NI kubwa kuliko. Ndivyo unaweza kusema baada ya Rais Dk. John Magufuli kulazimika kuagiza zaidi ya vigogo 10 wahojiwe na vyombo vya dola kuhusu ushiriki wao wa namna mbalimbali, ikiwamo kusaini mikataba ya madini na kuisababishia nchi hasara ya Sh trilioni 108.46 za mapato ya Serikali.
Vigogo hao ambao ni mawaziri watano wa zamani wa Nishati na Madini (akiwamo marehemu Abdallah Kigoda), wanadaiwa mbali na kusaini mikataba hiyo, pia kwa nyakati tofauti wakiwa katika nyadhifa zao, waliifanyia marekebisho mikataba hiyo na kuongeza muda wa leseni za baadhi ya migodi bila kufuata utaratibu kati ya mwaka 1998 na 2017.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana wakati akipokea ripoti ya kamati ya pili aliyoiunda Aprili 10, mwaka huu chini ya Mwenyekiti wake Profesa Nehemiah Osoro kuchunguza usafirishaji wa makinikia nje ya nchi iliyohusisha wajumbe wachumi na wanasheria.
Akifanya mchanganuo wa malori yenye madini ya dhahabu ambayo yanasafirishwa kwenda nje ya nchi, Rais Magufuli alisema kwa lori lenye tani saba kwa kiwango cha chini ni tani 177 hadi 304 kwa kiwango cha juu.
Alisema kwa lori hilo lenye tani saba, Serikali imepoteza Sh trilioni 132.56 hadi Sh trilioni 229.977 kiwango cha juu.
Mawaziri waliotajwa katika ripoti hiyo ni Dk. Abdallah Kigoda (marehemu), Daniel Yona, Nazir Karamagi, William Ngeleja na Profesa Sospeter Muhongo.
Wengine ni waliokuwa makamishna wa madini; Kamishna Paulo Masanja, Dk. Dalaly Kafumu na Kaimu Kamishna Ally Samaje.
Mbali na hao, pia wapo wanasheria wakuu wa Serikali ambao katika kipindi hicho walikuwa washauri wakuu wa Serikali katika masuala ya kisheria; Andrew Chenge, Johnson Mwanyika na manaibu wanasheria wakuu; Felix Mrema na Sazi Salula na wakuu wa Idara ya Mikataba; Maria Kejo na Julius Malaba.
Pamoja na mambo mengine, ripoti iliitaja mikataba mikubwa iliyoingiwa ama kufanyiwa marekebisho na mawaziri hao kuwa ni Mgodi wa Bulyanhulu, Mgodi wa Geita, North Mara, Pangea na mengine.
KIGODA
Ripoti inamtaja Dk. Kigoda kuufanyia marekebisho mkataba wa Mgodi wa Bulyanhulu ambayo hayakuwa na masilahi kwa taifa kwani Serikali ilipoteza haki ya umiliki wa hisa na kuinyima mapato kutokana na gawio.
“Awali katika mkataba huo, Waziri wa Nishati na Madini aliyekuwapo (mwaka 1998), alifanikiwa kujadiliana na kampuni hii ambapo ilizaa matunda kwa kuiwezesha Serikali kupata asilimia 15 za hisa.
“Hata hivyo, mkataba huo ulifanyiwa marekebisho Juni, 1999 na kusainiwa na Waziri wa Nishati na Madini aliyefuata, Dk. Abdallah Omari Kigoda. Marekebisho hayo yaliondoa asilimia 10 ya hisa ambazo Serikali ilikuwa inamiliki na kubakiza asilimia tano tu.
“Marekebisho mengine katika mkataba huo huo yalifanyika Oktoba, 1999, ikiwa ni miezi minne tu tangu marekebisho ya awali yafanyike. Marekebisho haya ya pili pia yalitiwa saini na Dk. Kigoda na kuondoa asilimia tano ya hisa za Serikali zilizokuwa zimebakia na hivyo Serikali kubaki bila hisa yoyote,” alisema Profesa Osoro.
