MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro ametangaza vita kwa wananchi wanaojichukulia sheria mkononi, bodaboda wanaokiuka sheria za barabarani na kujihusisha na vitendo vya uhalifu, wanaojihusisha na dawa za kulevya na wala rushwa, huku akiahidi Polisi watajibu ubaya kwa ubaya kwa wahusika wa mauaji ya raia mkoani Pwani.
IGP Sirro aliyasema hayo Dar es Salaamjana, ikiwa ni mara yake ya kwanza kuzungumza na waandishi wa habari tangu alipoteuliwa na kuapishwa kushika wadhifa huo Jumatatu wiki hii, akichukua nafasi ya IGP Ernest Mangu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais John Magufuli, Mei 28, mwaka huu.
Amewahakikishia wananchi kuwa yeye pamoja na walioko chini yake watashirikiana kwa pamoja kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa kwa kulinda raia na mali zao. Amshukuru Rais Magufuli “Kwa kuwa ni mara ya kwanza kuzungumza nanyi nikiwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, nianze kwa kumshukuru Rais John Magufuli kwa kuniamini na kuniteua kushika nafasi hii muhimu katika kuwatumikia Watanzania… kwa ujumla hali ya usalama hapa nchini ni shwari, japokuwa kuna matatizo machache yamekuwa yakijitokeza na tunaendelea kukabiliana nayo,” alisema IGP Sirro, ambaye kabla ya uteuzi wake alikuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Alisema pamoja na nchi kuwa shwari, lakini bado yapo matukio ambayo yanahitaji nguvu ya pamoja ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kuyashughulikia ili kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kuishi katika hali ya amani na utulivu.
Mauaji ya wananchi Pwani
Akizungumzia mauaji ya wananchi mkoani Pwani, IGP Sirro alisema wameshuhudia mauaji ya wananchi na askari katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji ambayo yamekuwa yakifanywa na wahalifu wachache kwa malengo wanayoyajua wao.
“Ukiangalia mikoa yote hatuna matukio makubwa sana ya kutisha, changamoto tuliyonayo kubwa ni tatizo la Mkoa wa Pwani ambalo mmesikia baadhi ya raia wema wameuawa bila sababu, kuna kikundi cha watu wachache ambao wanafikiri wanaweza kufanya ule mkoa usiwe na amani,” alieleza.
“Siku zote haki lazima itatoa majibu na niwahakikishie Watanzania kwamba suala la Ikwiriri, Rufiji ni suala la muda mfupi viongozi wangu wamezungumza na mimi sitaki kulizungumzia tena. Ninachosema ni kwamba Watanzania wanataka kupata majibu, lakini mimi na timu yangu pamoja navyombo vingine vya dola lazima tupate hayo majibu.
Ubaya kwa ubaya tu
“Mimi nawapa tu salamu kile kikundi cha watu wachache, watu hawa ni Watanzania hawana sababu ya kuwafanyia Watanzania wenzao ubaya, lakini siku zote wanasema mwenzako akikufanyia ubaya huna sababu ya kufanya ubaya, lakini waandishi wa habari kwa hao wanaofanya ubaya tupeleke tu salamu kwamba ubaya huu tutajibu kwa ubaya kwa mujibu wa sheria,” aliahidi kachero huyo wa Polisi.
Aliongeza: “Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linaendelea na operesheni mbalimbali za kuhakikisha kwamba vitendo hivyo haviendelei, ikiwa ni pamoja na kuwatafuta wote wanaojihusisha na mauaji hayo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao japokuwa baadhi yao wameshakamatwa.”
Alisema ili kufanikiwa zaidi katika operesheni hizo, amewaomba wananchi wa wilaya hizo kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahalifu hao na yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa wahalifu hao atazawadiwa Sh milioni 10.
“Sisi tupo vizuri na tumejipanga vizuri hawa watu hawajatuzidi nguvu na hawatatuzidi nguvu lengo letu ni kuhakikisha watanzania wanaishi kwa amani na utulivu… sisi ni wengi hawa ni wachache tunaweza na majibu ya Ikwiriri, Kibiti, Rufiji hayatachukua muda mrefu wale waliofanya kazi na mimi nafkiri tunafahamiana zaidi maneno yawe machache vitendo viwe vingi,” alieleza.
Alisema: “Wanamkuranga, Wana Ikwiriri wasubiri majibu na haya majibu watayapata kwa ushirikiano, ingawa nimeona kwamba wananchi wanalalamika kuna nguvu imetumika zaidi… hapo ndipo nataka tushirikiane kwa sababu tusipokuwa pamoja na kuaminiana kazi itakuwa ni ngumu ili tukiwa pamoja kazi itakuwa rahisi. Ni suala la muda, sitasema sana ila nitasema tukishapata majibu.”
Matukio ya kujichukulia sheria mkononi
IGP Sirro alisema tatizo la wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga, kuwachoma moto, kuwaua na kuwadhalilisha kwa kuwavua nguo baadhi ya wananchi wanaoshukiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu na mbaya zaidi baadhi ya watu wamefikia hatua ya kushabikia na kuhamasisha tabia hizo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi.
“Takwimu zetu zinaonesha kwamba tabia hii inazidi kukua ambapo matukio 245 yameripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Machi 2017 ukilinganisha na matukio 222 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2016… Mauaji ya hasira kali ni mengi ikilinganishwa na mauaji ya silaha,” alisema IGP Sirro.
Aliongeza: “Hawa watu wanaojiita wenye hasira kali unakuta mtu ameiba kuku wananchi wanaitana na kumuua, hili halikubaliki. Kila mtu atahukumiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu, hivyo wenye hasira kali nitoe onyo kwamba hiyo hasira kali yako itakufanya uondoke uache familia yako.”
