Ofisa Programu wa TGNP Mtandao, Anna Sangai (kushoto), akitoa mada katika kongamano la siku moja lililohusu elimu ya afya ya uzazi lililofanyika Makao Makuu ya TGNP Mabibo Dar es Salaam jana. Kongamano hilo liliandaliwa na TGNP.
Mwanafunzi Leila Kisinga kutoka Sekondari ya Mabibo akitoa mada kuhusu via vya uzazi vya mwanamke vinavyofanya kazi.
Kongamano likiendelea.
Mshiriki Idd Hamisi akichangia jambo katika kongamano hilo.
Usikivu katika kongamano hilo.
Aisha Kijavara akichangia.
Akina mama wakiwa katika kongamano hilo. Wakina mama hao walitoa uzoefu wao kuhusu afya ya uzazi kwa watoto.
Mwanafunzi Juma Nasoro kutoka Sekondari ya Mabibo akitoa mada kuhusu via vya uzazi vya mwanaume vinavyofanya kazi.
Mdau Selemani Bishagazi akichangia kuhusu wanaume kuwasaidia watoto wao wa kike wanapokuwa katika hedhi.
Mary Mbarawa akichangia jambo.
Na Dotto Mwaibale
WAKINA Baba nchini wametakiwa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa watoto wao badala ya kuwaachia kazi hiyo ifanywe na wakina mama pekee.
Mwito huo umetolewa na Selemani Bishagazi wakati akichangia mada katika kongamano la siku moja lililohusu elimu ya afya ya uzazi kwa watoto hasa wa kike lililoandaliwa na TGNP Mtandao jijini Dar es Salaam jana.
"Suala la utoaji wa elimu ya afya ya uzazi kwa watoto wetu hasa wa kike ni letu sote kati ya baba na mama kwani baba ndie chanzo kikubwa cha mapato katika familia" alisema Bishagazi.
Bishagazi alisema suala la kutoa fedha za kunulia pedi wakati mtoto wa kike anapokuwa kwenye hedhi si la mama bali hata baba anawajibu wa kutoa fedha hizo na akaomba dhana hiyo potofu kuwa mama ndiye anawajibika katika suala hilo iachwe.
Alisema ni vizuri mtoto wa kike anapokuwa katika hedhi kuwajulisha wazazi wake ili aweze kusaidiwa kupata fedha za kununulia pedi badala ya kukaa kimya kwa hofu na kujikuta akishindwa kujistiri na kuchafuka.
Mshiriki mwingine katika kongamano hilo alisema usiri imekuwa ni changamoto kubwa katika kumsaidia mtoto kujua afya za uzazi kwani wazazi wengi wanashindwa kuwaweka wazi watoto wao kuhusu jambo hilo.
Alisema mtoto wa kike anapobalee na kuanza kuingia katika hedhi wazazi wanapaswa kumueleza kuwa amekuwa na hivyo iwapo atakutana na mwanaume atapata mimba hivyo kumpa elimu hiyo kwa wazi ataweza kujiepusha na kupata mimba badala ya kufanya siri.
Aisha Kijavara ambaye alishiriki katika kongamano hilo alisema ni vizuri elimu ya afya ya uzazi ikatolewa kwa uwazi na kutaja viungo vya uzazi bila ya kuona aibu ili watoto waweze kuelewa vizuri badala ya kufichaficha.
"Katika suala ili la utoaji wa elimu hii ya afya ya uzazi tunapaswa kuwa na muda wa kutosha na kutamka wazi viungo vya uzazi jinsi vinavyofanya kazi ili walengwa waweze kuelewa vizuri somo" alisema Kijavara.
Ofisa Programu wa TGNP Mtandao, Anna Sangai alisema wanapopigania bajeti zinazopitishwa na bunge ziwe na mlengo wa kutoa kipaumbele kijinsia zinamlenga zaidi mtoto wa kike ambao wanachangamoto nyingi hasa wale waliopo mashuleni kwani wengi wao hawana uwezo wa kununua pedi wanapokuwa katika hedhi.
Alisema baadhi yao wamejikuta wakiingia katika vishawishi vya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume ambao wamekuwa wakiwasaidia kuwanunulia bedi.
"Tumekuwa tukihimiza kutengwa kwa bajeti kubwa za wizara husika ili kuwasaidia watoto hawa ambao wapo katika changamoto hiyo" alisema Sangai.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Mabibo ambao baadhi yao walitoa mada kuhusu afya ya uzazi na matumizi ya via vya uzazi.
Social Plugin