Aidha, alisema katika marekebisho hayo, Serikali ilikubali kulipwa Dola za Marekani milioni tano ikiwa ni malipo ya mauzo ya hisa za Serikali na ilikubali kuendelea kulipwa kiasi cha Dola 100,000 kwa mwaka.
Hata hivyo, alisema kamati haikuweza kupata uthibitisho wa kufanyika kwa malipo ya jumla ya Dola milioni 6.8 ambapo pia kamati imeona marekebisho hayo ya mkataba yaliyofanywa na Dk. Kigoda.
Profesa Osoro alisema mkataba mwingine uliosainiwa na Dk. Kigoda ni ule wa Mgodi wa Geita ambao Serikali haikupata hisa yoyote katika kampuni na pia mkataba huo unatoa nafuu mbalimbali za kodi kwa kampuni, jambo ambalo linaikosesha Serikali kodi nyingi na mapato.
YONA NA KARAMAGI
Katika Mgodi wa Pangea, Profesa Osoro alibainisha ulikuwa na mikataba miwili ya uchimbaji madini. Mkataba wa kwanza ulisainiwa Desemba 2003 na Yona na wa pili ulisainiwa na Karamagi.
Alisema katika mikataba hiyo, Serikali haina hisa yoyote katika kampuni na pia mkataba huo unatoa nafuu kubwa za kodi kwa kampuni, jambo
ambalo linaikosesha Serikali kodi nyingi na mapato.
“Aidha, katika mkataba wa North Mara ambao ulisainiwa Juni 1999 na Yona na baadaye kufanyiwa marekebisho mwaka 2007 na Karamagi akiwa Waziri wa Nishati na Madini, Serikali haina hisa yoyote katika kampuni.
“Pia mkataba wa awali uliotiwa saini na Yona, Serikali ilitoa nafuu ya asilimia 15 ya nyongeza ya mtaji wa kampuni na kuifanya kampuni hiyo iwe inajilipa kwanza ili kurudisha mtaji wake na asilimia 15 iliyopewa na Serikali na hivyo kusababisha kampuni kutangaza hasara katika biashara kila mwaka.
“Jambo hilo limekuwa linaikosesha Serikali kodi ya mapato ambapo pia kamati imebaini kwamba marekebisho hayo ya kuondoa nafuu ya asilimia 15, bado malimbikizo ya hasara kutokana na nafuu ya kodi iliyokuwa imetolewa na Serikali iliendelea kudaiwa na kampuni hii,” alisema mwenyekiti huyo.
PROF. MUHONGO NA NGELEJA
Profesa Osoro alisema kuwa kamati yao imebaini kuwa Profesa Muhongo na Ngeleja, kwa pamoja wamehusika katika uongezaji wa muda wa leseni (renewal) wa maeneo ya uchimbaji madini kinyume cha sheria na bila kuzingatia masilahi ya taifa.
Alizitaja kampuni zilizoongezewa muda wa uchimbaji madini na mawaziri hao ni North Mara na Pangea Minerals Limited.
“Mikataba ya uchimbaji madini ina vifungu thabiti ambavyo vinazuia marekebisho ya sera na sheria kuathiri masharti yaliyomo katika mikataba ya uchimbaji madini.
“Kamati inaona kuwa masharti ya aina hiyo ni batili kisheria kwani waziri hawezi kurekebisha masharti ya leseni yaliyotolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni kwa kupitia vifungu vya mkataba wa uchimbaji wa madini.
“Kamati iliona kuwa pamoja na uwepo wa vifungu thabiti, Serikali haizuiliwi kurekebisha au kubadili sera na sheria zinazoweza kuathiri mikataba ya uchimbaji madini.
“Aidha, mkataba wowote ule hauwezi kisheria kuwa juu ya mamlaka asili ya nchi (state soveregnity) na masilahi ya umma kuhusu rasilimali zake za asili.
