JINSI LOWASSA ALIVYOKOLEZA MOTO MCHANGA WA MADINI

WAZIRI Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, amekoleza moto wa sakata la usafirishaji wa mchanga wa madini (makinikia) nje ya nchi kwa kumpongeza Rais Dk. John Magufuli.



Amesema anampongeza Rais Magufuli kwa kutumia Ilani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliyoinadi katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015 ambapo kuundwa kwa tume hiyo ilikuwa ni moja ya ahadi zake alipokuwa akinadi sera zake kugombea urais.

Kauli hiyo ya Lowassa imekuja siku moja baada ya Rais Magufuli kupokea ripoti ya pili ya usafirishaji makinikia nje ya nchi iliyoongozwa na Profesa Nehemia Osoro.
Pamoja na mambo mengine, Lowassa alisema iwapo Rais Magufuli atatekeleza mapendekezo ya kamati hiyo ya kuwachukulia hatua wote waliohusika na mikataba hiyo, basi hatua hiyo itawahusu marais waliokuwapo wakati huo.
“Ni wazi kabisa hawa mawaziri na wasaidizi wengine waliyafanya haya kwa baraka za Baraza la Mawaziri ambalo mwenyekiti wake ni Rais, kwa hiyo uamuzi wote uliotoka hapo ni mali ya Rais.
“Lakini tiba ya yote haya ni katiba mpya. Watu wameiba kwa kupitisha mikataba yenye faida kwao na wengine walifikia hatua ya kujiuzia migodi, kwa hiyo kukiwa na katiba mpya ambayo inaruhusu kiongozi wa juu wa nchi ambaye ametumia vibaya madaraka yake kushtakiwa, itawaogopesha kufanya uhuni huu,” alisema Lowassa.
Aidha Lowasaa alisema tatizo katika mikataba ya madini aliliona tangu akiwa ndani ya CCM, na alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu aliita kampuni za madini na kujadiliana nao.
“Angalau wakaongeza malipo ya mirabaha, lakini bado mikataba ile ilikuwa mibaya na dhamira yangu wakati natangaza kuwania urais ndani ya CCM ilijulikana wazi kuwa ni kwenda kuifumua mikataba ile, ndiyo maana wakubwa wale wakasimama kidete kuhakikisha sipenyi pamoja na kwamba niliungwa mkono na idadi kubwa ya wanachama.
“Nilipotoka CCM hili suala nililiweka wazi kabisa kuwa nikiingia madarakani nitaunda tume ya kuchunguza mikataba hii na pale itakapoonekana kuwa taifa linanyonywa nitaifutilia mbali.
“Suala hili pia tulilisema sisi (Ukawa) katika mikutano yangu yote kule Kanda ya Ziwa kwenye migodi, kwa hiyo anachokifanya Rais Magufuli ni kile nilichoahidi, nampongeza kwa hilo,” alisema.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa aliyonayo Rais Magufuli ni kuhakikisha anamaliza suala hilo kwa kuwaomba radhi Watanzania kwa niaba ya chama chake (CCM) kwani awamu mbili zilizotangulia ndiyo chimbuko la matatizo yote hayo.
“Awe muungwana kuwaomba radhi Watanzania, wabunge wa upinzani, hawa kina Tundu Lissu na wenzake Zitto Kabwe, John Mnyika na wengine, walipiga sana kelele na wameendelea kupiga kelele kutaka mikataba yote ipelekwe bungeni.
“Lakini hata miswada ile ya dharura ya marekebisho ya sheria ya madini ilipopelekwa bungeni, walipinga kwa hoja nzito na u-CCM bila kuangalia masilahi ya wananchi ikapitishwa kwa makofi mengi kweli kweli, sasa leo hii kamati hii ya Rais Magufuli imewaumbua wana CCM wote,” alisema.
Aidha Lowassa alisema pamoja na hatua hiyo nzuri ya rais kuunda tume hiyo, lakini anashangaa kuona anaanza kampeni ya kuwaaminisha wananchi kuwa upande wa upinzani wanatetea wizi huo na kuhoji wanatetea vipi wakati wabunge wao ndio wanapiga kelele kila uchao kupinga mikataba ya aina hiyo na ushahidi upo kwenye hansard za Bunge. 
MJADALA WAKOLEA
Mbali na Lowassa, baadhi ya wasomi, wanasheria na watu wa kada mbalimbali wamesema kupeleka mikataba ya madini bungeni haitasaidia kubadilisha masharti ya mikataba iliyopo baina ya Serikali na Kampuni ya Acacia.
Mmoja wa wanasheria ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini kwa sababu maalumu, alisema sheria inafanya kazi kwa kwenda mbele, hivyo marekebisho yoyote yanayotarajiwa kupelekwa bungeni hayataihusu Acacia.
