MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imemhukumu kutumikia kifungo cha maisha, Erick Mbugwa (22) baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka 14 (jina linahifadhiwa) kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo ilitolewa jana mahakamani hapo na Hakimu Mkazi, Flora Haule baada ya kujiridhisha na hoja za upande wa mashahidi uliowasilishwa mahakamani hapo bila kuacha shaka yoyote.
“Mahakama inakutia hatiani baada ya kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ambao ulikuwa na mashahidi watano pamoja na vielelezo vya daktari, hivyo inakuhukumu kutumikia kuifungo cha maisha jela kulingana na kosa ulilolifanya ili iwe onyo na fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizi,” alisema Hakimu Flora.
Alisema iwapo mshtakiwa hajaridhika na uamuzi huo kwenye shauri hilo namba 362 la mwaka 2016, ana haki ya kukata rufaa ndani ya siku 30.
Awali kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Wakili wa Serikali, Chences Gavyiole, alidai mahakamani hapo kuwa hakukuwa na kumbukumbu za mashtaka ya nyuma dhidi ya mshatakiwa na hivyo kuiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe onyo na fundisho kwa wote wenye tabia kama hizo kwani matendo ya namna hiyo yamekithiri kwenye jamii.
Katika utetezi wake juu ya kwa nini asipewe adhabu kali, Bugwa alidai kuwa anaomba asamehewe kwa kuwa haikuwa ni mipango yake na huku akisitiza kuwa hana cha kufanya na badala yake anamwachia Mwenyezi Mungu ndiye atakayemlipia.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Mbugwa ambaye ni mkulima na mkazi wa Chanika, anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Septemba 8 na Novemba 6, mwaka jana maeneo ya Chanika jijini Dar es Salaam ambako alimlawiti mvulana wa miaka 14 kinyume cha sheria.
Na FARAJA MASINDE-MTANZANIA -DAR ES SALAAM