“Pia, mikataba hiyo ina vifungu vinavyoruhusu Serikali na makampuni ya uchimbaji kujadili na kurekebisha sharti lolote la kimikataba. Hivyo, mikataba ya uchimbaji madini inaweza kurekebishwa,” alisema.
ACACIA FEKI
Pamoja na mambo mengine, katika matokeo ya uchunguzi wake, kamati ilibaini kuwa Kampuni ya Migodi ya Acacia si halali na inafanya kazi nchini kinyume cha sheria kutokana na kutosajiliwa na Msajili wa Kampuni (Brela).
Profesa Osoro alisema licha ya kutosajiliwa, kampuni hiyo pia haina hati ya utambuzi (certificate of compliance) kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni, Sura ya 212.
“Kamati pia imebaini kuwa Kampuni ya Acacia Mining Plc, ambayo inajinasibisha kuwa mmiliki wa makampuni ya Bulyanhulu Gold Mines Ltd, North Mara Gold Mine Ltd na Pangea Minerals Ltd, haikuwahi kuwasilisha nyaraka wala taarifa yoyote kuonesha kuwa kampuni hiyo ni mmiliki wa makampuni hayo wala kuwa na hisa katika makampuni hayo.
“Kwa kuwa Acacia Mining Plc haina usajili wala utambuzi wa kisheria nchini Tanzania, haina sifa ya kupata leseni, kuchimba wala kufanya biashara ya madini nchini Tanzania,” alisema Profesa Osoro.
UDANGANYIFU USAFIRISHAJI WA MAKINIKIA
Aidha, kamati ilibainisha udanganyifu katika uuzaji na usafirishaji wa makinikia nje ya nchi ambako husafirishwa kwa madai ya kwenda kuchenjuliwa, lakini ukweli ni kwamba husafirishwa ikiwa tayari imeshauzwa.
Kamati pia ilibainisha kuwa kampuni za Bulyanhulu na Pangea ndizo wazalishaji na wauzaji wa makinikia nje ya nchi.
“Kwa mujibu wa mikataba ya mauzo ya makinikia baina ya makampuni hayo na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi, makinikia husafirishwa kutoka Tanzania yakiwa yameshauzwa na hupelekwa nje ya nchi kwa madai ya kwenda kuchenjuliwa kupitia bandari za Dar es Salaam na Tanga.
“Makinikia hayo hupelekwa nchi za China, Japan na Ujerumani, yakiwa kwenye makontena yenye urefu wa futi 20 na wastani wa tani 20 kila moja. Wafanyabiashara wa makinikia ni makampuni yaitwayo Aurubis AG na Aurubis Bulgaria ADM, Mark Rich Co. Investment AG na Pan Pacific Copper Co. Limited kutoka nchi za Ujerumani, Uswisi na Australia,” alisema Profesa Osoro.
Alisema mauzo hayo ya makininkia hufanywa kwa mujibu wa mikataba ya uchimbaji wa madini kati ya Serikali na makampuni ya uchimbaji madini ambapo kutokana na taarifa za kiuchunguzi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mauzo ya makininkia hufanyika kupitia Ofisi ya Uhasibu ya makampuni hayo iliyopo Afrika Kusini.
“Kamati imebaini kwamba kifungu cha 51 cha Sheria ya Madini kinaruhusu mwenye leseni ya uchimbaji wa madini kufanya biashara ya madini, ikiwa ni pamoja na kuuza nje ya nchi.
“Kifungu hicho kinamtaka mwenye leseni ya uchimbaji kupata kibali cha kusafirisha madini kutoka kwa ofisa mwenye mamlaka atayethibitisha kwamba mrabaha stahiki umelipwa kwa Serikali.
“Mbali ya kupata kibali kinachoonesha malipo ya mrabaha, hakuna utaratibu mwingine maalumu katika biashara ya uuzaji na usafirishaji wa makinikia nje ya nchi. Aidha, kisheria makampuni ya madini yanapaswa kutoa taarifa sahihi kwa Serikali kuhusu aina, kiasi na thamani ya madini yaliyomo ili kuiwezesha Serikali kukokotoa na kutoza mrabaha stahiki,” alisema.
