Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JUMUIYA YA WAZAZI YALAANI MAUAJI YA WANANDOA

JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imelaani migogoro katika ndoa inayosababisha ongezeko la matukio ya mauaji miongoni mwa wanandoa hali inayotishia ustawi wa watoto na kuchangia ongezeko la watoto waishio katika mazingira magumu.

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi kitaifa, Burhan Rutta alisema, Jeshi la Polisi na jamii kwa jumla zikiwamo taasisi za dini, waongeze ushirikiano kubaini dalili za maisha hatarishi ili kunusuru mauaji kutokea. Wakati akisema hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wajane Tanzania (Tawia), Rose Sarwatt alisema jana kuwa, vurugu na mauaji miongoni mwa wanandoa yanayoelezwa kusababishwa na wivu wa mapenzi, ni matokeo ya baadhi ya watu kuingia katika ndoa kwa kuvutwa na maslahi binafsi, badala ya upendo.

“Wengi siku hizi wanaingia katika ndoa wakisukumwa na maslahi binafsi na kwamba kuna kitu anakwenda kukipata. Mambo yakiwa tofauti, anaamua kuishi na kufanya lolote kwa sababu haoni kutimia kwa matarajio yake,” alisema Rose. Akaongeza kuwa, kinachoelezwa kuwa wivu wa mapenzi, kimeficha mambo mengi ndani yake likiwamo hasa la mtu kukosa yale aliyotarajia kuyakuta hasa mali na tamaa na mvuto wa mwonekano wa nje. Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM alisema: “Jambo hili la ukatili na hata mauaji miongoni mwa wanandoa lipigiwe kelele na watu wote.

vyombo vya dola viwatafute na kuwakamata wanaofanya mambo hayo na kukimbia ili wapatikane na kufikishwa mbele ya sheria.” Pia aliitaka jamii ya Watanzania kubadilika na kuutanguliza utu, badala ya maamuzi mabovu yanayosababisha vifo na kuwaweka watoto katika maisha magumu huku taifa likipoteza nguvu kazi. Hivi karibuni mkazi wa Kijiji cha Muriti wilayani Ukerewe, Melikiad Misana (50) alifariki dunia wakati akikimbizwa hospitali baada ya mkewe Bukherehere William (25) kumchoma na kitu chenye ncha kali mgongoni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema tukio hilo lilitokea baada ya mwanaume huyo kumjeruhi mkewe huyo kwa kuchoma na kitu chenye ncha kali kwenye mikono yake na tumboni kiasi cha kusababisha utumbo wa mwanamke huyo, kutoka nje. Tukio hilo lilikuja siku chache baada ya mkazi wa Kanyerere jijini Mwanza, Maximilian Ndegere (40), kumuua mkewe Teddy Patrick (38) kwa risasi na kisha yeye kujiua.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com