Mkurugenzi wa Kampuni ya Travel House Global, Sojan Varghese amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kupandishwa kizimbani akikabiliwa na mashtaka ya kujipatia Sh 193 milioni alizopewa kwa ajili ya mahujaji zaidi ya 119 wa Chama cha Karismatiki Katoliki Tanzania.
Varghese alidaiwa kuchukua fedha hizo kutoka kwa John Ngotty kwa lengo la kukata tiketi za ndege kwa mahujaji hao waliokuwa wakitaka kusafiri kuelekea nchi za Roma, Italia na Israeli kwa ajili ya hija.
Wakili wa Serikali, Adolf Mkini akimsomea hati ya mashtaka jana Ijumaa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alidai kuwa Desemba 23, 2016 katika maeneo ya ofisi za kampuni hiyo zilizopo Mtaa wa Jamhuri, Vargherse alijipatia fedha kutoka kwa Ngotty, fedha ambazo ni kwa ajili ya nauli ya kupata tiketi ya ndege kwa Wakarismatiki 119 kutoka Dar es Salaam kwenda Roma na Israeli.
Mkini alidai kuwa Desemba 23, 2016 mshtakiwa huyo alijipatia kiasi kingine cha fedha kupitia hundi namba 000005 kutoka kwa Ngotty kwa ajili ya kuwakatia tiketi ya ndege mahujaji hao kwenda nchi hizo.
Alidai kuwa Januari 11, 2017 katika maeneo ya ofisi hizo, Varghese alijipatia Dola za Marekani 9,500 kutoka kwa Ngotty ili zitumike kununulia tiketi za ndege kwa wanachama wa Wakarismatiki 119 kwenda hija nchi za Roma na Israeli.
“Januari 11, 2017, alijipatia kiasi kingine cha fedha kwa hundi namba 000008 kutoka kwa Ngotty,” alisema.
Imedaiwa kuwa Januari 31, 2017, Varghese alijipatia fedha kutoka kwa Ngotty kwa ajili ya nauli ya tiketi ya ndege kwa wanachama 199 wa Karismatiki.
Mkini alidai, Aprili 12, 2017, maeneo ya ofisi za kampuni yake, alijipatia fedha kutoka kwa Ngotty kwa ajili ya kununulia tiketi kwa wanachama 119 wa Karismatiki waliokuwa wanakwenda hija nchi za Roma na Israeli.
Baada ya mshtakiwa huyo kusomewa mashtaka hayo, alikana na upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi haujakamilika na kwamba hawana pingamizi la dhamana.
Hakimu Mashauri alimtaka mshtakiwa huyo kuwasilisha fedha taslimu Sh 100 milioni ama hati ya mali yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha pamoja na hayo pia awe na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria.
Pia alimtaka mshtakiwa huyo kuwasilisha hati yake ya kusafiria na haruhusiwi kutoka nje ya Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama.
Kesi imeahirishwa hadi Julai 6, 2017. Mshtakiwa amepelekwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana.