayepata mimba kurudi shuleni baada ya kujifungua. Kauli ya Mwenyekiti wa CCM na Rais inaonyesha kuwa CCM iliwalaghai wananchi ili kupata kura.
ACT Wazalendo inatambua uwepo wa changamoto mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kimazingira anazokabiliana nazo mtoto wa kike na zinachangia kwa kiasi kikubwa kumuingiza bila kutarajia katika matatizo ya kupata ujauzito akiwa shuleni.
Watoto wengi wa kike hasa waishio maeneo ya vijijini na watokanao na familia masikini ndio wamekuwa wahanga wakubwa wa matatizo ya kupata ujauzito wakiwa shuleni kutokana na miundombinu isiyo rafiki ya elimu kama vile ukosefu wa mabweni, kusafiri mwendo mrefu kwenda na kurudi shuleni, kusaidia shughuli za nyumbani na shughuli za kuziingizia kipato familia zao ambapo kote huko hukabiliana na changamoto kadha wa kadha zinazoweza kuwasababishia ujauzito.
Sisi tunaamini ni wajibu wa Serikali iliyopo madarakani, jamii pamoja na familia kuhakikisha kuwa wanatengeneza mazingira rafiki na salama kwa mtoto wa kike ili nae aweze kupata haki yake ya msingi ya elimu kama ilivyo kwa watoto wengine na sio kumbagua, kumkandamiza na kumnyima haki yake ya elimu. Zanzibar ni mfano hai kwenye hili kwa kuwalinda wasichana wasipate ujauzito na kuwapa fursa ya kurudi shule hata pale kwa bahati mbaya wanapopata ujauzito. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iige jambo hili jema.
ACT Wazalendo tunamtaka Rais Magufuli kutathmini upya msimamo wake na kuzingatia mazingira, hali halisi, sera, sheria na maazimio mbalimbali ambayo nchi imeyaridhia na kusaini kuhusu kulinda na kuhifadhi haki za mtoto wa kike. Pia anapaswa kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoto wa kike badala ya kuwaongezea matatizo zaidi. Hivyo ni muhimu atengue kauli yake hii.
Dhana ya elimu kwa ujumla sio zawadi kwa watiifu na wale wanaoonekana na nidhamu (hapa tukirejea sera ya elimu ya 2014) ambayo imeelezea vema juu ya dhima na dira ya elimu). Kupata elimu ni haki ya kila mtoto.
Esther Kyamba,
Katibu, Ngome ya Wanawake,
ACT Wazalendo
Juni 24, 2017
Tanzania
Social Plugin