UDANGANYIFU WA WATUMISHI SERIKALINI
Akizungumzia ushiriki wa watumishi katika udanganyifu wa kutoa taarifa za uongo na kusaidia kampuni za madini kukwepa kodi, Profesa Osoro alisema wamelisababishi taifa hasara.
“Kwa kuzingatia nyaraka na taarifa mbalimbali za kiuchunguzi, kamati imeridhika kuwa baadhi ya watumishi wa Serikali, watumishi na wamiliki wa kampuni za madini, kampuni za usafirishaji na upimaji wa madini na kampuni zenyewe, zimetenda makosa mbalimbali ya kijinai, yakiwamo ukwepaji wa kodi, kutoa taarifa za uongo, kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu, uhujumu uchumi,” alisema.
Alisema kutokana na hatua hiyo, imelisababishia taifa hasara kinyume cha vifungu vya 18, 114 na 115 vya Sheria ya Madini ya 2010, vifungu vya 101 na 106 vya sheria ya kodi ya mapato, 2004 vifungu vya 79 na 82 vya Sheria ya Usimamizi wa Kodi, 2015 na kifungu cha 24 cha Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika sekta ya Madini Tanzania, 2015 kifungu cha 27 cha Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 na kifungu cha 203 cha Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, 2004.
UKWEPAJI WA KODI YA MAPATO
Akizungumzia ukwepaji kodi, Profesa Osoro alisema kamati pia ilibaini mauzo ya makinikia kwa wafanyabiashara na wachenjuaji nje ya nchi hayakufanyika kwa ushindani kutokana na kuonyesha vipindi virefu vya uhusiano wa kibiashara kwa kuzingatia nyaraka za mikataba baina yao.
Alisema masharti ya usafirishaji wa makinikia yalionyesha yanatakiwa kusafirishwa bure badala ya gharama za usafirishaji na mzigo au gharama ya bima na mzigo ambapo makinikia hayo yaliuzwa kwa wafanyabiashara wale wale na wachenjuaji wale wale wenye mahusiano ya kibiashara kama ilivyoonyeshwa katika mikataba ya mauzo ya makinikia baina yao.
“Madini yaliyouzwa nje ya nchi hayakuwa makinikia hasa, badala yake yalikuwa ni madini ya aina mbalimbali mahususi yaliyopatikana kutokana na uchenjuaji,” alisema.
Aidha, katika upandishaji wa gharama za uendeshaji migodi uchunguzi wa kisayansi wa mifumo ya kompyuta kupitia TRA, ulibaini kuwa gharama za utafutaji na upembuzi wa miamba yenye madini imejumuishwa kwenye gharama za mauzo na kwa sababu hiyo, kuathiri faida halisi ambayo ilipaswa
kutozwa kodi.
THAMANI YA MADINI KATIKA MAKONTENA
Pamoja na mambo mengine, Profesa Osoro alisema uchunguzi wa kamati ulibaini kuwapo takwimu mbalimbali za idadi ya makontena yaliyosafirishwa nje ya nchi kuanzia mwaka 1998 hadi Machi mwaka huu.
Alisema kamati iliamua kutumia takwimu kutoka Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa (TRA) kwa kuwa moja ya majukumu ya idara hiyo ni kukusanya takwimu za bidhaa zote zinazosafirishwa nje ya nchi kupitia bandari, viwanja vya ndege na mipaka ya nchi.
“Kutokana na chanzo hicho, idadi ya makontena yaliyosafirishwa yalikuwa 44,277 kwa kiwango cha chini na makontena 61,320 kwa kiwango cha juu kutoka kwenye vyanzo vyetu vya uchunguzi,” alisema.
VIWANGO VYA DHAHABU KATIKA MAKINIKIA
Aidha, viwango vya dhahabu vilivyobainishwa kwenye kamati ni wastani wa kilo 28 za dhahabu katika kila kontena.