Alisema marekebisho ya sheria mpya yataihusu mikataba mingine nchi itakayoingia, si iliyopo kwani huwezi kubadilisha masharti ya sheria katikati ya mkataba na kama kweli Serikali imedhamiria basi ipeleke mikataba yote si ya madini pekee.
“Kama kuna dhamira ya dhati, basi wapeleke mikataba yote ya gesi, madini na ya uvuvi wa samaki wa bahari kuu inayoendelea katika bahari zetu ili wabunge na wanasheria washauri.
“Tatizo tuna mkataba wa Bolivia ambao tulisaini ili yasitokee ya Nyerere (Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere) ya kuwanyang’anya watu mali zao, ambapo huwezi kuchukua hatua ambazo zitaathiri haki za watu,” alisema.
TRA, CCM WAVUTA PUMZI
Aidha Mamlaka ya Mapato (TRA) imegoma kuzungumzia utaratibu iliyokuwa inautumia kutoza kodi kwa Acacia, huku CCM ikisita kuweka wazi hatua zitakazochukuliwa kwa makada wake waliotajwa katika sakata hilo.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema: “Siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu liko katika ngazi za uchunguzi wa vyombo vya dola, nitakuwa navunja sheria, siwezi.”
Akizungumzia makada wa CCM waliotajwa kuhusika katika mikataba ya madini, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, alisema wanasubiri matokeo ya uchunguzi wa vyombo vya dola.
“Rais ameelekeza vyombo vyote kila kimoja kwa nafasi yake, kuwahoji na baada ya hapo ndiyo chama kitakaa vikao kujadili, ni mapema mno, siwezi kuhukumu,” alisema Polepole. 
LISSU AKUMBUSHIA YA 1997
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliandika katika ukurasa wake wa facebook kuwa Machi 1997, Bunge lilipitisha sheria mbili kwa siku moja kwa kutumia hati ya dharura.
Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), alisema Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali za fedha ya mwaka 1997 ilifuta au kupunguza kodi nyingi kwa kampuni za kigeni za madini.
Alisema Sheria ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 1997 iliwapa wawekezaji wa kigeni ulinzi mkubwa na manufaa mengi kama vile kuondosha nje fedha na faida yote wanayopata kwa uwekezaji wao nchini.
Lissu alisema mwaka 1998, Bunge lilipitisha Sheria ya Madini ambayo ilitamka kwamba mwenye miliki ya madini na fedha yote itokanayo na mauzo ya madini ni mwenye leseni ya kuchimba madini hayo.
“Sheria hizo tatu nimeziita ‘utatu usio mtakatifu’ (Unholy Trinity) katika maandiko yangu mbalimbali, na nimezichambua sana tangu mwaka 1999 nilipoanza harakati dhidi ya sekta ya madini ya aina hii.
“Kwa miaka yote hii hadi leo, sheria hizi za madini zimeungwa mkono na kupigiwa debe na kila kiongozi na mbunge wa CCM, Magufuli ‘included’.
“Watu hawa, ‘with very few and minor exceptions’, ndio wamekuwa washangiliaji wakubwa wa unyonyaji wa makampuni ya kigeni ya madini katika nchi yetu. Watu hawa na chama chao ndio wamefaidika sana na utaratibu huu katika sekta ya madini.
“Wachache tuliopinga utaratibu huu tuliitwa kila aina ya majina mabaya na uzalendo wetu ulihojiwa kama ulivyohojiwa juzi na Rais Dk. Magufuli.
“Kwa mfano, Rais Mkapa alidai wakati anazindua mgodi wa Bulyanhulu, kwamba upinzani wetu ulikuwa ni ‘ujinga uliofichama katika kivuli cha taaluma.’
“Baadhi yetu, kama mimi na Dk. Rugemeleza Nshala, tulikamatwa na kushtakiwa mahakamani kwa uchochezi. Tulikabiliwa na kesi hiyo kuanzia Mei mwaka 2001 hadi 2008 ilipofutwa kwa kukosekana ushahidi.
“Kama ilivyokuwa wakati wa Mkapa mwaka 2001, leo pia Rais Magufuli ametukebehi na kuahidi kutushughulikia ‘tukiropoka’ nje ya Bunge.
“Tunaambiwa ni lazima tumuunge mkono Rais wetu katika hii ‘vita ya uchumi’. Ni sheria ipi ya Tanzania inayotulazimu kumuunga mkono Rais wetu hata kama tunaona amekosea?” alisema Lissu.
Alisema inashangaza kwa hatua ya Rais Magufuli kuruhusu Kampuni ya Acacia ambayo wanadai haikusajiliwa kuendelea kuchimba, kusafisha na kusafirisha nje ya nchi dhahabu kutoka Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara Tarime.
