Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limetoa tahadhari kwa watumiaji wote wa barabara nchini kuzingatia sheria ili kuepuka ajali hususani wakati wa sikukuu ya Eid el Fitri.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana juni 25, 2017, Kaimu Kamanda Kikosi cha Usalama Barabarani, (SACP) Fortunatus Musilimu alisema kuwa katika kipindi cha sikukuu madereva wamekuwa wakiendesha magari kwa mwendo kasi, kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari na kubeba abiria kupita kiasi hali inayoweza kusababisha ajali.
“Tutafanya operesheni kali barabarani, kuwapima madereva kiwango cha ulevi na watakaobainika wamelewa watakamatwa na kuwekwa mahabusu na kufikishwa mahakamani, nasisitiza kwamba,dereva anayetaka kuendesha gari asinywe pombe,akitaka kunywa pombe asiendeshe gari” alisisitiza Kamishna Musilimu katika taarifa hiyo.
Wamiliki wa magari wametahadharishwa yatakayokodishwa kwenda maeneo ya Fukwe bila kibali yatakamatwa na wahusika kufikishwa mahakamani.
Kamishna Musilimu pia alitoa wito kwa wazazi kuangalia usalama wa watoto wao na wasiwaache wakatembea peke yao barabarani bila uangalizi ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
Akizungumzia upande wa madereva wa Pikipiki (Bodaboda) alieleza kuwa wamekuwa wakipita taa nyekundu, wakiendesha pikipiki zao bila kuvaa kofia ngumu, kubeba abiria zaidi ya mmoja (mishikaki) na abiria hao kutovaa kofia ngumu hivyo kuhatarisha Usalama wao hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kamishna Musilimu alisema, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limekuwa likihamasisha na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na matumizi sahihi ya barabara ili kuepuka ajali katika kipindi chote na hasa wakati huu wa sikukuu.
Social Plugin