“Kwa kutumia kiasi hiki cha dhahabu kwenye kila kontena katika makontena 44,277 yatakuwa na dhahabu kiasi cha tani 1,240, kiasi hiki kina thamani ya Sh trilioni 108.06 sawa na Dola bilioni 49.12.
Kwa kutumia kiwango cha juu cha dhahabu kwa kontena moja, kiasi cha dhahabu katika makontena 44,277 kitakuwa tani 2,103 ambazo thamani yake ni Sh trilioni 183.32 sawa na Dola bilioni 83.32,” alisema.
Hata hivyo, alibainisha thamani ya madini yote katika makontena 61,320 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi kati ya 1998 na 2017 kwa kutumia kiwango cha wastani ni Sh trilioni 183.597 sawa na Dola bilioni 83.45.
“Jumla ya thamani ya madini katika makontena 61,320 yaliyosafirishwa nje ya nchi kati ya 1998 na 2017, kwa kutumia kiwango cha juu ni Sh trilioni 380.499 sawa na Dola bilioni 144.77,” alibainisha.
MAPATO YALIYOPOTEA
Kamati pia katika uchunguzi wake ilibainisha upotevu wa kodi kati ya mwaka 1998 hadi mwaka huu ambayo Serikali ilipoteza ni Sh trilioni 108.46, ambazo ni sawa na bajeti inayokaribia miaka mitatu.
“Kiasi hicho ni kwa kiwango cha chini ambapo robo ya fedha hizo zingetosha kujenga reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza,” alisema.
UCHENJUAJI MAKINIKIA NJE YA NCHI
Profesa Osoro alisema kupitia mikataba ya mauzo ya makinikia kati ya makampuni ya uchimbaji na wachenjuaji, kamati imebaini Serikali si sehemu ya mikataba hiyo licha ya kuwapo na salio la kodi katika makinikia hayo.
“Aidha, mikataba hiyo haina masharti yanayozilazimu kampuni za uchenjuaji kutoa taarifa za uchenjuaji kwa Serikali au muuzaji.
“Kwa msingi huo, taarifa ambazo zimekuwa zikiwasilishwa kwa TMAA baada ya kuomba taarifa hizo kutoka makampuni ya madini, hazina ukweli na hazibebi takwimu sahihi kuhusu aina, kiasi na thamani ya madini yaliyochenjuliwa ambazo zingewezesha TRA kutoza kodi stahiki,” alisema.
MAPENDEKEZO YA KAMATI
Kutokana na ukiukwaji wa sheria za nchi kupitia kwa viongozi na watumishi mbalimbali ambao wamehusika kwa njia moja ama nyingine katika suala hili, kamati ilipendekeza uchunguzi ufanyike kwa mawaziri, manaibu waziri, watumishi, wanasheria na naibu wanasheria waliohusika na sheria ichukue mkondo wake.
Aidha, Brela ichukue hatua kwa Kampuni ya Acacia na Serikali iendelee kuzuia usafirishaji wa makinikia nje ya nchi hadi watakapolipa kodi.
Kamati pia imependekeza Serikali ianzishe wakala wa uchenjuaji nchini ili makinikia yasisafirishwe nje ya nchi na ifute utaratibu wa kupokea mrabaha baada ya kuuza.
“Kamati inashauri Serikali kupitia mwenendo wa watumishi kitengo cha walipakodi wakubwa TRA na mabaraza ya kodi kwa kutotolea uamuzi wa kodi kwa muda mrefu, Benki Kuu (BoT) ifuatilie malipo ya fedha za kigeni.
“Serikali kupitia wataalamu wapitie mikataba yote mikubwa na kufanya majadiliano na kuweka masharti yenye tija na pia sheria iweke wakala wa meli kuzuia utoroshwaji wa makinikia nje ya nchi,” alisema.
Na Esther Mbussi-MTANZANIA DAR ES SALAAM