Lissu alisema wakati mapambano ya vita ya uchumi yakiendelea, dhahabu yote inayochimbwa katika mgodi mkubwa kuliko yote nchini wa Geita inaendelea kuchimbwa, kusafirishwa nje ya nchi.
LWAITAMA
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Azaveli Lwaitama, alisema anashukuru Rais Mgufuli ameliona tatizo katika mikataba ya madini, lakini akamtaka kutaja sababu za nchi kufikia hapo.
“Kilichotufikisha hapa ni katiba inayompa rais madaraka makubwa na wateule wake, tuweke katiba ambayo itamfanya rais adhibitiwe na Bunge, mawaziri wasiwe sehemu ya Bunge,” alisema.
Dk. Lwaitama alisema cha kufanya kwa sasa ni kuwa na demokrasia ya kweli kwani marais waliopita walipuuza upinzani, uteuzi wa rais uidhinishwe na Bunge na kurudisha elimu ya juu iwe inalipiwa na Serikali ili watu wawe wazalendo.
 PROFESA SEMBOJA
Mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Hajji Semboja, alisema hajaona jipya katika ripoti hiyo labda hatua ya kuwataja wezi na kuwapeleka mahakamani na takwimu, lakini vingine vyote vimo katika ripoti za kwanza ambazo zote zinasema migodi haifai.
“Nilitegemea ingekuwa kama Azimio la Arusha, kwamba kimebadilishwa hiki na hiki na tunataka kwenda hivi.
“Tatizo ni mfumo tulio nao, tunataka kusomesha watoto, kujenga reli na barabara tunategemea fedha kutoka nje, ni ujinga.
“Mali ya Mtanzania ni ya Watanzania wenyewe, Waarabu wanaringa kwa petroli wakati sisi tuna gesi na madini zaidi ya 10, lakini sisi ni masikini zaidi ya Waarabu, kama tutaendelea na mfumo huu tutaendelea ‘kupigwa’, ndiyo maana mwaka 1980 Mwalimu Nyerere alikataa misaada kutoka nje,” alisema Profesa Semboja.
 KINYONDO
Mchambuzi kutoka Taasisi ya REPOA, Dk. Adel Kinyondo, akizungumza juzi katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), alisema pamoja na kwamba Tanzania ina wataalamu, lakini kwenye suala la uzalendo walipwaya.
“Lazima tukumbuke pia katika zama za miaka ya 90 wakati bado tunapokea zile sera kutoka katika benki na zile taasisi kutoka Washington, tulikuwa tunashauriwa kwenye mambo mengi kwa sababu zile jumuiya kubwa kubwa zilikuwa na sauti kubwa ya namna gani ile mikataba iwe. Mwisho wa siku ile mikataba ikatuumiza sana,” alisema Dk. Kinyondo.
Kuhusu usajili wa Acacia, alisema ni jambo linaloshangaza kwamba kama hawakusajiliwa imeonekanaje kuwa wanadaiwa.
“Ni kitu kinashangaza, kama hawajasajiliwa japo wao wamekataa, unapata kigugumizi waliwezaje kuonekana kama wanadaiwa. Hii kidogo inaleta ukakasi,” alisema.
Kuhusu Rais Magufuli kusema kwamba endapo kampuni hizo zitakuwa tayari kutubu watakaa meza moja, alisema mkuu huyo wa nchi yuko sahihi kwa sababu wakati mwingine ni bora kukaa meza moja kuliko kwenda kwenye hizo mahakama za kimataifa, kwani ni vigumu kupata ushindi hata tukiangalia maeneo mengine.
 MTATIRO
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Julius Mtatiro, alisema ni jambo linaloshangaza kwamba pamoja na kamati kueleza kuwa Acacia haitambuliki, waliisajili wenyewe kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na watu wakanunua hisa.
Alisema pamoja na kuwa Rais ameambiwa na kamati kuwa kampuni hiyo haitambuliki, lakini kwenye majumuisho yake ameeleza kuwa zuio la makinikia kwenda nje linaendelea, huku kampuni hiyo ikiendelea kuchimba madini.
 WALIOTAJWA WAZUIWA SAFARI ZA NJE
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amewataka wote waliotajwa kwenye ripoti hiyo ya pili wasiruhusiwe kutoka nje ya nchi isipokuwa kwa ruhusa.
“Hakuna uzalendo zaidi ya kulinda rasilimali za taifa, hakuna utetezi wa wanyonge zaidi ya kulinda rasilimali zao. Hongera Rais kwa uzalendo wa vitendo kwa taifa letu.
“Naelekeza wote waliotajwa kuhusika hakuna kutoka nje ya mipaka ya nchi yetu isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka serikalini. Vyombo vitekeleze maagizo ya Rais kwa utimamu,” aliandika katika ukurasa wake wa Twitter.
ELIZABETH HOMBO NA ESTHER MBUSSI-MTANZANIA DAR ES SALAAM

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
أحدث أقدم