Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JINSI KIGOGO WA CHADEMA ALIVYOFARIKI AKISAINI HUNDI YA RAMBIRAMBI WAATHIRIKA AJALI YA ARUSHA


KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema kabla ya aliyekuwa Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (83) kufariki dunia jana, alikuwa katika harakati za kusaini hundi kwa ajili kutoa rambirambi kwa waathirika wa ajali iliyoua wanafunzi wa Shule ya Lucky Vincent ya jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni Dodoma jana, Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alisema kifo cha muasisi huyo ni cha ghafla kwani hata siku ya jana, aliamka salama na kuendelea na shughuli zake.

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro, alisema hata kwenye vikao vya Baraza Kuu la Chadema vilivyofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki, Ndesamburo alihudhuria akiwa na nguvu zake bila kuonesha dalili yoyote ya ugonjwa.

“Baada ya kumaliza vikao vya Baraza, alirudi Moshi na jana (juzi) alimpigia simu Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro ili afike nyumbani kwake Moshi kwa ajili ya kumpatia rambirambi kwa ajili ya watoto walopata ajali na kupoteza maisha wa Shule ya Lucky Vincent,” alifafanua Mbowe.

Alisema Ndesamburo alimtaka meya huyo wakutane jana asubuhi na wakati wa mazungumzo, alitaka kujua waathirika wa ajali hiyo walikuwa wangapi na alipotaarifiwa kuwa wapo 35, aliahidi kutoa Sh 100,000 ambayo ni sawa na Sh milioni 3.5 kwa kila familia ya waathirika hao.

“Baada ya makubaliano hayo, wakati mzee wetu anaanza kusaini kitabu chake cha hundi kwa lengo la kumkabidhi meya mchango huo kalamu aliyoishikilia ikaanguka na akaanza kuishiwa nguvu, hata pale meya alipohoji kuhusu afya yake pamoja na kujibu kuwa anaendelea vizuri alionesha wazi kuwa nguvu zinamuishia,” alieleza Mbowe.

Alisema baada ya hali hiyo, meya pamoja na familia Ndesamburo wakaamua kumkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako wakati anatibiwa kwa kuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua alifariki dunia saa 4.45 asubuhi.

Mbowe alisema wabunge wote wa Chadema wamepokea taarifa za msiba huo kwa masikitiko na wanauchukuliwa kuwa ni msiba mzito ikizingatiwa kuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya ni mtoto wa marehemu.

Aliongeza kuwa kwa sasa taratibu nyingine za msiba huo zinaendelea. Wakati akiahirisha shughuli za Bunge kwa kipindi cha asubuhi, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko kifo cha Mzee Ndesamburo ambaye alikuwa mbunge mwenzao katika Bunge la 10. Aliwatangazia wabunge kuhusu kifo hicho na kufafanua kuwa alipatiwa taarifa za msiba huo na Mbowe.

Hata hivyo, alisema baada ya kupata taarifa ya kifo hicho alimruka Lucy Owenya ambaye alikuwa kwenye orodha ya wabunge wa kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango ili kutoa nafasi kwa wabunge wenzake wa Chadema kumtoa nje ya ukumbi.

“Lakini kama mlivyoona alilalamika kuwa kwanini nimemruka ikabidi tu nimpatie nafasi na alipomaliza ndipo walipomtoa nje,” alieleza Chenge na aliwataka wabunge hao kushirikiana na familia ya marehemu ambaye alihudumu kwenye Bunge la 10 ili kukamilisha taratibu zilizobaki.

Aidha, wakati Bunge hilo limerejea tena kwa awamu ya jioni, wabunge hao walitoa heshima kwa ajili ya kifo hicho kwa kusimama kimya kwa sekunde kadhaa. Mjini Moshi, Katibu wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Basil Lema alikiri kiongozi wake alipoteza maisha wakati akiwa katika mazungumzo na Meya Lazaro aliyefika ofisini kwake kwa ajili ya kupokea fedha hizo na kuziwasilisha kunakohusika.

“Mbunge mstaafu hakuugua, alikuwa ofisini kwake akizungumza na Meya wa Arusha aliyefika mkoani hapa kwa ajili ya kuchukua fedha za rambirambi za Shule ya Lucky Vincent... kabla ya kufanya hivyo alihisi kupoteza nguvu na kuanguka, baadaye tukamkimbiza Hospitali ya KCMC na alifia njiani,” alieleza.

Lema alieleza kuwa Ndesamburo maarufu kwa jina la Ndesa Pesa, alifanya kazi katika serikali ya kikoloni na baadaye Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi mwaka 1974 alipojihusisha na shughuli za kibiashara ndani na nje ya nchi.

Alikuwa mfanyabiashara maarufu. Mwaka 1992 aliingia katika kuhitaji mabadiliko ya kisiasa, na mwaka 2000 hadi 2015 alikuwa Mbunge wa Moshi Mjini na baadaye kustaafu nafasi hiyo. Hadi anafariki dunia alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Mbowe kufuatia kifo cha Ndesamburo. Ndugai alisema, “Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Ndesamburo ambaye pia ni baba wa Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya, hakika ni pigo kubwa.

Pia natoa pole kwa ndugu jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu. Namuomba Mungu awape nguvu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.” Aidha, Spika huyo alisema marehemu atakumbukwa kwa uchapakazi wake wakati akiwa mbunge hasa katika kutetea wananchi wa jimboni kwake.

Kwa upande wake, Rais John Magufuli, alisema, “Kwa masikitiko nimepokea taarifa za kifo cha Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Moshi Mjini, Mzee wangu Philemon Ndesamburo kilichotokea leo tarehe 31 Mei, 2017 katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Namkumbuka Mzee Ndesamburo kwa hekima zake na uongozi wake uliozingatia siasa za kistaarabu.” Alituma salamu za rambirambi kwa familia ya Ndesamburo, viongozi na wanachama wa Chadema pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na kifo hicho.

Rais Magufuli alisema alifanya kazi na Ndesamburo wakati wote wakiwa wabunge na wakati wote walishirikiana, kutaniana na anamkumbuka kwa namna ambavyo alitumia muda wake bungeni kupigania mambo yenye maslahi kwa wananchi wa jimbo lake la Moshi Mjini.

Aliitaka familia ya Ndesamburo na wote waliguswa na msiba huu kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu na amemuombea apumzishwe mahali pema peponi. Imeandikwa na Halima Mlacha (Dodoma) na Nakajumo James (Moshi).
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com