Kutokana na hali hiyo, alitoa onyo kali kwa wote wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi kuacha mara moja na badala yake wananchi wajenge tabia ya kuheshimu na kufuata sheria za nchi, kwani kwa kufanya hivyo watasaidia vyombo vyenye mamlaka ya utoaji haki kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Bodaboda sasa kukiona
Akizungumzia bodaboda kutokutii sheria za usalama barabarani pamoja na kujihusisha na vitendo vya kihalifu, alisema waendesha bodaboda wamekuwa na tabia ya kukaidi ikiwemo kubeba abiria zaidi ya mmoja, kupita katika taa nyekundu pamoja na kutovaa kofia ngumu, tabia ambayo husababisha kuwaweka katika mazingira hatarishi na wakati mwingine kusababisha vifo, majeruhi na ulemavu wa kudumu.
“Mbali na kusababisha ajali, pia wapo madereva bodaboda ambao wanajihusisha na matukio ya uporaji na ujambazi huku wakitumia mwavuli wa biashara ya kusafirisha abiria. Ieleweke wazi kuwa suala la kufuata sheria za usalama barabarani kwa bodaboda halina mjadala…Huu ni wakati wa kufuata sheria bila shuruti,” alieleza.
Alisema amewaagiza makamanda wote wa mikoa kuwashughulikia wale wote wasiofuata sheria za usalama barabarani ama kujihusisha na vitendo vya kihalifu kwa kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Vitendo vya rushwa
Aidha, alisema kumekuwa na malalamiko dhidi ya baadhi ya askari polisi kujihusisha na vitendo vya rushwa katika utoaji huduma za kipolisi, lakini pia baadhi ya wananchi kuwashawishi askari kupokea rushwa kama ngao ya kukwepa kuwajibishwa pindi wanapokuwa wamefanya makosa na kuwataka wote kuacha tabia hiyo.
“Niwatake wananchi kuacha tabia ya kushawishi na kutoa rushwa katika mazingira yoyote na badala yake wazingatie sheria, kanuni na taratibu za nchi katika kupata huduma wanazostahili… Ndani ya Jeshi la Polisi tayari upo utaratibu wa kumuadhibu askari anayepokea rushwa lakini pia kumzawadia askari wanaokataa rushwa kiwango sawa cha thamani ya rushwa waliyokataa,” alifafanua.
Alitoa rai kwa wananchi kutambua kwamba jukumu la ulinzi na usalama kikatiba ni la kila mwananchi na si suala la Jeshi la Polisi peke yake na kusema kwamba kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha kuwa anashirikia kikamilifu katika kuimarisha amani na usalama ndani ya nchi yake.
Aidha, aliwashukuru wananchi wanaoendelea kupata taarifa ambazo zimefanikisha kukamatwa kwa wahalifu na kuwaomba kuendelea kutoa taarifa za kihalifu kila wanapoona viashiria vya uhalifu ili kwa pamoja waweze kuiweka nchi salama.
Dawa za kulevya
Akizungumzia dawa za kulevya, alisema vita inakwenda vizuri na wataendelea kuisimamia na kuwataka wale ambao kipato chao kilikuwa ni dawa za kulevya kuachana na hiyo biashara, kwa kuwa mwisho itawafanya kuacha familia zao.
Hata hivyo, alipoulizwa kwamba atakuja na safu yake, alisema atafanya kazi na watendaji waliopo na makamanda waliopo na askari hao hao na kusema kwamba endapo bajeti itaruhusu watafurahi kuongezewa askari.
Mauaji ya askari Polisi
Akijibu maswali kuhusu mauaji ya askari polisi, alisema mauaji hayo ni ajali kazini kwa kuwa unapopambana na uhalifu kuna mawili askaria afe au jambazi afe na ndiyo sababu wameapa na wana wajibu wa kutumia nguvu ya kadri.
“Ndo maana ninashangaa mtu anapotakiwa kukamatwa ana polisi anakataa wakati yeye amepewa wajibu wa kutumia nguvu ya kadri… hivyo inapotokea kifo cha askari ni ajali kazini na hiyo inatupa nguvu ya kupambana zaidi mana hiyo changamoto ya askari kufa inatupa fursa ya kutaka kujua kwanini askari amekufa hivyo tunajipanga zaidi,” alieleza na kuongeza kuwa watazidi kupambana na wahalifu na kuwataka raia wema kutokukimbia, kwa kuwa mtu anayetumia silaha ukamataji wake ni maalumu hivyo raia wema hawana haja ya kuogopa.
Waandishi kupigwa
Akizungumzia matukio ya waandishi kupigwa, alisema wote ni wabia, hivyo wakati mwingine matukio kama hayo hutokea kwa bahati mbaya na siyo sahihi kumpiga mwandishi.
“Kama hujajitambulisha vizuri na ukaingia kwenye maeneo ambayo ni ya mapambano kuna shida ya kutambua kwamba huyu ni mwandishi, lakini tukishajua huyu ni mwandishi hatuwezi kumpiga kwa sababu ni mwandishi labda iwe ni bahati mbaya… ninachosema si sahihi kumpiga mwandishi kwa sababu ni mwandishi na hata kama ni mualifu hatakiwi kupigwa kwa sababu taratibu zinafahamika,” alifafanua.
Kuhusu suala la upelelezi wa kesi kuchukua muda mrefu, alisema linatokana na maeneo ya upelelezi ila wameweka utaratibu wa siku 60 na usipokamilika kuna hatua ambazo wanachukua kwa mujibu wa sheria, lakini hawana nia ya kuchelewesha upelelezi.
IMEANDIKWA NA HELLEN MLACKY - HABARILEO
Social Plugin