JELA MAISHA KWA KUBAKA MTOTO WAKATI WAKILINDA NGEDERE KWENYE SHAMBA LA TUMBAKU




MAHAKAMA ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi imehukumu mkazi wa kijiji cha Kamsisi, Richard Chambanenge (20) kutumikia kifungo cha maisha baada ya kukiri kosa la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka sita akiwa ni binti wa tajiri yake.


Mshitakiwa huyo alikuwa akifanya kazi ya kibarua katika shamba la tumbaku mali ya Joseph Felix ambaye ni baba mzazi wa mtoto huyo wa kike. Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mlele, Teotimus Swai alishangazwa na uamuzi wa kuvunja shitaka kwa kukiri kosa hata baada ya mashahidi wanane walioitwa na upande wa mashtaka mahakamani hapo.

“Pamoja na mshtakiwa kukiri kosa… kwanza namshangaa kwa kuwa alikana kosa alipofikishwa mahakamani hapa kwa mara ya kwanza na upande wa mashitaka waliita mashahidi wanane kutoka ushahidi wao mahakamani hapa, na leo hii mshtakiwa amevunja shtaka kwa kukiri kosa lake,” alisema Swai.

Akaongeza, “Pamoja na uamuzi wake huo, hakuna mbadala wa adhabu isipokuwa utatumikia kifungo cha maisha jela.”

 Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi, Bakari Hongoli alidai mahakamani hapo kuwa, mshtakiwa alitenda kosa hilo, Januari 20, mwaka jana saa tisa mchana ambapo alivizia na kumbaka msichana huyo wakati wakilinda ngedere katika shamba la tumbaku ambalo ni mali ya baba yake mzazi.

IMEANDIKWA NA PETY SIYAME-HABARILEO MLELE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم